YALIYOJIRI USIKU WA EPL: LEICESTER CITY YAZIDI KUJICHIMBIA KILELENI
Jammie Vardy akipasua katikati ya mabeki wa Liverpool jana Mamadou Sakho (kushoto) na Dejan Lovren (kulia) jana PICHA ZAIDI GONGA HAPA
Vardy akifunga bao maridadi kabisa mbele ya mlinzi wa Liverpool Dejan Lovren |
TIMU ya Leicester City imetanua mbawa zake kileleni mwa Ligi Kuu ya England kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Liverpool Uwanja wa King Power usiku jana. Shukrani kwake mshambuliaji wa kimataifa wa England, Jamie Vardy aliyefunga mabao hayo dakika ya 60 na 71 na Leicester City sasa inafikisha pointi 50 baada ya kucheza mechi 24, ikifuatiwa na Manchester City yenye pointi zake 47. Bao pekee la Sergio Aguero dakika ya 16, limeipeleka Man City nyuma ya Leicester kufuatia kuilaza Sunderland 1-0 Uwanja wa Light, baada ya Arsenal kulazimishwa sare ya 0-0 na Southampton Uwanja wa Emirates. Matokeo hayo yanaifanya Tottenham Hotspur iliyoshinda 3-0 dhidi ya Norwich City iwe juu ya Arsenal nafasi ya tatu kwa wastani mzuri wa mabao baada ya timu hizo kulingana kwa pointi 45 kila moja.
Sergio Aguero akiifungia Man City bao pekee jana Uwanja wa Light PICHA ZAIDI HAPA
Manchester United imezinduka na kuitandika 3-0 Stoke City Uwanja wa Old Trafford, mabao ya Jesse Lingard dakika ya 14, Anthony Martial dakika ya 23 na Nahodha Wayne Rooney dakika ya 53. West Bromwich Albion imelazimishwa sare ya 1-1 na Swansea City, bao lake likifungwa na Salomon Rondon dakika ya 92 baada ya wageni kuanza kufunga kupitia kwa Gylfi Sigurdsson dakika ya 64 Uwanja wa The Hawthorns. Bournemouth imeshinda 2-1 ugenini dhidi ya Crystal Palace, mabao yake yakifungwa na Marc Pugh dakika ya 34 na Benik Afobe dakika ya 57 Uwanja wa Selhurst Park, wakati la wenyeji limefungwa na Scott Dann dakika ya 27 na West Ham United imeilaza 2-0 Aston Villa mabao ya Michail Antonio dakika ya 58 na Cheikhou Kouyate dakika ya 85 Uwanja wa Boleyn Ground.
Nahodha Wayne Rooney akishangilia usiku wa jana baada ya kuifungia Manchester United bao la tatu PICHA ZAIDI HAPA
Tottenham Hotspur imeshinda ugenini 3-0 dhidi ya Norwich City, mabao ya Bamidele Alli dakika ya pili na Harry Kane kwa penalti dakika ya 30 na dakika ya 90 Uwanja wa Carrow Road. Ligi Kuu ya England inaendelea leo kwa mechi mbili, Everton ikimenyana na Newcastle United Uwanja wa Goodison Park na Watford wakiwa wenyeji wa Chelsea Uwanja wa Vicarage Road kuanzia Saa 3:45 usiku.
Mesut Ozil alikaribia kufunga jana Uwanja wa Emirates dhidi ya Southampton PICHA ZAIDI HAPA
0 comments:
Post a Comment