Monday, 16 May 2022
Friday, 11 March 2022
SAFARI ZA TRENI KUREJEA NDANI YA SAA 24 - PROF MBARAWA
11:14 |
No Comments |
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akionesha vipengele vinavyohitaji maboresho katika mkataba wa ujenzi wa Kiwanda cha Mkulazi, unaojengwa na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), wakati alipotembelea mradi huo Mkoani Morogoro.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Viongozi wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na Uongozi wa Kiwanda cha Mkulazi, wakati alipotembelea mradi huo kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kiwanda cha Mkulazi, Mkoani Morogoro.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, kuhusu hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Daraja la jipya la Reli linalojengwa katika eneo la Kidete, Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro.
Muonekano wa daraja la reli lililosombwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini katika stesheni ya Kidete, Wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro. Kusombwa kwa daraja hilo kumesimamisha huduma za treni kwa takribani siku 10.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya daraja jipya la reli linalojengwa na Kampuni ya Yapi Markezi katika stesheni ya Kidete, WIlayani Kilosa Mkoani Morogoro. Daraja hilo limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 3 na linatarajiwa kukamilika leo tarehe 11 Machi 2022.
Mafundi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) wakiendelea na kazi ya kutandika reli katika stesheni ya reli ya Kidete, Wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro.
Serikali imesema ujenzi wa Daraja jipya la reli ya kati linalojengwa baada ya daraja la zamani kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika eneo la kidete Wilayani Kilosa litakamilika ndani ya saa 24 ili kuruhusu huduma ya treni kuendelea.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema kurejeshwa kwa safari za treni kutapunguza changamoto ya usafirishaji wa abiria na mizigo hususani kwa mikoa ya pembezoni mwa Tanzania.
“Leo ni takribani siku ya kumi hakuna bidhaa zinazokwenda mikoa ya pembezoni mwa Tanzania kama Kigoma sababu wanategemea sana reli hii hasa wafanyabiashara, mtakampokamilisha ujenzi huu kutawapunguzia adha wananchi wa maeneo hayo’ Amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa amelipongeza Shirika la Reli Tanzania (TRC), kwa kufanya maamuzi ya haraka na kuhakikisha huduma zinarejea ndani ya muda mfupi na kuwataka kuzingatia thamani ya fedha kwa fedha zote zinazotumika nyakati za dharura.
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa ameupongeza Uongozi wa Yapi Markezi kwa kushirikiana kwa karibu na TRC katika kutekeleza ujenzi wa daraha hilo kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vilivyokubalika.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Shirika linafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha huduma za usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo zinarejea.
Masanja ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo umegharimu kiasi cha shilngi takribani bilioni 3 na linatarajiwa kukamilika muda wowote kuanzia sasa na hatimaye kuruhusu treni ya majaribio kupita.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Makame Mbarawa ameitaka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kuangalia upya vipengele vya ujenzi wa mradi wa Kiwanda cha Mkulazi ili kujiridhisha na vipengele vilivyopo kama vina tija na vimezingatia uhalisia.
Prof. Mbarawa ameeleza umuhimu wa kukamilisha mradi huo na kueleza kuwa Serikali haitosita kuvunja mkataba na Mkandarasi Kampuni ya Kay Bouvet Enginerring ltd ya nchini India itakapoona hairidhishwi na maendeleo ya mradi huo.
“Hatuwezi kukubali mwende namna hii, mmeeshaandikiwa barua za onyo mbili ikiandikwa ya tatu mkataba utakuwa umeishia hapo, sababu hamjatilia uzito na kasi yenu haioneshi kama mtamaliza kwa wakati’ amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Kampuni ya Mkulazi Selestine Some amesema mradi huo unapashwa kukamilika mwezu agosti mwaka hu una kazi zinazoendelea zimefikia asimlia zaidi ya 30.
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WIzara ya Ujenzi na Uchukuzi)
Tuesday, 25 January 2022
BARABARA YA RUANGWA-NAGANGA KM 53 KUKAMILIKA NOVEMBA
20:04 |
No Comments |
Mmoja wa Wananchi wa Kata ya Nanganga, akimshukuru Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kwa uamuzi wa Serikali wa kuijenga barabara Naganga-Ruangwa KM 53.2 kwa kiwango cha lami mkoani Lindi.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akisisitiza jambo kwa wananchi wa Kata ya Naganga Mkoani Lindi, alipokagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Naganga-Ruangwa KM 53 kwa kiwango cha lami mkoani Lindi.
Eng. Simoni Makala akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alipokagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Naganga-Ruangwa KM 53.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Lindi. Kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoani humo Eng. Andrea Kasamwa akifuatilia.
Muonekano wa Barabara ya Naganga-Ruangwa Km 53.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Lindi.
Imeelezwa kuwa barabara ya Ruangwa-Nanganga yenye urefu wa KM 53.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Lindi itakamilika Novemba mwaka wa huu.
Barabara hiyo ambayo ni sehemu ya barabara ya Nachingwea-Ruangwa-Nanganga yenye urefu wa KM 106 inatarajiwa kuufungua mkoa wa Lindi kiuchumi kwa kuwa itaunganisha Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Masasi kwa urahisi na hivyo kuhamasisha shughuli za maendeleo kwa wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Lindi Eng. Andrea Kasamwa amemweleza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo leo.
Eng. Kasamwa amesema Ujenzi huo unahusisha ujenzi wa daraja kubwa moja la Mto Lukuledi, makalvati makubwa 31 na makalvati madogo 68 ambayo yako katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Kwa upande wake Waziri Prof. Mbarawa amesema zaidi ya shilingi bilioni 59 zinatarajiwa kutumika katika awamu ya kwanza ya ujenzi huo sehemu ya Nanganga-Ruangwa hivyo kumtaka Msimamizi wa ujenzi huo kampuni ya TECU na wafanyakazi wa TANROADS mkoa wa Lindi kuhakikisha ujenzi wake unaendana na thamani ya fedha na kuharakisha usanifu wa kina kwa haraka sehemu iiliyobaki ya Nachingwea-Ruangwa KM 52.8.
Prof. Mbarawa amemtaka Msimamizi wa mradi huo TECU kuhakikisha anazingatia viwango vilivyokubaliwa katika mkataba ili kuwezesha barabara kudumu kwa muda mrefu na kuchochea maendeleo ya wakazi wa mkoa wa Lindi.
“Barabara hii itapitisha mzigo mkubwa kuupeleka kwenye bandari ya Mtwara na maeneo mengine ya nchi hivyo simamieni kikamilifu na muweke alama zote za barabara zinazohitajika ikiwemo taa na alama za usalama barabarani” amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Amemtaka Meneja TANROADS Mkoa wa Lindi kuhakikisha wananchi wanaelimishwa ili kupisha eneo la mradi na kumuwezesha Mkandarasi kufanya kazi na wananchi wenye malalamiko yapatiwe ufumbuzi kwa haraka.
Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya siku tatu katika Mkoa wa LIndi kukagua miradi ya miundombinu ya Sekta ya Ujenzi na Uchukuzi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
Monday, 24 January 2022
TAA WEKENI TAA KATIKA VIWANJA VYA NDEGE-PROF. MBARAWA
19:00 |
No Comments |
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi. Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya M/S Beijing Construction Enginering Group Company ltd inayojenga Kiwanja cha Mtwara, alipokagua ujenzi wake. Wa tatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali, Marco Gaguti.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mtwara, Eng. Dotto John akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi. Prof. Makame Mbarawa, alipokagua ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mtwara. Kulia ni Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Mtwara Bw. Samweli Mruma.
Akizungumza mara baada ya kukagua upanuzi na ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Mtwara Prof. Mbarawa amesema uwepo wa viwanja vya ndege ni uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali hivyo viwanja ivyo vitumike kikamilifu.
“Zaidi ya shilingi bilioni 55 zimetumika kukarabati na kupanua kiwanja hiki, jambo jema hapa ni kuwa kiwanja hiki kikikamilika kitaweza kufanya kazi kwa saa 24, hongereni “ amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amepongeza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na (TAA) mkoani Mtwara kwa usimamizi mzuri wa upanuzi na ukarabati wa kiwanja hicho ambao kwa ujumla ujenzi wake umefikia asilimia themanini na tano na mradi unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Aidha, Prof. Mbarawa ameitaka TAA na Uongozi wa Mikoa kuhakikisha maeneo ya viwanja vya ndege yanalindwa na yaliyovamiwa yarejeshwe mara moja kwa kufuata sheria wakati Serikali ikijipanga kuendeleza maeneo hayo.
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mtwara Eng. Dotto John amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutawezesha ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 200 kuruka na kutua katika kiwanja hicho na hivyo kuchochea uchumi wa ukanda wa kusini mwa Tanzania.
“Kiwanja hiki kimerefushwa kutoka mita 2258 hadi kufikia mita 2800, na upana wa mita 45 kutoka mita 30 zilizokuwepo awali’ amesema Eng. John.
Kwa upande wake Meneja wa Kiwanja cha Ndege Mtwara Bw. Samweli Mruma amesema kukamilika kwa kiwanja hicho kutakipandisha daraja kutoka Daraja la Code 3C kwenda Code 4E kulingana na Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) na hivyo kuongeza viwango vya kuhudumia ndege kubwa kwa wakati mmoja hapa nchini.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua Bandari ya Mtwara na kuagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuhakikisha usalama wa wafanyakazi unapewa kipaumbele wakati wote.
“Bandari nawapa kazi tatu, kuhakikisha usalama wa wafanyakazi mahali pa kazi, kujitangaza na kukusanya mapato’ Amesema Prof. Mbarawa.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa upanuzi wa miundobinu ya bandari, usafiri wa anga na barabara mkoani humo italindwa kwa karibu kwa kuwa ni ukombozi wa uchumi kwa wananchi wa kanda ya Kusini kwa ujumla.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Friday, 21 January 2022
UJENZI WA DARAJA LA KITENGULE NA BARABARA UNGANISHI KUKAMILIKA MEI
21:45 |
No Comments |
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akisisiza jambo kwa Wasimamizi wa ujenzi wa Daraja la Kitengule lenye urefu wa mita 40 alipokagua maendeleo ya ujenzi wake mkoani Kagera.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akiangalia mtambo wa kuunganisha mabomba katika shamba la Miwa la kiwanda cha sukari cha Kagera
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akishuka katika moja ya magari yanayotumika kuandaa mashamba ya miwa katika kiwanda cha sukari Kagera, alipokagua miundombinu ya barabara katika kiwanda hicho.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya awali katika Kiwanda cha Sukari mkoani Kagera, alipotembelea shule hiyo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akimsikiliza Mhandisi Umwagiliaji Neema Senyael wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera, alipokagua miundombinu ya kiwanda hicho.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya daraja la Kitengule lenye urefu wa Mita 40 linalounganisha Wilaya za Misenyi na Karagwe, mkoani Kagera.
Imeelezwa kuwa kufanikiwa kwa miradi ya kiuchumi na uzalishaji katika mkoa wa Kagera kutategemea kukamilika kwa haraka kwa miundombinu ya barabara na madaraja mkoani humo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema hayo alipokagua ujenzi wa daraja la Kitengule lenye urefu wa mita 140 na barabara unganishi za daraja hilo zenye urefu wa KM 18.
Amesema kukamilika kwa darala hilo na barabara unganishi kutahuisha shughuli za kilimo, biashara na kuongeza uzalishaji wa sukari katika kiwanda cha Kagera.
“Kutokana na kazi kubwa inayofanyika hapa ya ujenzi wa daraja na barabara ni Dhahiri kutachangia uzalishaji mkubwa wa miwa na mazao mengine ya kilimo hivyo nakuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Kagera kuanza usanifu wa barabara hii sehemu iliyobaki ya Kitengule-Bunazi KM 24 ili kuziunganisha Wilaya za Misenyi na Karagwe kwa lami’ amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Amekipongeza kiwanda cha sukari cha Kagera kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya maji itakayokiwezesha kuongeza uzalishaji wa sukari nchini.
Naye Meneja TANROADS mkoa wa Kagera Eng. Yudas Msangi amesema ujenzi wa daraja la Kitengule umesanifiwa kupitisha uzito wa tani mia moja na kwa sasa umefikia asilimia 90 kukamilika na barabara unganishi zenye urefu wa KM 18 zinatarajiwa kukamilika mwezi mei mwaka huu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Sukari Kagera Bw. Seif Seif amesema Ujenzi wa daraja la Kitengule lenye urefu mita 40 na barabara unganishi zenye urefu wa KM 18 zinazounganisha Wilaya ya Misenyi na Karagwe ukikamilika utarahishisha kazi ya uzalishaji wa sukari katika kiwanda hicho na kuibua fursa nyingi za ajira ambapo tumejipanga kuongeza ukubwa wa mashamba ili kutatua changamoto ya upungufu wa sukari nchini.
Aidha, ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa barabara katika Wilaya za Misenyi na Karagwe na kusisitiza kwamba kiwanda hicho kitatoa ushirikiano wote unaohitajika katika kuhakikisha malengo ya Serikali katika kuongeza uzalishaji wa sukari, kutoa ajira kwa wahitimu wa kada zinazohitajika katika kiwanda hicho yanafikiwa kwa wakati.
Amesema kwa sasa kiwanda kinazalisha sukari tani elfu tisini na nne ila kutokana na kukamilika kwa miundombinu na daraja la Kitengule kunatoa fursa ya kuongeza mashamba na katika miaka mitatu ijayo kiwanda kimejipanga kuzalisha tani 170,000/- kwa mwaka.
Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Kanali Wilson Sakulu ameipongeza Serikali kwa kuziunganisha Wilaya ya Misenyi na Karagwe kwa barabara ya lami na daraja la uhakika kwani kutainua uchumi na kuongeza usalama kwa wakazi wa Wilaya hizo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa yuko katika ziara ya siku tatu kukagua maendeleo ya miradi ya Sekta ya Ujenzi na Uchukuzi na kuhamasisha wadau wa mbalimbali kuibua fursa za uchumi mkoani Kagera.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI, WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI.
Thursday, 20 January 2022
MKOA WA KAGERA KUFUNGULIWA KIMIUNDOMBINU-PROF. MBARAWA
19:38 |
No Comments |
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge akizungumza na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, mara baada ya kuwasili mkoani Kagera kwa ziara ya kukagua miundombinu ya sekta za Ujenzi na Uchukuzi.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, katika picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa wa Kagera na Watendaji wa taasisi za Ujenzi na Uchukuzi mkoani humo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge (kushoto) na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Profesa Faustin Kamuzora.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema Serikali itaendelea na mkakati wake wa kuhakikisha miundombinu yote ya usafiri na uchukuzi mkoani Kagera inajengwa kwa viwango vya juu ili kuchochea uchumi wa mkoa huo.
Akizungumza mara baada ya kuanza ziara ya siku tatu Mkoani humo Prof. Mbarawa amesema Mkoa wa Kagera ni mkoa muhimu kiuchumi kwa Taifa kwa kuwa uko pembezoni mwa nchi na unaiunganisha nchi ya Tanzania na Uganda, Rwanda na Burundi ambapo ni soko zuri kwa bidhaa mbalimbali toka nchini.
“Tumejipanga kuhakikisha kwamba usafiri wa majini, angani na barabarani katika mkoa huu hususani kwa njia zote zinazounganisha Tanzania na Nchi jirani unaimarishwa na matokeo yake mtaanza kuyaona siku za hivi karibuni’ amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha mipango yote iliyopangwa na Serikali mwaka huu mkoani humo inatekelezwa kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha katika miradi yote.
Prof. Mbarawa amitaka TPA Mkoani Kagera kutowabugudhi wafanyakazi katika bandari hiyo (makuli) ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi.
Aidha, amesema kwa sasa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kitaendelea kutumika na kuboreshwa ili kiweze kutoa huduma wakati wote na kuitaka Serikali ya Mkoa wa Kagera kuhakikisha eneo lililotengwa kwa ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Omukajunguti linahifadhiwa kwa matumizi ya siku zijazo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuhakikisha barabara nyingi mkoani humo zinapitika wakati wote wa mwaka na kuwahakikishia kuwa mkoa huo utatoa ushirikiano kwa Wizara ili kuhakikisha miradi yote iliyopangwa kutekelezwa inakamilika kwa wakati.
‘Mhe Waziri Mkoa wetu huu barabara zake zikifunguka na meli ya MV Mwanza ikianza kutoa huduma uchumi wa Kagera utaimarika na kuchochea uzalishaji wa mazao ya kilimo amesema Meja Jenerali Mbuge.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora amemuomba Waziri Prof. Mbarawa kuwa ujenzi wa barabara ya Omugakorongo-Murongo KM 110 unaotarajiwa kuanza hivi karibuni sehemu ya kwanza uanzie Kayanga ili kuleta urahisi katika utekelezaji wa mradi huo.
Prof. Mbarawa yuko Mkoani Kagera kukagua miradi ya sekta za Ujenzi na Uchukuzi inayoendelea mkoani humo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.







