Friday 11 March 2022

SAFARI ZA TRENI KUREJEA NDANI YA SAA 24 - PROF MBARAWA



Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akionesha vipengele vinavyohitaji maboresho katika mkataba wa ujenzi wa Kiwanda cha Mkulazi, unaojengwa na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), wakati alipotembelea mradi huo Mkoani Morogoro. 



Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Viongozi wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na Uongozi wa Kiwanda cha Mkulazi, wakati alipotembelea mradi huo kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kiwanda cha Mkulazi, Mkoani Morogoro.






Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, kuhusu hatua iliyofikiwa  ya ujenzi wa Daraja la jipya la Reli linalojengwa katika eneo la Kidete, Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro.



Muonekano wa daraja la reli lililosombwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini katika stesheni ya Kidete, Wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro. Kusombwa kwa daraja hilo kumesimamisha huduma za treni kwa takribani siku 10. 



Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya daraja jipya la reli linalojengwa na Kampuni ya Yapi Markezi katika stesheni ya Kidete, WIlayani Kilosa Mkoani Morogoro. Daraja hilo limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 3 na linatarajiwa kukamilika leo tarehe 11 Machi 2022.



Mafundi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) wakiendelea na kazi ya kutandika reli katika stesheni ya reli ya Kidete, Wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro. 


Serikali imesema ujenzi wa Daraja  jipya la reli ya kati  linalojengwa  baada ya daraja la zamani kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika eneo la kidete Wilayani Kilosa litakamilika ndani ya saa 24 ili kuruhusu  huduma ya treni kuendelea. 

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema kurejeshwa kwa safari za treni kutapunguza changamoto ya usafirishaji wa abiria na mizigo hususani kwa mikoa ya pembezoni mwa Tanzania. 

“Leo ni takribani siku ya kumi hakuna bidhaa zinazokwenda mikoa ya pembezoni mwa Tanzania kama Kigoma sababu wanategemea sana reli hii hasa wafanyabiashara, mtakampokamilisha ujenzi huu kutawapunguzia adha wananchi wa maeneo hayo’ Amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa. 

Waziri Prof. Mbarawa amelipongeza Shirika la Reli Tanzania (TRC), kwa kufanya maamuzi ya  haraka na kuhakikisha huduma zinarejea ndani ya muda mfupi na kuwataka kuzingatia thamani ya fedha kwa fedha zote zinazotumika nyakati za dharura.

Aidha, Waziri Prof. Mbarawa ameupongeza Uongozi wa Yapi Markezi kwa kushirikiana kwa karibu na TRC katika kutekeleza ujenzi wa daraha hilo kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vilivyokubalika. 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Shirika linafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha huduma za usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo zinarejea. 

Masanja ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo umegharimu kiasi cha shilngi takribani bilioni 3  na linatarajiwa kukamilika muda wowote kuanzia sasa na hatimaye kuruhusu treni ya majaribio kupita.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Makame Mbarawa ameitaka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kuangalia upya vipengele vya ujenzi wa mradi wa Kiwanda cha Mkulazi ili kujiridhisha na vipengele vilivyopo kama vina tija na vimezingatia uhalisia. 

Prof. Mbarawa ameeleza umuhimu wa kukamilisha mradi huo  na kueleza kuwa Serikali haitosita kuvunja mkataba na Mkandarasi Kampuni ya Kay Bouvet Enginerring ltd ya nchini India itakapoona hairidhishwi na maendeleo ya mradi huo. 

“Hatuwezi kukubali mwende namna hii, mmeeshaandikiwa barua za onyo mbili ikiandikwa ya tatu mkataba utakuwa umeishia hapo, sababu hamjatilia uzito na kasi yenu haioneshi kama mtamaliza kwa wakati’ amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Kampuni ya Mkulazi  Selestine  Some  amesema mradi huo unapashwa kukamilika mwezu agosti mwaka hu una kazi zinazoendelea zimefikia asimlia zaidi ya 30. 

(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WIzara ya Ujenzi na Uchukuzi)

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA