Saturday, 30 January 2016

YANGA ‘NDEMBENDEMBE’ MKWAKWANI, WACHEZEA 2-0 ZA COASTAL… SIMBA SC YAITANDIKA 4-0 AFRICAN SPORTS TAIFA


Hamisi Kiiza (kulia) akishangilia na Hajji Ugando kushoto leo Uwanja wa Taifa

Na Waandishi Wetu, DAR, TANGA
YANGA SC imepoteza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara leo, wakati mahasimu wao Simba SC wameibuka na ushindi mnono na kufufua matumaini ya ubingwa.
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Wekundu wa Msimbazi, SImba SC wameitandika African Sports ya Tanga mabao 4-0.
Ushindi huo, unaifanya Simba SC ifikishe pointi 36 baada ya kucheza mechi 16, sasa ikizidiwa pointi tatu tu na vinara, Yanga na Azam FC wenye pointi 39 kila mmoja. 
Simba ilipata bao lake la kwanza dakika ya 14 kupitia kwa mshambuliaji Mganda, Hamisi Kiiza aliyefumua shuti kali kwa mguu wa kushoto baada ya pasi ya beki Hassan Kessy.
Kessy mwenyewe akafunga dakika ya 30 kuipatia Simba SC bao la pili kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia pasi ya mshambuliaji Ibrahim Hajib na kumchambua vizuri kipa Zakaria Mwaluko.
Kiiza akamlamba chenga kipa Mwaluko baada ya kupata pasi ya kiungo Mwinyi Kazimoto kuifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 42.
Hajji Ugando akaifungia Simba SC bao la nne dakika ya 75 baada ya kupokea nzuri ya kiungo aliyekuwa katika kiwango kizuri siku ya leo.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Hassan Kessy, Abdi Banda, Juuko Murshid, Hassan Isihaka, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto/Mussa Mgosi dk86, Jonas  Mkude, Haji Ugando/Said Ndemla dk76, Ibrahim Hajib na Hamisi Kizza/Brian Majwega dk67. 
African Sports; Zakaria Mwaluko, Mwaita Gereza, Halfan Twenye, Juma Shemvuni, Rahim Juma, Mussa Chambega/Hussein Amir dk51, Ally Ramadhani, Pera Ramadhani, Hamad Mbumba, Rajab Isihaka na James Mendy/Mohammed Issa dk56.
Kocha wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm timu yake imechapwa 2-0 leo Tanga

YANGA YALOWA 2-0 MKWAKWANI;
Yanga SC imefungwa mabao 2-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na matokeo hayo yanawafanya wabaki na pointi zao 39 baada ya kucheza mechi 16, sawa na Azam FC iliyocheza mechi 15.
Coastal Union walipata bao lao la kwanza dakika ya 27 kupitia kwa beki wa zamani wa Simba SC, Miraj Adam aliyefunga kwa shuti la mpira wa adhabu lililomparaza mikononi kipa Deo Munishi ‘Dida’ kabla ya kutinga nyavuni.
Refa Andrew Shamba wa Pwani aliwapa nafasi ya kupiga faulo Coastal Union, baada Miraj Adam mwenyewe kuangushwa na beki wa Yanga, Kelvin Yondan nje kidogo ya boksi.
Mshambuliaji chipukizi, Juma Mahadhi aliifungia bao la pili Coastal Union dakika ya 62 baada ya pasi nzuri ya Hamad Juma.
Bao hilo liliwavunja nguvu kabisa wachezaji wa Yanga SC na kujikuta wanacheza bila malengo. Refa Andrew Shamba alimtoa kwa kadi nyekundu beki wa Yanga, Kevin Yondan dakika ya 100.
Awali, dakika ya 97 Shamba alijichanganya kwa kumuonyesha kadi nyekundu Said Jeilan badala ya njano.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deogratias Munishi, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondan, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe/Paul Nonga dk76, Donald Ngoma na Deus Kaseke/Issoufou Boubacar dk80.
Coastal Union; Fikirini Bakari, Hamad Juma, Adeyoum Ahmed, Said Jeilan, Miraji Adam, Sabo Youssouf, Juma Mahadhi/Omar Wayne dk86, Ayoub Yahya/Mtenge Juma dk97, Chidiebele Abasarim, Ally Ahmed  na Ismail Mohammed.
-BINZUBERY


MATOKEO NA RATIBA LIGI KUU YA VODACOM TZ BARA
Januari 30, 2016 Coastal Union 2-0 Yanga SC Simba SC 4-0 African Sports JKT Ruvu 0-0 Majimaji Mwadui FC 1-0 Toto Africans Kagera Sugar Vs Mbeya City Kesho; Januari 31, 2016 Mgambo JKT Vs Ndanda FC Mtibwa Sugar Vs Stand United

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA