TANZANIA YASAINI MKATABA WA KUBORESHA HUDUMA YA AFYA
PICHA TOKA MAKTABA |
Na Jacquiline Mrisho na
Nyakongo Manyama -MAELEZO
Serikali ya Tanzania imesaini
mikataba miwili na Serikali ya Uswisi ili kuendeleza na kuimarisha huduma za
kijamii nchini hasa katika Sekta ya Afya.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salam Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius
Likwelile amesema kuwa kupitia ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili, Serikali
ya Uswisi inaendelea kusaidia kuboresha Sekta ya Afya nchini hususani
kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
“Uswisi imesaidia Sekta
ya Afya kwa miaka 15 na mpaka sasa imeshachangia jumla ya shilingi billion
181.7 kuanzia miradi ya afya ianzishwe nchini” alisema Likwelile.
Aidha, Dkt. Likwelile aliongeza
kuwa Serikali ya Uswisi imelenga pia kusaidia kuimarisha utoaji wa huduma katika
idara ya Afya katika Serikali za Mitaa kwa kuzingatia usawa na ubora wa huduma
hizo hasa kwa wanawake,watoto pamoja na makundi yaliyotengwa hasa maeneo ya
vijijini.
Zaidi ya hayo, Dkt. Likwelile
amesema kuwa Serikali ya Uswisi itarajia kuungana na Serikali ya Tanzania
katika kuboresha sera za malipo kwa wafanyakazi wa Afya ili watoe huduma bora yenye
tija kwa jamii.
Kwa upande wake Balozi
wa Uswisi Nchini Tanzania Bi. Florence Tinguely Mattli amesema kuwa amefurahishwa
na utoaji bora wa huduma za Afya Nchini Tanzania ambazo zimekuwa zenye tija kwa
wananchi wanapokuwa wanahitaji huduma hizo kwa wakati.
Bi. Florence aliongeza
kuwa Serikali ya Uswisi kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya mkoa wa Dodoma umekuwa
wa kwanza kunufaika na mfuko huo ambapo mikoa mingine inayotarajiwa kunufaika
ni pamoja na Morogoro na Shinyanga ili kuboresha afya ya wanawake, watoto, vijana
wazee na watu wasiojiweza.
Naye Katibu Mkuu Wizara
ya Afya Dkt. Donan Mmbando alisema kuwa lengo la fedha hizo ni kuhakikisha
huduma za Afya zinawafikia watu wote wenye mahitaji hayo kwa wakati.
“Mchango huo wa fedha
umechangia sana katika kutekeleza malengo ya Millenia kwa kupunguza vifo vya
watoto kwa asilimia 4 kwa mwaka 2013 kwa kuboresha utoaji wa chanjo kwa watoto
na tiba sahihi ya ugonjwa wa Malaria kwa kiasi kikubwa”. Alisema Dkt. Mmbando
Pia Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Jumanne
Sagini amesema kuwa ameishukuru Serikali ya Uswisi kwa msaada walioupata na kuahidi kuwa fedha hizo zitatumiwa katika kuboresha
zaidi huduma ya Afya katika Mikoa iliyoongezwa kuanzia ngazi za Wilaya.
Mfuko wa pamoja wa Afya
ulianzishwa nchini kwa lengo la kusaidia kuboresha huduma za Afya kwa kushirikiana na Serikali ya Uswisi pamoja
na nchi zingine zilizoendelea ikiwemo Canada, Denmaki na washirika wengine wa
maendeleo.
0 comments:
Post a Comment