Saturday 19 March 2016

NEC YAIGOMEA CUF, YASEMA HAITAMBUI CUF KUJITOA KATIKA UCHAGUZI

Kailima Ramadhani
Kailima Ramadhani
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema haitambui kujitoa kwa Chama cha Wananchi (CUF), katika uchaguzi wa Mbunge Jimbo la Kijitoupele hapa Zanzibar unaotarajiwa kufanyika Jumapili licha ya kuwa Tume imepokea barua rasmi toka kwa uongozi wa Chama hicho.
Mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya Taifa Bw. Kailima Ramadhani amesema Tume imefikia maamuzi hayo kutokana na ukweli kuwa barua hiyo ya CUF imechelewa huku maandalizi ya uchaguzi huo yakiwa yamekamilika na ni Wananchi tu kwa sasa Wanasubiriwa kwenda kupiga kura.
Aidha, Bw. Kailima ameeleza kuwa, kwakuwa karatasi za kupigia kura zilishachapishwa na kuwasili hapa nchini tayari kwa uchaguzi huo, zitaendelea kuwa na picha za Wagombea wa CUF hata kama wamejitoa katika uchaguzi huo.
Awali, wajumbe wa Tume ya Taifa ya uchaguzi wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji mstaafu Hamid Mahamood Hamid walitembelea katika vituo mbalimbali vya kupigia kura katika Jimbo la Kijitoupele ili kujiridhisha na maandalizi ya uchaguzi huo kabla ya uchaguzi kufanyika jumapili.
Tume ilibaini kuwepo kwa baadhi ya kasoro ndogo ndogo katika baadhi ya vituo vya kupigia kura ikiwa ni pamoja na kubanduliwa kwa karatasi zenye majina ya wapiga kura, mfano katika kituo cha Skuli ya sekondari Kinuni.
Jimbo la Kijitoupele lina jumla ya Wapiga kura wapatao 17,274 na vituo vipatavyo 53 vitatumiwa na wapiga kura ili kumchagua mbunge waJimbo la Kijitoupele siku ya Jumapili.
Sambamba na Uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Kijitoupele, marudio ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar Oktoba 25,2015 ambayo matokeo yake yalifutwa uatafanyika Jumapili hiyo pia.
Uchaguzi katika jimbo la Kijitoupele uliahirishwa mwaka jana kutokana na hitilafu ndogo ndogo zilizojitokeza katika karatasi za kupigia kura, kabla ya kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, 2015.
Na Clarence Nanyaro.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA