Baada ya tetesi za muda mrefu za Manchester United kumtaka kiungo mshambuiaji wa Borussia Dortmund, Henrikh Mkhitaryan hatimaye Dortmund imetoa taarifa kuhusu mchezaji huyo kuwa atajajiunga Man United kwa kitita cha Pauni Milioni 26.
Katika taarifa ambayo imetolewa na Dortmund imeeleza kuwa wamechukua uamuzi wa kumruhusu Mkhitaryan kujiunga Man United kwani akisalia katika timu hiyo 2017 ataondoka bure kwakuwa mkataba wake utakuwa umemalizika.
“Manchester United walituletea ofa kubwa lakini tuliikataa na tunatambua mchezaji atakuwa huru kuondoka 2017,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Dortmund, Hans-Joachim Watzke katika taarifa iliyotolewa na klabu na kuongeza.
“Borussia Dortmund inamtakia kila la heri Henrikh Mkhitaryan kwa msimu ujao kwa Ligi Kuu ya Uingereza na UEFA Europa League”
Mkhitaryan alitua Dortmund mwaka 2013 akitokea Shakhtar Donetsk kwa kitita cha Pauni Milioni 27.5 kipindi hicho Dortmund ikinolewa na Jurgen Klopp ambaye kwa sasa anainoa Liverpool.