Tuesday 2 July 2024

FAHAMU THAMANI YA MUDA ULIONAO





Baada ya kuzaliwa tu kitu ambacho mwanadamu lazima kitamkuta ni kifo. Kifo ndio mwisho wa mtu aliyezaliwa.Kati ya kuzaliwa na kufa kuna muda wa maisha ambao hatuna dhamana nao na hatujui ni mrefu kiasi gani.

Siku moja ya maisha ya mwanadamu ina urefu wa masaa ishirini na nne (24) tu ambayo ni sawa na dakika 1440 tu. Na mwaka mmoja wa maisha ya mwanadamu huyo una siku 365 tu ambazo ni sawa na dakika laki tano ishirini na tano elfu na mia sita tu (525,600).

Katika nchi zinazoendelea ambapo Tanzania ni moja ya nchi hizo, Tunategemea mtu astaafu kazi na kuanza kula pensheni ya kazi yake ya maisha afikapo umri wa miaka hamsini na tano (55) ambayo ni sawa na dakika milioni ishirini na nane laki tisa na elfu nane tu (28,908,000) lakini mtu huyu huanza kufanya kazi afikishapo umri wa miaka kumi na nane (18) ya maisha yake ambapo atakuwa ameishi dakika milioni tisa laki nne sitini elfu na mia nane (9,460,800) na hivyo ili astaafu amebakiza miaka Thelathini na saba tu (37) ambapo ni sawa na dakika milioni kumi na tisa laki nne arobaini na saba elfu na mia mbili (19,447,200) tu.

Swali muhimu la kujiuliza hapa je ulipokua na miaka kumi na nane (18) ulikua tayari ushaanza kazi? Kama hapana ulikua wapi? Umeanza kufanya kazi ya kukuingizia kipato ukiwa na miaka mingapi? Wakati unajiuliza maswali hayo usisahau point yetu ya msingi kuwa utastaafu ukiwa na umri wa miaka hamsini na tano (55) tu hivyo umri wa kuanza kazi ukitoa kwenye miaka hamsini na tano miaka itakayobaki ndo umri wako wa kazi.

Kanuni hii hawaachi nje wanaosema wao hawataajiriwa bali watajiajiri kwani wengi tukishafikisha miaka hamsini na tano (55) hatutakua na nguvu tena na hivyo tutatakiwa kustaafu.

Kumbe tuna muda mfupi sana wa kufanya mambo katika dunia hii. Kitu cha pekee cha thamani kubwa tulichonacho ni MUDA. Unatumiaje muda wako ndilo swali kubwa la kujiuliza

Unatumiaje muda wako wa asubuhi? Unatumiaje muda wako wa mchana na kabla ya kulala unatumiaje muda wako wa usiku?

Unamaliza masaa 12 kuangalia tamthilia ambayo waigizaji wake walitumia masaa 12 ya siku kuindaa ili iangaliwe unanufaika nini?

Unawekeza nini ili muda huu wa kufanya kazi ukifika ukomo uje kusema nilifanikiwa kujiwekeza sawasawa?

Unapowaza kufanya uwekezaji leo usisahau kuwa ili ufanikiwe ni lazima uwe na matumizi sahihi ya muda, ujue ni kwa namna gani utazigawanya dakika zako za siku kufanya mambo yaliyo muhimu na kwa kipaumbele.

Unapowaza kuwa mtu mwenye mafanikio jambo la kwanza unalotakiwa kufanikiwa ni jinsi ya kuutawala muda, hatuna muda wote duniani kiasi cha kuwa na muda wa kuupoteza bila kujua kuwa hatuna uwezo wa kuirudisha hata sekunde moja tu.

Utawala bora wa muda ni nguzo muhimu kuelekea kwenye mafanikio, sisemi usiwe na muda wa kupumzika na kufurahi na jamii bali je kabla hujapumzika umefanya nini?

Kuna watu wanajitoa sadaka kwelikweli, utakuta mtu anapoteza siku nzima, wiki, mwezi hata mwaka hajafanya chochote kuongeza thamani yake kisha anabaki analaumu tu!!!!!!!

Akiingia mitandaoni anatazama mambo yasiyoongeza thamani, anaangalia kuna picha gani mpya imepostiwa, anaangalia kuna wimbo gani mpya umetoka huu ni upuuzi nasema upuuzi kwakuwa hauongezi thamani yako na unafanya hivyo kabla ya kuongeza thamani na huu ni upotezaji wa muda.

Sisemi usiingie mtandaoni lakini kabla ya kuingia ujiulize unaenda kufanya nini kuna mambo mengi mazuri mtandaoni yanayofaa na hata makala hii ipo mtandaoni pia ambayo naamini roho wa Mungu yu juu yangu ili niwafikishie ninyi habari hii njema ya kujua thamani halisi ya muda.

Zawadi ya thamani mtu mmoja anaweza kumpa mtu mwingine ni zawadi ya muda. Hii ndio zawadi kubwa kuliko zote kwa kuwa mtu anakupa kitu ambacho hawezi kukipata tena. Huwezi kumlipa.

Je umeshawahi kumshukuru yeyote aliyepoteza masaa matatu ya dakika 180 kukaa kwenye sherehe yako ya kuagwa (sendooff)?  Aliyekuja kwenye sherehe yako ya kuzaliwa (birthday)? na sherehe nyingine za aina hiyo?

Muda ndio zawadi kubwa kuliko zawadi zote tulizonazo tunazoweza kumpa mtu. Hii ndiyo thamani halisi ya muda

Jifunze kuheshimu muda na kuupa thamani inayostahili ikiwa ni pamoja na kuifanyia kazi kila dakika inayopita.

Zaidi ya yote uyafanyayo muda wako ni muhimu zaidi. Tenga muda wako kwa kila jambo, zaidi sana tenga muda wako kwa ajili ya Mungu wako.

 

1day=1440min

1year=365days

1year=525600min

55years=28908000min

37years=19447200 min

  Kwa kumalizia tutafakari mambo machache ambayo naamini yanaweza kukusaidia na kuifanya safari muhimu ya maisha yako kuwa ya kuvutia na kuongeza thamani kwenye hii raslimali muhimu muda.

  1. Fahamu kuwa muda una thamani.

Muda una tathamani kama pesa tena tunaweza kusema kuwa ni zaidi ya mali kwa kuwa unaweza kuishi bila pesa lakini huwezi kuishi bila muda. Muda ni kipimo cha maisha kwa hiyo unaweza kutumika vizuri au kutumika vibaya. Ni muhimu kukaa chini na kutafakari je unatenda haki unapofika mahali pa kutamini muda?

  1. Thamani ya muda inaweza kuongezeka

Unaweza kuongeza thamani ya muda wako kwa kuchagua vipaumbele vichache vitakavyokula muda wako. Mambo utakayofanya yakaongeza thamani kwenye maisha yako na watu wengine inamaanisha kwamba muda wako umeuongezea thamani.

  1. Muda ni muhimu kuliko pesa

Watu wengi hukosea kuthamini muda na ndio maana mtu akipoteza pesa mara moja atapiga kelele sana,lakini ni mara ngapi amekuwa akipoteza muda kila siku bila hata kujali kama anapoteza kitu cha thamani.Kuna mamia ya watu duniani waliopatwa na shinikizo la damu na hata wengine kufa baada ya kujikuta wamepoteza pesa;lakini katika maisha yangu sijawahi kusikia mtu aliyejinyonga kwa kupoteza muda. Inawezekana wapo haiwezi kuwa wazi kama ilivyo kwa pesa.

Hivyo ndivyo mfumo wa maisha ulivyotutengeneza kuthamni vitu ambavyo havina maana sana na kuacha vike vyenye maana kama muda. Anthony Robin aliwahi kusema afadhali upoteze pesa kuliko kupoteza muda kwa sababu pesa uliyopoteza unaweza kutafuta ukapata pesa nyingi zaidi lakini huwezi kurudisha muda ambao umekwishapota.

  1. Muda unaweza kupotea

Kwa kuwa muda ni mali basi muda unaweza kupotea mtu asipohakikisha anafanya maamuzi ya matumizi ya mi=uda kwa busara. Muda unaopotea ni hasara kwa yule anayepoteza muda kwa sababu hakuna muda ambao umetolewa kwa mwanadamu ambo hauna kusudi la kutimiza.

  1. Muda unaweza kukombolewa

Kwa kuwa watu wengi tumefanya makosa katika swala zima la muda kwa kuupoteza,binadamu tumeumbwa kujifunza sana kutokana na makosa. Ukiwa katika mazingira ya kujikuta umepoteza muda kwa kujua au hata bila kujua upo uwezekano wa kuukomboa muda uliopotea na kuanza kuishi maisha ya matumaini na mafanikio makubwa kwa kuishi kusudi la kuwepo kwako.

Usifanye kosa la kutazama nyuma ulikoharibu haitakusaidia kuvuka kwa namna yoyote zaidi ya kujuta. Pale unapogundua kuwa ulikuwa unathamini vibaya muda wako na kujikuta unapoteza muda basi anzia hapo kwa kuanza kupanga mambo muhimu ambayo utayapa muda wa kutumia. Mambo hayo lazima yawe ni yake yanayokusaidia kutimiza kusudi la kuwepo kwako hapa duniani.

Naamini utakuwa umepata kitu kupitia Makala hii.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA