Thursday 7 April 2016

AL AHLY ‘WAFUKUZA’ WAANDISHI KWENYE MAZOEZI YAO



Na Prince Akbar wa BIN ZUBERY BLOG, DAR ES SALAAM
KOCHA Mholanzi wa Al Ahly ya Misri ameiongoza timu yake katika mazoezi jioni ya leo Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam, lakini Waandishi wa Habari wakazuiwa kuingia.
Al Ahly waliweka walinzi wao pamoja na walinzi wa Gymkhana kuhakikisha Waandishi wa Habari hawaingii katika mazoezi hayo.
Hata hivyo, mwandishi wa BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE alishuhudia mazoezi hayo kutoka nje ya uzio wa Gymkhana na kufanikiwa kupiga picha kadhaa kabla ya kuondolewa.
Al Ahly ipo nchini kwa ajili ya mchezo wa kwanza hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga SC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kocha Martin Jol (kushoto) akiongoza mazoezi ya timu yake leo Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam


Lakini kesho, klabu hiyo bora ya karne Afrika itafanya mazoezi yake Uwanja wa Taifa kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) timu wageni kuruhusiwa kufanya maZoezi Uwanja wa mechi siku moja kabla ya mechi.
Timu hiyo ya kocha Mholanzi, Maarten Cornelis Jol maarufu kama Martin Jol, kiungo wa zamani wa Bayern Munich ya Ujerumani, FC Twente ya Uholanzi, West Bromwich Albion na Coventry City za England mwenye umri wa miaka 60, iliwasili Dar es Salaam jana Alfajiri na kufikia katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam.
Kikosi kilichotua jana chini ya kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, Fulham za England, Hamburger SV ya Ujerumani na Ajax ya Uholanzi kinaundwa na makipa; Ahmed Abdul Monem, Mosaad Awad, Sherif Ekramy.
Mabeki; Ahmed Fathy, Bassem Ali, Mohamed Hany, Rami Rabia, Saad Samir, Ahmed Hagazy na Sabri Rahil.
Viungo; Amir El-Sulaya, Ahmed El El- Sheikh, Walid Soliman, Abdalla El Said, Hossam Ghaly, Hossam Ashour, Ramadan Sobhi na Momen Zakaria.
Washambuliaji; Malick Evouna, Emad Moteab na Amr Gamal.

Martin Jol akiongoza mazoezi ya timu yake leo Dar es Salaam
Martin Jol akizungumza na wachezaji wake leo Uwanja wa Gymkhana
Waandishi wa Habari walizuiwa kuingia ndani ya Uwanja wa Gymkhana leo
Kesho Al Ahly watafanya mazoezi Uwanja wa Taifa mwa mujibu wa kanuni za CAF
Wachezaji wa Al Ahly wakijiandaa kuanza mazoezi leo Gymkhana


Wenyeji, Yanga wameweka kambi katika hoteli ya Misali Sun Set Beach, Chake Chake kisiwani Pemba tangu Jumatatu na wanatarajiwa kurejea Dar es Salaam kesho.
Yanga ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm mwenye umri wa miaka 67, inatarajiwa kurejea kesho Dar es Salaam na kufikia katika hoteli moja ya kifahari ambako wataamkia kwenye mechi Jumamosi.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA