Tuesday 25 January 2022

BARABARA YA RUANGWA-NAGANGA KM 53 KUKAMILIKA NOVEMBA



Mmoja wa Wananchi wa Kata ya Nanganga, akimshukuru Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kwa  uamuzi wa Serikali wa kuijenga barabara Naganga-Ruangwa KM 53.2 kwa kiwango cha lami mkoani Lindi.



Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akisisitiza jambo kwa wananchi wa Kata ya Naganga Mkoani Lindi, alipokagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Naganga-Ruangwa KM 53 kwa kiwango cha lami mkoani Lindi.



Eng. Simoni Makala akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alipokagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Naganga-Ruangwa KM 53.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Lindi. Kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoani humo Eng. Andrea Kasamwa akifuatilia.



Muonekano wa Barabara ya Naganga-Ruangwa Km 53.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Lindi.





Imeelezwa kuwa barabara ya Ruangwa-Nanganga yenye urefu wa KM 53.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Lindi itakamilika Novemba mwaka wa huu.

Barabara hiyo ambayo ni sehemu ya barabara ya Nachingwea-Ruangwa-Nanganga yenye urefu wa KM 106 inatarajiwa kuufungua mkoa wa Lindi kiuchumi kwa kuwa itaunganisha Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Masasi kwa urahisi na hivyo kuhamasisha shughuli za maendeleo kwa wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Lindi Eng. Andrea Kasamwa amemweleza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo leo. 

Eng. Kasamwa amesema Ujenzi huo unahusisha ujenzi wa daraja  kubwa moja la Mto Lukuledi, makalvati makubwa 31 na makalvati madogo 68 ambayo yako katika hatua mbalimbali za ujenzi.


Kwa upande wake Waziri Prof. Mbarawa amesema zaidi ya shilingi bilioni 59 zinatarajiwa kutumika katika awamu ya kwanza ya ujenzi huo sehemu ya Nanganga-Ruangwa hivyo kumtaka Msimamizi wa ujenzi huo kampuni ya TECU na wafanyakazi wa TANROADS mkoa wa Lindi kuhakikisha ujenzi wake unaendana na thamani ya fedha na kuharakisha usanifu wa kina kwa haraka sehemu iiliyobaki ya Nachingwea-Ruangwa KM 52.8.

Prof. Mbarawa amemtaka Msimamizi wa mradi huo TECU kuhakikisha anazingatia viwango vilivyokubaliwa katika  mkataba ili kuwezesha barabara kudumu kwa muda mrefu na kuchochea maendeleo ya wakazi wa mkoa wa Lindi.

“Barabara hii itapitisha mzigo mkubwa kuupeleka kwenye bandari ya Mtwara na maeneo mengine ya nchi hivyo simamieni kikamilifu na muweke alama zote za barabara zinazohitajika ikiwemo taa na alama za usalama barabarani” amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Amemtaka Meneja TANROADS Mkoa wa Lindi kuhakikisha wananchi wanaelimishwa ili kupisha eneo la mradi na kumuwezesha Mkandarasi kufanya kazi na wananchi wenye malalamiko yapatiwe ufumbuzi kwa haraka.

Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya siku tatu katika Mkoa wa LIndi kukagua miradi ya miundombinu ya Sekta ya Ujenzi na Uchukuzi.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

 

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA