SERIKALI HAIJAFUTA VIPINDI VYA BUNGE TBC
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Mose Nnauye
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Serikali
imetolea ufafanuzi kuhusu taarifa za upotoshaji kwa umma kuwa imefuta
vipindi vya shughuli za Bunge kuoneshwa katika televisheni ya Shirika la
Utangazaji la Tanzania (TBC) kama zisemazo taarifa zilizozagaa mitaani.
Hayo
yamesemwa jana Mjini Dodoma na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na
Michezo Mhe.Nape Mose Nnauye wakati akiongea na wananchi moja kwa moja
kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini kutolea ufafanuzi taarifa za
upotoshaji juu ya TBC kufuta vipindi vya matangazo ya vikao vya Bunge.
Mhe.Nape
Moses Nnauye amesema Serikali haijafuta vipindi vya Bunge bali
ilichofanya ni kubadilisha muda wa kurusha vipindi hivyo kutoka muda wa
mchana na kuviweka usiku kwa lengo la kupunguza gharama za kurusha moja
kwa moja matangazo hayo ya Bunge na pia kuwapa fursa wananchi zaidi
kuangalia na kufatilia yanayoendelea Bungeni kwa kuwa muda wa usiku watu
wengi wanakuwa wamesharejea kutoka katika shughuli zao za ujenzi wa
taifa.
Ameongeza
kuwa Serikali imechukua uamuzi wa busara katika hili kwani TBC inatumia
Sh Billion 4.2 kwa mwaka kama gharama za urushaji wa moja kwa moja wa
matangazo hayo , hivyo itasaidia katika kubana matumizi ya shirika hilo
kwani fedha hizo hazipo katika bajeti ipewayo shirika bali ni fedha za
ndani zinazokusanywa na shirika hilo.
Aidha
amesema kuwa sio kitu kigeni kwa Bunge kutotangazwa moja kwa moja kwani
kuna baadhi ya mabunge katika nchi nyingine urekodiwa na kurushwa
baadae kama kipindi maalum cha Bunge,amezitaja baadhi ya nchi hizo kuwa
ni New Zealand, India, Malawi, Lesotho, Uingereza na Singapore.
Shirika
la Utangazaji la Tanzania (TBC) lilianza kurusha matangazo ya moja kwa
moja ya vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005
ila baada ya Serikali kukaa na kujadili kwa kina kuhusu gharama za
urushaji wa matangazo hayo moja kwa moja ikaamua kubadili mtindo wa
urushaji wa matangazo hayo kutoka matangazo ya moja kwa moja kwa siku
nzima kwenda kwenye mfumo wa kuyarekodi na kuyarusha katika kipindi cha
LEO KATIKA BUNGE.
0 comments:
Post a Comment