MTIBWA YAIVUA SIMBA "SHELA" LA MPINDUZI CUP
Wekundu wa Msimbazi Simba wamevuliwa ubingwa wa Mapinduzi Cup na kikosi cha Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa nusu fainali uliomalizika jioni ya Jumapili January 10, 2016 baada ya kulala kwa bao 1-0 lililokwamishwa wavuni na Ibrahim Jeba dakika ya 45 kipindi cha kwanza.
Simba walibanwa vilivyo na Mtibwa Siugar ambao walitawala eneo la katikati ya uwanja wakiongozwa na viungo wao hatari Ibrahim Jeba pamoja na Ibrahim Mohamed ambao kwa pamoja walizima mipango ya Simba katika muda wote wa mchezo.
Kipindi cha pili Simba walifanya mabadiliko kwa kuwangiza wachezaji watatu kwa mpigo Said Ndemla, Ibrahim Ajib na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambao mara nyingi wamekuwa wakicheza kwenye kikosi cha kwanza lakini kwenye mchezo wa leo walianzia benchi.
Madiliko hayo yalileta tija kwa Simba kwani mchezo ulibadilika na Simba kutengeneza mashambulizi kadhaa lakini sifa za pekee ziende kwa safu ya ulinzi ya Mtibwa ikiongozwa na golikipa wao Said Mohamed ambaye aliokoa michomo ya washambuliaji wa Simba.
Wakati dakika zikiyoyoma, kocha wa Simba Dylan Kerr alifanya tena mabadiliko kwa kuwaingiza Paul Kiongera na Abdi Banda lakini bado Jahazi lake ambalo tayari lilishaenda mrama halikuweza kurejesha matumaini.
Mtibwa wamelipa kisasi kutokana na kupata ushindi kwenye mchezo wa leo baada ya kupoteza mchezo wa fainali mbele ya Simba kwenye mashindano yaliyopita na hivyo Simba wamevuliwa rasmi ubingwa wa Mapinduzi Cup.
Wakali hao wa Morogoro watacheza mchezo wa fainali siku ya Jumatano, January 13 dhidi ya mshindi wa mechi kati ya Yanga dhidi ya URA ya Uganda.
-Shafi Dauda
0 comments:
Post a Comment