Monday, 24 January 2022

TAA WEKENI TAA KATIKA VIWANJA VYA NDEGE-PROF. MBARAWA

 


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi. Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya M/S Beijing Construction Enginering Group Company ltd inayojenga Kiwanja cha Mtwara, alipokagua ujenzi wake. Wa tatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali, Marco Gaguti.

 

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mtwara, Eng. Dotto John akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi. Prof. Makame Mbarawa, alipokagua ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mtwara.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mtwara, Eng. Dotto John akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi. Prof. Makame Mbarawa, alipokagua ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mtwara. Kulia ni Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Mtwara Bw. Samweli Mruma.


Muonekano wa barabara ya kuruka na kutua ndege iliyoongezwa urefu kutoka mita 2200 hadi 2800.



Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Nobert Kalembwe, akimwelezea Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa utendaji kazi wa mashine ya kupimia mafuta (Flow Meter) alipokagua upanuzi wa bandari hiyo.


Kufuatia uamuzi wa Serikali kuimarisha usafiri wa anga nchini Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuweka mikakati itakayayowezesha viwanja vyote vya ndege vya Mikoa kuwekwa taa ili kufanya kazi kwa saa ishirini na nne.

Akizungumza mara baada ya kukagua upanuzi na ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Mtwara Prof. Mbarawa amesema uwepo wa viwanja vya ndege ni uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali hivyo viwanja ivyo vitumike kikamilifu.

“Zaidi ya shilingi bilioni 55 zimetumika kukarabati na kupanua kiwanja hiki, jambo jema hapa ni kuwa kiwanja hiki kikikamilika kitaweza kufanya kazi kwa saa 24, hongereni “ amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amepongeza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na (TAA) mkoani Mtwara kwa usimamizi mzuri wa upanuzi na ukarabati wa kiwanja hicho ambao kwa ujumla ujenzi wake umefikia asilimia themanini na tano na mradi unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Aidha, Prof. Mbarawa ameitaka TAA na Uongozi wa Mikoa kuhakikisha maeneo ya viwanja vya ndege yanalindwa na yaliyovamiwa yarejeshwe mara moja kwa kufuata sheria wakati Serikali ikijipanga kuendeleza maeneo hayo.

Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mtwara Eng.  Dotto John  amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutawezesha ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 200 kuruka na kutua katika kiwanja hicho na hivyo kuchochea uchumi wa ukanda wa kusini mwa Tanzania.

“Kiwanja hiki kimerefushwa kutoka mita 2258 hadi kufikia mita 2800, na upana wa mita 45 kutoka mita 30 zilizokuwepo awali’ amesema Eng. John.

Kwa upande wake Meneja wa Kiwanja cha Ndege Mtwara Bw. Samweli Mruma amesema kukamilika kwa kiwanja hicho kutakipandisha daraja kutoka Daraja la Code 3C kwenda Code 4E kulingana na  Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO)  na hivyo kuongeza viwango vya kuhudumia ndege kubwa kwa wakati mmoja hapa nchini.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua Bandari ya Mtwara na kuagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuhakikisha usalama wa wafanyakazi unapewa kipaumbele wakati wote.

“Bandari nawapa kazi tatu, kuhakikisha usalama wa wafanyakazi  mahali pa kazi, kujitangaza na kukusanya mapato’ Amesema Prof. Mbarawa.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa upanuzi wa miundobinu ya bandari, usafiri wa anga na barabara mkoani humo italindwa kwa karibu kwa kuwa ni ukombozi wa uchumi kwa wananchi wa kanda ya Kusini kwa ujumla.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. 


0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA