Friday 19 August 2016

SAMATTA ATUPIA KRC GENK IKIKARIBA KUFUZU HATUA YA MAKUNDI EUROPA



TIMU ya KRC Genk inayoshiriki ligi kuu nchini Ubelgiji imekaribia kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya Europa baada ya kutoka sare ya kufungana mabao 2-2 ugenini dhidi ya Lokomotiva Zagreb.

Genk walilianza kwa kasi pambano hilo lililopigwa katika dimba la Stadion Kranjceviceva jijini Zagreb na kufanikiwa kupata penati dakika ya 34 iliyowekwa nyavuni kiufundi na winga raia wa Jamaica, Leon Bailey.

Dakika moja tu baada ya mpira kuanza kipindi cha pili kiungo Sandy Walsh alifanya kazi ya ziada na kumtengenezea nafasi Mtanzania Mbwana Samatta ambaye hakufanya ajizi na kuukwamisha mpira wavuni hivyo kuifanya Genk kuwa mbele kwa mabao mawili ugenini.

Lokomotiva walifanikiwa kupata penati katika dakika ya 51 ambayo alipigwa na Mirco Maric aliyewapatia wenyeji bao la kwanza. Bao hilo liliwaongezea ari na kuanza kulisakama lango la Genk.




Genk ambayo inasumbuliwa na tatizo la mabeki licha ya hivi karibuni kumsajili Omar Colley raia wa Gambia, ilikubali kugawana pointi na wenyeji baada ya kuruhusu bao la kusawazisha dakika 59 lililofungwa na Ivan Fiolic.

Katika mchezo huo Samatta alitolewa dakika ya 83 na nafasi yake kuchukuliwa na Nikos Karelis lakini mabadiliko hayo hayakubadilisha matokeo kwani hadi dakika 90 zinamalizika hakuna timu ambayo iliongeza bao.

Genk inayofundishwa na Peter Maes itaikaribisha Lokomotiva katika dimba la Cristal Arena jijini Genk kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa alhamisi ijayo.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA