Thursday 28 April 2016

BALOZI SEIF AFUNGUA KONGAMANO LA KIBIASHARA KATI YA SHIRIKISHO LA URUSI NA JAMUHURI YA MUUNGAO WA TANZANIA JIJINI DAR ES SALAAM


Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Tanzania Mh. Charles Mwijage kulia amkimshindikiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuingia katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Mjini Dar es salaam kufungua Kongamano la Biasharfa kati ya Tanzania na Shirikisho la Urusi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua Kongamano la Kimataifa baina ya Shirikisho la Urusi na Tanzania lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara wa Shirikisho la Urusi Bwana Denis Manlurov akielezea nia ya Wafanyabiashara wa Urusi wanavyoshawishika kutaka kuwekeza miradi yao Nchini Tanzania kwenye Kongamano la Urusi na Tanzania. Mwenyekiti wa IPP Dr. Reginal Mengi kulia akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzikbar Balozi Seif mara baada ya ufunguzi wa Kongamano la Kibiashara la Urusi na Tanzania katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Dar es salaam.

Baadhi ya Wafanyabiashara wa Shirikisho la Urusi na wale wa Tanzania wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi Balozi Seif hayupo pichani wakati akilifungua Kongamno la Biashara vkati ya Pande hizo mbili.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wakuu wa Kongamano la Biashara kati ya Urusi na Tanzania mara baada ya kulifungua rasmi.

Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Vianda na Biashara wa Urusi Bwana
Denis Manlurov na kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Biashara,
Viwanda na Uwekezaji wa Tanzania Mh. Charles Mwijage, Waziri wa
Biashara wa Zanzibar Balozi Amina Salim Ali na Mwenyekiti wa IPP Dr.
Reginal Mengi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akifafanuja jambo mbele ya Wana Habari mara baada ya kulifungua Kongamano la Kimataifa la Biashara kati ya Tanzania na Urusi. 
Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati
umefika kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Shirikisho la Urusi
kulitumia soko la Kiuchumi liliopo Tanzania katika kuwekeza miradi yao
ya Kiuchumi itakayosaidia kuimarisha zaidi uhusiano wa kihistoria
uliopo kati ya Nchi mbili hizo rafiki.
Alisema kutokana na mabadiliko ya mfumo wa dunia uliojikita zaidi
katika masuala ya Teknolojia ya Kisasa  uhusiano wa Tanzania na
Shirikisho hilo unastahiki kwa sasa kuelekezwa zaidi katika Nyanja za
uwekezaji badala ya Siasa na utamaduni.
 
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akilifungua Kongamano la
Kibiashara kati ya Shirikisho la Urusi na Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa
Mwalimu Julius K. Nyerere Jijini Dar es salaam.
 
Alisema Tanzania hivi sasa imebahatika kuwa kituo maarufu katika
kuimarisha Biashara, Uchumi na uwekezaji ndani ya Mwambao wa Afrika
Mashariki na eneo la Ukanda wa Nchi za Sahara fursa ambayo inaweza
kutumiwa  vyema na wawekezaji wa Shirikisho la Urusi ambao Taifa lao
tayari limeshapiga hatua kubwa ya maendeleo katika sekta za Nishati,
madini, mafuta pamoja na anga.
 
Balozi Seif alisema katika kuendelea kuimarisha uhusiano wa pande hizo
mbili Watanzania watafarajika kuona wawekezaji wa Shirikisho hilo
wanatumia fursa ya kuanzisha miradi yao katika sekta ya Kilimo,
nishati, viwanda, usafiri pamoja na utalii.
 
Alifahamisha kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
tayari imeshatenga eneo kubwa la ardhi lenye  zaidi ya Hekta Milioni
43 kwa ajili ya shughuli za uwekezaji  wa sekta ya kilimo cha
umwagiliaji.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza ujumbe mkubwa wa
wafanyabiashara hao wa Shirikisho la Urusi waliongozwa na Waziri wao
wa Viwanda na Biashara kwa uamuzi wao wa kutembelea Tanzania kuangalia
fursa za uwekezaji.
 
Alisema uwekezaji wa wafanyabiashara wa Urusi unaweza kufanikiwa kwa
kiwango kizuri kwa vile kundi kubwa la wasomi wa Tanzania wamepata
taaluma ya Juu Nchini Urusi jambo ambalo wanaweza kutumiwa vyema na
Wafanyabiashara hao katika uanzishwaji wa miradi ya uwekezaji.
 
Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na uamuzi wa pande hizo
mbili kufanya  Kongamano la Biashara Mjini Dar es salaam kitendo
ambacho kitaongeza kasi ya ushirikiano kati ya Urusi na Tanzania
katika kupanua kasi ya biashara na uwekezaji.
 
Akizungumzia sekta ya Utalii inayoonekana kuongoza katika uchumi wa
Dunia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Tanzania imebahatika
kuwa na vivutio vingi vya utalii vinavyoweza kuwashawishi watalii wa
Urusi wakaamua kuitembelea Tanzania.
 
Yapo maeneo ya Kihistoria hasa Zanzibar, Misitu  pamoja na hifadhi za
Taifa zenye wanyama tofauti zinazoweza kutumiwa katika masuala ya
uwekezaji ambapo wafanyabiashara wa Nchi hiyo wanakaribishwa kuwekeza
kwenye eneo hilo muhimu.
 
Balozi Seif aliwahakikishia wawekezaji hao kutoka Urusi kwamba
Tanzania bado salama yenye utulivu na amani unaoweza kuwaletea tija na
mafanikio wataoamua kuanzisha miradi yao.
 
Mapema Waziri wa Viwanda na Biashara wa Shirikisho la Urusi Bwana
Denis Manlurov alisema Tanzania na Urusi zina uhusiano wa Kihistoria
wa muda mrefu uliojengeka katika uimarishaji wa Taaluma katika sekta
tofauti.
 
Bwana Denis alisema uhusiano huo ulitoa fursa kwa Watanzania wengi
waliomaliza masomo yao ya sekondari kupendelea kuongeza elimu yao ya
juu katika vyuo mbali mbali vikuu vya Urusi.
 
Waziri huyo wa Shirikisho la Urusi aliwahakikishia Watanzania kwamba
Nchi yake kupitia Makongamano  yanayoandaliwa kila Mwaka baina ya
Urusi na Mataifa ya Bara la Afrika {Russian – African Forum }
itaendelea kuunga mkono Nchi za Afrika katika harakati zake za
kujinasua na ukali wa maisha hasa kwa wananchi wao wa kipato cha
chini.
 
Akitoa salamu katika Kongamano hilo la  Kibiashara kati ya Shirikisho
la Urusi na Mwenyekiti wa IPP  Dr. Reginal Mengi alisema Watanzania
wana fursa ya kuingia ubia na Wawekezaji wa Urusi katika sekta za
Madini, Nishati, Kilimo, Utalii na hata Anga maeneo ambayo bado yana
rasilmali ya kutosha.
 
Dr. Mengi alisema ubia huo ambao umekuwa ukitangazwa mwa muda mrefu
katika azma ya kuimarisha uchumi wa Taifa utasaidia kuongeza pato la
Serikali na Wananchi sambamba na kuongeza fursa za ajira.
Mwenyekiti huyo wa IPP alielezea matumaini yake kwamba Tanzania
inatarajia kuwa ya Viwanda ili kuingia vyema katika uchumi wa kati
kati ifikapo mwaka 2020.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
28/4/2016.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA