WAKUU WA TAASISI ZA USAFIRI WA ANGA - AFRIKA WAKUTANA JIJINI ARUSHA
Wakuu wa taasisi za Usafiri wa Anga Afrika wanakutana jijini Arusha, Tanzania kujadili kwa Pamoja namna bora ya kuboresha sekta ya Usafiri wa Anga Barani Afrika.
Akizungumza wakati wa kuufungua mkutano huo,Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema sekta ya Usafiri wa Anga Barani Afrika imekuwa ikipiga hatua kusonga mbele lakini juhudi za Pamoja zinahitajika ili kuongeza kasi ya ukuaji wake.
Prof. Mbarawa amesema mkutano huu ni muhimu sana na unafanyika wakati sahihi ambapo uelewa wa wananchi wengi juu ya Usafiri wa anga umeongezeka.
"Ni heshima kwetu kama nchi kupata fursa ya kuandaa mkutano huu, sina shaka kuwa mtajadili na kufanya maamuzi sahihi kwa maslahi ya bara letu la Afrika" amesema Prof. Mbarawa
Kwa upande wa Rais wa Kamisheni hiyo Bw. Silas Udahemuka ameishukuru Tanzania kwa kukubali kuwa mwenyeji na kuandaa mkutano huu na kuwataka wajumbe kuitumia vyema fursa hii kupanga na kujadili mambo chanya yatakayoleta utatuzi wa changamoto zinazoikabili sekta hii barani Afrika.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania Bw. Hamza Johari amesema mkutano huu siyo tu unawakutanisha wakuu wa taasisi kujadili utatuzi wa changamoto bali ni kuwa na sauti ya Pamoja kama Afrika katika majukwaa ya kimataifa ili kuhakikisha maslahi ya Afrika yanazingatiwa.
Mkutano huu wa pili unafanyika kwa siku mbili katika hoteli ya Gran Melia jijini Arusha na wajumbe watapata nafasi ya kutembelea hifadhi ya Ngorongoro ikiwa ni sehemu ya kukuza utalii nchini.
0 comments:
Post a Comment