NAMNA YA KUKABILIANA NA TABIA YA KUHUKUMU WATU WENGINE
Kuhukumu ni hali ya mtu mmoja kutoa maamuzi kuhusu mtu mwingine kutokana na mwonekano,matendo,tabia au imani yake kwa mtazamo hasi bila kuwa na taarifa za kutosha juu ya suala au mtu husika.
Wahukumu ni watu wenye tabia ya kujiona kuwa ni sahihi na bora zaidi kuliko wengine na mara nyingi wanatumia mitazamo yao,mapenzi na tabia zao kama vigezo vya kuwapimia wengine kama wako sawa au la.
Kwa watu hawa ni ngumu sana kuwafurahisha na kufanya sawa na wanavyotaka, ni ngumu kuwaridhisha kwasababu mara zote wanaangalia katika upande hasi na ndicho wanachokiona kwa kila mtu.
Mifano:
Umemwona mtu amkekonda baada ya kuugua kwa muda mrefu unahitimisha kuwa “Atakuwa na UKIMWI”
Umekutana na mtu katika ndege ana ndevu nyingi na ni wa asili ya Arabuni basi unahitimisha kuwa ni “Gaidi” na unaanza kumwepa na kumtenga.
Hii ni mifano ya kuhukumu wengine
Mambo Yanayosababisha Mtu Kuwa Mhukumu
Wataalamu wa saikolojia wanaeleza kuwa watu watoa hukumu wana matatizo ya akili yanayowafanya kukosa kujiamini na kushindwa kuona mambo toka upande wa pili,yaani wanashindwa kuvaa viatu vya mtu wanayemtazama na kumuhukumu.
Watu wanakuwa wahukumu kutokana na mapungufu ya tabia zao wenyewe kama ifuatavyo:
- Kukosa Kujimini
Mtu anapokuwa na hisia za kukosa kitu fulani,kuwa chini ya mwingine au kukosa nguvu kwa namna fulani basi inakuwa rahisi kuwahukumu wengine ili kuziba pengo ndani yake
- Wivu
Mtu anayemwonea wivu mwingine kwa kuwa anakitu fulani ambacho yeye hana au anatamani angekuwa nacho anakuwa na tatizo la kukosa raha na fahari juu yake mwenyewe,hali hii hupelekea kumfanya awe mwepesi wa kuwahukumu wengine wenye vile anavyokosa
- Kujiona Mkamilifu
Watu wanaojiona kuwa wanakila kitu kizuri,tabia njema,mali,elimu nk wana kawaida ya kufikiri wengine wanaupungufu na niwepesi kufanya maamuzi ya haraka juu yao
- Ubaguzi
Watu wenye tabia ya kubagua wengine kutokana na kabila,rangi,imani na tamaduni huwa na tabia ya kuhukumu wengine.
- Mtazamo Finyu
Mhukumu anakosa kujua kuwa kuna namna tofauti za kuona na kuangalia jambo moja na anafikiri kuwa mtazamo wake pekee ni sahihi na pekee.
Jinsi Ya Kukabiliana Na Wahukumu
Wahukumu wako kila mahali na unakutana nao kila siku. Anaweza kuwa ni mzazi wako,mpenzi wako au bosi kazini na hata rafiki yako.
Ni vizuri kujua namna ya kukabiliana nao na hukumu zao juu yako. Kitu cha msingi siku zote ni kubaki na mtazamo chanya juu ya kila kitu ikiwemo hukumu zao
Usiawaamini Na Jiamini:
Maneno na mtazamo wao hasi juu yako haumaanishi kuwa ni kweli na usife moyo na kujiona kama mtu usiyefaa. Kuwa na misingi yako ya ubora na tembea katika mstari huo,vingine vyote watakavyosema wengine visikushushe mtima wako kwakuwa kunakitu kizuri ndani yako na si rahisi kwao kuona kwasababu wanaangalia upande hasi wa kila kitu. Fahamu kuwa wanayoyasema hayaakisi tawira yako bali ni mtazamo wao juu yako.
Mhukumu anataka kukushusha wewe ili yeye aonekane yuko juu. Usimpe hiyo nafasi.
Jenga Utulivu Na Wapuuze:
Ni vyema kuwa mtulivu na kuwa kimya juu ya suala husika badala ya kujibu au kujitetea. Wakati mwingine UKIMYA ni jibu sahihi zaidi. Majibu ya haraka yanaweza yakawa ya kujihami tu na unapojihami unajiweka katika nafasi sawa na mtuhumu. Nafasi ya chini na hasi.
Mfikirie Mhukumu Na Vaa Viatu Vyake
Chukua nafasi ya mumfikiria mhukumu na angalia ni nini kinamfanya aseme anayoyasema juu yako. Unaweza kugundua kuwa hana taarifa za kutosha juu yako,au elimu yake juu ya maisha na mazingirza aliyotoka na kukulia yanachangia kuwa mtu wa aina hiyo.
Hii itakusaidia kumchulia jinsi alivyo na kumsamehe. Pengine hata wewe ungefanya hivyo katika mazingira yake.
Fahamu pia tabia zinajengwa na hatuzaliwi nazo,hivyo mtu anaweza akajifunza na kubadirika.
Muelimishe
Wahukumu hutoa maamuzi bila kuwa na taarifa za kutosha kuhusu we na suala husika.
Pata nafasi na mweleze juu ya suala linalohusika na hukumu zake. Hii itamsaidia kuwaza tofauti juu yako na pengine kubadiri tabia ya kuwa mhukumu bila kujua vyakutosha.
Jinsi Ya Kujidhibiti Na Tatizo LaUhukumu
Pengine wewe mwenyewe unaweza ukawa na tabia za kuhukumu pia na unapenda kuondokana na tabia hii.
Kama nilivyosema hapo awali kuwa tabia tunazijenga wenyewe na hatuzaliwi nazo hivyo pia tunaweza kuzibomoa na kujenga tabia nyingine mpya bila kujali una umri gani.
Kama unataka kuondokana na tabia ya uhukumu fuata njia zifuatazo:
Jifunze Kuvaa Uhusika Wa Mtu Mwingine
Vaa nafasi ya mwingine na tembea katika viatu vyake. Hii ni muhimu sana katika kudhibiti tabia ya uhukumu kwa wengine. Ukivaa uhusika utajua nini kinamsibu mwingine.
Pata Taarifa Za Kutosha Kabla Ya Kuamua Juu Ya Jambo Au Mtu
Uliza maswali au jifunze zaidi kuhusu mlengwa na jambo husika. Ukijua sbabu za hali kuwa kama ilivyo utagundua kuwa maamuzi yako yanaweza kuwa tofauti kama ujingejua.
Usimhukumu Mtu Kutokana Na Mwonekano
Jifunze kuhusu mtu husika ili kujua zaidi na usiharakishe kuamua juu yake. Mwonekano wa nje au kabila,rangi na imani havitoshi kukupa taarifa za kutosha kufanya maamuzi.
Usisikilize Maneno Ya Watu Na Kuamua
Watu wanasema chochote na sio yote ni kweli kuhusu jambo au mtu. Usifanya maamuzi au kuweka msimamo juu ya jambo au mtu kwa maelezo toka kwa watu peke yake
Kuwa Na Mawazo Chanya
Jifunze na amua kuangalia mambo na kufikiria katika upande chanya. Fahamu kuwa “unaona na kusikia kile unachotaka kusikia” ukiawa chanya katika kila jambo utaona vitu vizuri tu ambavyo mtu anavyo na kukufanya uache tabia ya kuhukumu
Jifunze Juu Ya Mitazamo Tofauti
Unatakiwa kufahamu kuwa kila jambo linaweza kuangaliwa na kuonekana tofauti kulingana na jinsi unavyoliangalia na nafasi uliyosimama wakati wa kuliangalia.
Mfano Kama unafikiri “kufanya kazi jumapili ni uovu” kama muumini dini fulani mwingine anawezakuona kuwa “kufanya kazi jumapili ni sawa ila kufanya kazi jumamosi ni uovu”
Unaona unachoona kulingana na pale uliposimama. Ukitambua hili utabadili tabia yako ya kuhukumu vibaya wengine na kuona mambo kutoka pale walipo.
Kuwa Na Fikra Huru
Hii ina maanisha kuwa uwe mtu ambaye unaruhusu mambo mapya na tofauti katika fikra zako na kukubaliana nayo. Kuwa na misimamo isiyoruhusu kuangalia uwepo wa vinghine ni hatari na inachangia kuwa mhukumu. Kubaliana na hali kuwa kuna elimu na fikra tofauti na zako.
Jenga Upendo Na Huruma
Huwezi kumhukumu unayemependa,unapohukumu unakoma kupenda.
Kama unaona kuwa kunshida na mtu ni vyema kujenga huruma na kuweza kumsaidia kwa hali ambayo anayo ili awe bora zaidi.
Panua Ufahamu Na Ongeza Elimu Juu Ya Maisha
Elimu zaidi juu ya watu na ulimwengu itakusaidia kubadili tabia zako.
Pata nafasi ya kufahamu watu wengi zaidi na kushirikiana nao hta kama wana mitazamo na imani tofauti na wewe. Jifunze kuishi na kushirikiana na watu tofauti na wewe kwa mafanikio.
Hali Ikoje Kwako?
Je una mtu ambaye ana tabia ya kuhukumu? Au wewe mwenyewe unahisi unatabia hiyo? Unaathirika kiasi gani na hili au ni jinsi gani umetatua tatizo lako?
Tuandikie katika kisanduku cha maoni hapa chini
0 comments:
Post a Comment