Sunday, 24 April 2022

BARABARA YA KIDATU – IFAKARA KUKAMILIKA KWA KIWANGO CHA LAMI

 

Kazi za ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara yenye urefu wa kilometa 66.9 kwa kiwango cha lami zikiendelea Mkoani Morogoro. Ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 54.5.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya Nchini Tanzania Mhe. Manfredo Fanti, wakati lipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9), Mkoani Morogoro.

Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya Nchini Tanzania Mhe. Manfredo Fanti, akisisitiza jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati walipokutana na kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9), Mkoani Morogoro.

Mbunge wa Kilombero, Mhe. Abubakar Asenga, akizungumza jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati wakikagua ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9), Mkoani Morogoro.

Mhandisi Mkazi kutoka Kitengo Maalum cha Wahandisi Washauri cha TANROADS (TECU), Eng. Anorld Maeda, akifafanua jambo kwa Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya Nchini Tanzania Mhe. Manfredo Fanti na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati walipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9), Mkoani Morogoro.

PICHA NA WUU

Serikali imesema inaendelea kutatua changamoto zilizokuwa zinaufanya mradi wa ujenzi wa barabara ya Kidatu hadi Ifakara (km 66.9), kusuasua na kuwaahidi wananchi wanaotumia barabara hiyo kuwa mradi unaendelea na utakamilika kwa ubora na viwango vilivyowekwa.

Hayo yameelezwa mkoani Morogoro na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alipotembelea  mradi huo na kuona hatua maendeleo yake akiambatana na Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini Tanzania ambao ndio wafadhili wa mradi huo.

Amesema kuwa barabara hiyo iliyoanza mwaka 2017 ilikuwa ikamilike miaka michache iliyopita lakini kumekuwa na changamoto ambazo zilisababisha kazi ichelewe ikiwemo usimamizi wa mradi pamoja na uwezo wa mkandarasi kutokuwa na kasi ya ujenzi kama ilivyotarajiwa.

“Nawahakikishia wananchi wa Kilombero na wote wanaotumia barabara hii kuwa sasa barabara inakwenda kumalizika kwa kiwango cha lami”, amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amesema lazima tukubali kuwa mradi huu umetupa changamoto nyingi lakini hatutaki kurudi nyuma kwani nia ya wananchi na Serikali ni kuona barabara hi inakamilika kwa viwango vilivyokusudiwa.

Naye, Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya Nchini Tanzania, Mheshimiwa Manfredo Fanti, ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya mkoa wa Morogoro na hivyo amewahakikishia watanzania kuwa Umoja umejitoa kikamilifu kwa kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha mradi huo sasa unakwenda kukamilika hivi karibuni.

Akitoa taarifa ya mradi, Mhandisi Mkazi kutoka Kitengo Maalum cha Wahandisi Washauri cha TANROADS (TECU), Eng. Anorld Maeda, ameeleza kuwa mradi umefikia asilimia 54.5 na wanaendelea kumsukuma mkandarasi akamilishe kwa muda uliopangwa na ubora.

“Ni miezi saba toka tulivyoupokea mradi huu kwa Mhandisi Mkazi alliyeondoka ukiwa na asilima 33 na sasa kazi zinaendelea vizuri ambapo ujenzi wa Daraja la Ruaha Mkuu (m 130), umefikia asilimia 50, madaraja mengine manne asilimia 78, maboksi kalvati asilimia 67 na pipe kalvati asilimia 72”, amesema Eng. Maeda.

Kwa upande wake Mbunge wa Kilombero, Mhe. Abubakar Asenga, ameshukuru ujio wa Balozi  pamoja na Waziri wa Ujenzi kwa kutembelea mradi huo na kuzidi kusukuma ujenzi huo ambao wana kilombero wana imani ndani ya mwaka mmoja barabara hiyo itakamilika na kusaidia kuchochea maendeleo kwa wananchi wake.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hanji Godigodi, ameeleza kuwa barabara hiyo ikikamilika itakuwa mkombozi sana kwa wananchi na itapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za usafiri na usafirishaji wa abira na mazao.

Zaidi ya Shilingi Bilioni 100 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9) ambazo ni ufadhili toka nchi za Umoja wa Ulaya, USAID na UKAID.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA