BAJETI KUU YA SERIKALI 2016/2017 YAPITISHWA BUNGENI KWA ASILIMIA 100
Serikali ya Tanzania imepitisha bajeti ya shilingi trilion 29.5 kwa kupigiwa kura huku wabunge wa upinzani wakiwa wametoka nje wakiwa wameziba midomo yao kwa karatasi na plasta ikiwa ni ishara ya kuonesha kutoridhika na Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson wakigomea vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika huyo
Katika vikao vya Bunge la 11, wabunge wa vyama vya upinzani wamekuwa wakisusia vikao hivyo kwa takribani siku 23 sasa kwa madai ya kutokubaliana na ukandamizaji unaofanywa na Naibu Spika wa Bunge Dkt.Ackson Tulia.
Wakichangia bajeti hiyo, Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Mwijarubi Muhongo pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara Charles Mwijage wamesema bajeti hiyo inalenga kukuza uzalishaji.
Akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia katika Bajeti hiyo ikiwa ni pamoja na ya kuongeza fedha katika ofisi ya mkaguzi wa serikali CAG ili kutanua wigo wa ukaguzi pamoja na kuachana na mpango wa kuanza kuwakata kodi wabunge katika mafao ya kiinua mgongo ya Wabunge, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Phillip Mpango amesema msimamo wa serikali upo pale pale.
Kuhusiana na makato ya kodi kwenye mafao ya wabunge, Dkt Mpango amesema kuwa serikali imeamua kuwa itakata kodi hiyo kwa viongozi wote wa kisiasa wakiwemo wakuu wa wilaya, wakuu wa mkoa, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais pia, ili kuweka usawa katika makato ya kodi nchini.
Baadaye jioni wabunge walipiga kura mmoja mmoja kupitisha bajeti hiyo, ambapo wabunge wote 251 waliokuwemo bungeni walipitisha bajeti hiyo kwa kauli moja, ambapo kila mbunge alijibu "Ndiyo" akimaanisha anaipitisha bajeti hiyo.
Mapema Asubuhi mara baada ya dua, wabunge wa upinzani waliziba midomo yao kwa karatasi na Plasta na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge ikiwa ni ishara ya kuonesha kutoridhika na Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson.
Mbunge wa Vunjo Kupitia chama cha NCCR Mageuzi, Mhe. James Mbatia kwa niaba ya wabunge hao alisema hawataacha kulalamikia ukiukwaji wa sheria unaofanywa na kiti cha Naibu Spika.
0 comments:
Post a Comment