EPUKA MAKOSA HAYA 7 ILI KUANZA SIKU VIZURI
Kila siku ni nafaasi nyingine ya kuleta maendeleo kwako, familia
yako, na kwa taifa kwa ujumla. Waswahili wanasema nyota njema huonekana
asubuhi, je unaanza siku vizuri?
Lakini pengine ni vizuri kuuliza, siku nzuri inaanzaje? Kwa
mtazamo wangu mie ni kuwa, siku nzuri huanza baada ya kupata usingizi
mzuri kwa masaa muafaka – masaa 6 hadi 8. Vingine hufuata baada ya hapa,
maana usingizi ni kitu muhimu kuliko chochote kile.
Je kuna vingine zaidi?
Bila shaka. Kuna vingine vingi muhimu vya kuzingatika kwa siku yako.
Katika mada yetu ya leo tunaangalia kasumba 7 muhimu za kuepuka ili kuwa
na siku njema yenye mafanikio.
1. Kusongeza alarm mbele
Au ningeweza kusema – kutokulala vizuri. Mie sishauri kabisa kulala
na alarm, maana kuamka kwa kutega alarm inaonyesha jinsi gani ambayo
hupati kulala vizuri usiku. Kawaida mtu anatakiwa kulala masaa 6 hadi 8.
Unapotega alarm inaonyesha unalala muda mfupi kupita haya masaa, ambayo
ni mbaya kiafya.
Sasa, inapobidi kulala na alarm, hakikisha hausogezi muda mbele. Pale
alarm inapolia tu amka na anza siku yako vizuri. Mchezo wa kusogeza
mbele dakika 5 au 10 zitakuharibia mood yako mapema, hivyo bora amka na
anza siku.
2. Unaoga maji ya moto
Je unapenda kuoga maji ya moto asubuhi ? Hili ni kosa kwa sababu kuu mbili.
- Kwanza, maji ya moto sana si mazuri kwa afya ya ngozi yako - hufanya ngozi kuzeeka mapema.
- Pili, utafiti unaonyesha kuwa kuoga maji ya moto kunakufanya ujihisi uchovu na usingizi zaidi. Hivyo unaweza kuhisi kurudi kitandani kuendelea kulala.
Njia mbadala ni kuoga maji ya uvuguvugu. Haya ni maji yanayokupa
nguvu kuanza siku. Kama unataka kuoga maji ya moto, basi subiria usiku
ili upate kulala vizuri zaidi.
3. Unasahau kunywa maji
Watu wengi wana kasumba ya kunywa kahawa balada ya maji wakishaamka.
Pengine ni kasumba kuwa kahawa huwafanya wajisikie vizuri na kuwapa ari
ya kufanya kazi zaidi. Lakini si kweli. Maji ndio kitu muhimu zaidi
asubuhi maana hukupa nguvu zaidi na kukufanya kuwa na ari ya kufanya
kazi zaidi. Badilisha mwenendo, badala ya kahawa, anza na chai. Muhimu
zaidi, kama utaweza kunywa maji ya limao, faida zake ni nyingi kama ilivyoelezewa hapa.
4. Unaacha staftahi
Je wewe ni mtu wa kudharau kupata kifungua kinywa kila asubuhi ? Basi
jua kuwa hii siyo tabia nzuri. Kifungua kinywa ni muhimu sana mwilini
sababu inakata njaa na kuupa mwili nguvu iliyopoteza usiku kucha wakati
umelala. Unaweza kuangalia zaidi kwenye makala yetu ya nyuma hapa.
5. Unawaza sana majukumu
Usiwe mtu wa kuwaza majukumu mengi sana yanayokukabili kwenye siku
yako mara tu ukishaamka. Badala ya kuwaza majukumu na kazi inayokukabili
kwa siku yako, anza kwa shukrani na kufikiria vitu unavyopenda, ni njia
nzuri ya kuamka asubuhi ili kuanza siku kwa amani na mtazamo chanya.
6. Unaanza mazoezi mara tu baada ya kuamka
Sikatai, mazoezi ni njia nzuri ya kupata nguvu mwilini, lakini siyo
jambo la kwanza kulifanya mara tu baada ya kuamka. Unatakiwa kufahamu
kuwa kila kitu kitaenda sawa kama utaanza kwa kujali mwili wako, hivyo
pata chakula au kunywa maji ya kutosha. Mazoezi yatafuata baadae.
7. Kutunza mwili wako
Wengi wanapenda kukurupuka na kwenda kazini au shule bila kujali
muonekano wao. Hii siyo nzuri. Ili kujiamini na kuwa na Amani, ni vizuri
kama utachukua muda kujali mwili na afya yako. Tengeneza nywele, vaa
vizuri na tembea kwa kujiamini. Hii ni njia bora ya kukufanya kuanza
siku kwa Amani na mtazamo chanya zaidi.
Je wewe unafanya kosa gani katika haya?
-Nakutakia siku Njema
0 comments:
Post a Comment