MWILI WA MAWAZO KUAGWA KITAIFA KATIKA UWANJA WA FURAHISHA JIJINI MWANZA
Mkutano wa Naibu Katibu Mkuu Chadema Salum Mwalimu na Wanahabari Jijini Mwanza hii leo.
Na:Binagi Media Group
Mwili wa aliekuwa
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Mkoa wa Geita Marehemu
Alphonce Mawazo, kesho unatarajiwa kuagwa Jijini Mwanza kabla ya kusafirisha
kwenda Mkoani humo kwa ajili ya Mazishi.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema Salum Mwalimu, amesema Marehemu Mawazo
ataagwa Kitaifa kwa taratibu za chama hicho, katika uwanja wa Furahisha Jijini
Mwanza.
Amesema ratiba hiyo itatanguliwa na ratiba ya kifamilia ya kuuaga
mwili huo, ambayo itafanyika asubuhi Nyegezi Jijini Mwanza ambako ni nyumbani
kwa Mchungaji Charles Lugiko ambae ni baba mdogo wa Marehemu Mawazo hiyo ikiwa
ni baada ya mwili wake kutolewa katika Hospitali ya Rufaa Bugando
ulikohifadhiwa.
Mwalimu amebainisha kwamba mwili huo utasafirishwa hiyo kesho
kwenda Mkoani Geita kuanzia majira ya saa nane mchana ambapo wakazi wa Mkoa huo
pia watapata fursa ya kuuagwa kesho kutwa jumapili.
Ameeleza kwamba kuanzia majira ya saa mbili asubuhi, shughuli za
kuuaga mwili huo zitafanyika Kimkoa katika Uwanja wa Magereza Mjini Geita na
baadae kusafirisha kwenda Katoro ambapo wakazi wa Jimbo lake la Busanda
watapata fursa ya kuuaga mwili huo.
Mwalimu ametanabaisha kwamba, baada ya shughuli zote hizo
kukamilika, mazishi ya Marehemu Mawazo yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu
katika Kijiji cha Chikobe Jimbo la Busanda Mkoani Geita.
Shughuli zote hizo zinatarajiwa kuongozwa na Mwenyekiti wa Chadema
Taifa Freeman Mbowe, Viongozi waandamizi wa Chama hicho akiwemo Frederick
Sumaye, aliekuwa mgombea urais wa Ukawa Edward Lowasa, wabunge pamoja na makada
wa Chadema.
Ratiba za Mazishi ya Marehemu Mawazo ambae aliuawa Novemba 14
mwaka huu na watu wasiojulikana, zimejiri baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza
jana kuondoa zuio la Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza, lililokuwa zinazuia mwili
huo kuagwa Jijini Mwanza kutokana na hofu ya kiusalama pamoja na uwepo wa
mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambapo zuio hilo liliondolewa katika kesi
iliyofunguliwa na baba mlezi wa Mawazo, Mchungaji Charles Lugiko baada mvutano
mkali wa siku nne mahakamani hapo.
BONYEZA PLAY HAPA CHINI KUSIKILIZA
BONYEZA PLAY HAPA CHINI KUSIKILIZA
Naibu Katibu Mkuu Chadema, Salum Mwalimu akionyesha kibali kilichotolewa na Manispaa ya Ilemela ili kuruhusu ibada ya kumuaga Marehemu Mawazo Kufanyika kesho katika Uwanja wa Furahisha
Mkutano wa Naibu Katibu Mkuu Chadema Salum Mwalimu na Wanahabari Jijini Mwanza hii leo (hawapo pichani).
Kushoto ni Ezekiel Wenje na Kulia ni Grace Kihwelu ambae ni Mbunge Viti Maalumu Chadema Mkoani Kilimanjaro
Singo Kigaila Benson ambae ni Mkurugenzi wa Mafunzo Chadema (Kushoto) akiwa na Peter Mekele ambae ni Mwenyekiti Chadema Kanda ya Ziwa Victoria (Kulia)
Husna Amri Said ambae ni Mwenyekiti BAWACHA Wilayani Geita
Viongozi na Makada wa Chadema
Mkutano wa kutoa ratiba za kuuaga mwili wa Marehemu Mawazo kwa wanahabari Jijini Mwanza hii leo
Wanahabari
0 comments:
Post a Comment