Showing posts with label UCHUKUZI. Show all posts
Showing posts with label UCHUKUZI. Show all posts

Tuesday, 5 September 2023

PROFESA MBARAWA ASISITIZA USHIRIKIANO WIZARA MPYA

Waziri wa Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Watumishi wa Wizara hiyo (Hawapo pichani) mara baada ya kuwasili katika Wizara mpya kushoto ni Naibu Waziri Mhe. David Kihenzile, na Kulia ni Katibu Mkuu Prof. Godius Kahyarara, Mtumba Jijini Dodoma.


Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi , Prof.Godius Kahyarara, Akizungumza na
Menejimenti ya Wizara ya Uchukuzi,(hawapo pichani), mara baada ya kuwasili katika ofisi za Wizara mpya Mtumba, Jijini Dodoma.


Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame mbarawa  ametoa wito kwa menejimenti ya Wizara kushirikiana na wakuu wa taasisi  kuhakikisha kunakuwa na usimamizi madhubuti na wenye tija kwenye miradi inayoendelea ili iweze kukamilika kwa wakati na kwa thamani halisi ya fedha.

Prof. Mbarawa ameyasema hayo leo jijini Dodoma, mara baada ya kuwasili katika Wizara mpya, na kuwataka watumishi wa Wizara hiyo,kuwa na ushirikiano baina yao na kuongeza ufanisi wa kazi.

Aidha, Waziri Mbarawa, amesema kuwa Wizara ya Uchukuzi, ni moja ya Wizara ambayo ina miradi mingi na mikubwa ambayo ongeza tija kwenye maeneo ya usimamizi na uendeshaji pamoja na uboreshaji wa miundombinu.

“Awali ya yote napenda kumshukuru Mhe Rais wa awamu ya sita Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini tena na kuniteua kumsaidia tena,  na sasa ni katika Wizara ya Uchukuzi, ni wizara ambayo ina miradi mingi ya kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya Nchi yetu ikiwemo Ujenzi wa Reli ya kisasa ya SGR, uboreshaji wa bandari  na ununuzi wa ndege hivyo tufanye kazi ya kuleta matokeo kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla” amesema Prof Mbarawa

Kwa upande wake Naibu Waziri wa U chukuzi Mhe David  Kihenzile amesema ili Wizara ifikie malengo yaliyokusudiwa ni vyema viongozi pamoja na watumishi wote wa Wizara wakafanya kazi kama timu moja na kuongeza kuwa watendaji wa Wizara na Taasisi zake zote sasa wanapaswa kubadili fikra.

“Nawapongeza watumishi wote wa Wizara kwa mapokezi  mazuri na namshukuru Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na imani na mimi na kuniteua kumsaidia katika wizara hii ya Uchukuzi kama Naibu Waziri, tuendelee kufanya kazi kwa pamoja  na kwa ushirikiano” amesema Mhe Kihenzile.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius  Kahyarara amesisitiza kutoa ushirikiano mzuri  na Wizara hiyo na kuwataka watumishi kutekeleza majukumu yao kwa wakati na ufanisi.


IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO WIZARA YA UCHUKUZI

Saturday, 29 July 2023

TANZANIA NA URUSI KUENDELEZA MASHIRIKIANO SEKTA YA USAFIRI WA ANGA


Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Usafiri wa Anga na Hali ya Hewa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Biseko Chiganga akitia saini Mikataba makubaliano ya Usafiri wa Anga baina ya Tanzania na Urusi. Anayeshuhudia kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria Mamlaka ya  Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA),Maria Makalla Memba. Makubaliano hayo yamefikiwa nchini Urusi mwezi Julai 2023.


Timu ya wataalam kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) katika picha ya pamoja mara baada ya kukamilisha zoezi la saini Mikataba makubaliano ya Usafiri wa Anga baina ya Tanzania na Urusi.

 

Sunday, 24 April 2022

BARABARA YA KIDATU – IFAKARA KUKAMILIKA KWA KIWANGO CHA LAMI

 

Kazi za ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara yenye urefu wa kilometa 66.9 kwa kiwango cha lami zikiendelea Mkoani Morogoro. Ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 54.5.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya Nchini Tanzania Mhe. Manfredo Fanti, wakati lipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9), Mkoani Morogoro.

Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya Nchini Tanzania Mhe. Manfredo Fanti, akisisitiza jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati walipokutana na kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9), Mkoani Morogoro.

Mbunge wa Kilombero, Mhe. Abubakar Asenga, akizungumza jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati wakikagua ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9), Mkoani Morogoro.

Mhandisi Mkazi kutoka Kitengo Maalum cha Wahandisi Washauri cha TANROADS (TECU), Eng. Anorld Maeda, akifafanua jambo kwa Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya Nchini Tanzania Mhe. Manfredo Fanti na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati walipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9), Mkoani Morogoro.

PICHA NA WUU

Serikali imesema inaendelea kutatua changamoto zilizokuwa zinaufanya mradi wa ujenzi wa barabara ya Kidatu hadi Ifakara (km 66.9), kusuasua na kuwaahidi wananchi wanaotumia barabara hiyo kuwa mradi unaendelea na utakamilika kwa ubora na viwango vilivyowekwa.

Hayo yameelezwa mkoani Morogoro na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alipotembelea  mradi huo na kuona hatua maendeleo yake akiambatana na Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini Tanzania ambao ndio wafadhili wa mradi huo.

Amesema kuwa barabara hiyo iliyoanza mwaka 2017 ilikuwa ikamilike miaka michache iliyopita lakini kumekuwa na changamoto ambazo zilisababisha kazi ichelewe ikiwemo usimamizi wa mradi pamoja na uwezo wa mkandarasi kutokuwa na kasi ya ujenzi kama ilivyotarajiwa.

“Nawahakikishia wananchi wa Kilombero na wote wanaotumia barabara hii kuwa sasa barabara inakwenda kumalizika kwa kiwango cha lami”, amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amesema lazima tukubali kuwa mradi huu umetupa changamoto nyingi lakini hatutaki kurudi nyuma kwani nia ya wananchi na Serikali ni kuona barabara hi inakamilika kwa viwango vilivyokusudiwa.

Naye, Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya Nchini Tanzania, Mheshimiwa Manfredo Fanti, ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya mkoa wa Morogoro na hivyo amewahakikishia watanzania kuwa Umoja umejitoa kikamilifu kwa kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha mradi huo sasa unakwenda kukamilika hivi karibuni.

Akitoa taarifa ya mradi, Mhandisi Mkazi kutoka Kitengo Maalum cha Wahandisi Washauri cha TANROADS (TECU), Eng. Anorld Maeda, ameeleza kuwa mradi umefikia asilimia 54.5 na wanaendelea kumsukuma mkandarasi akamilishe kwa muda uliopangwa na ubora.

“Ni miezi saba toka tulivyoupokea mradi huu kwa Mhandisi Mkazi alliyeondoka ukiwa na asilima 33 na sasa kazi zinaendelea vizuri ambapo ujenzi wa Daraja la Ruaha Mkuu (m 130), umefikia asilimia 50, madaraja mengine manne asilimia 78, maboksi kalvati asilimia 67 na pipe kalvati asilimia 72”, amesema Eng. Maeda.

Kwa upande wake Mbunge wa Kilombero, Mhe. Abubakar Asenga, ameshukuru ujio wa Balozi  pamoja na Waziri wa Ujenzi kwa kutembelea mradi huo na kuzidi kusukuma ujenzi huo ambao wana kilombero wana imani ndani ya mwaka mmoja barabara hiyo itakamilika na kusaidia kuchochea maendeleo kwa wananchi wake.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hanji Godigodi, ameeleza kuwa barabara hiyo ikikamilika itakuwa mkombozi sana kwa wananchi na itapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za usafiri na usafirishaji wa abira na mazao.

Zaidi ya Shilingi Bilioni 100 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9) ambazo ni ufadhili toka nchi za Umoja wa Ulaya, USAID na UKAID.

Thursday, 27 January 2022

NAIBU WAZIRI MWAKIBETE AIPONGEZA TCAA KWA UKUSANYAJI WA MAPATO

 

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, akisisitiza jambo kwa Mwongoza Ndege Mwandamizi, Bw. Shukuru Nziku, wakati alipotembelea Chuo cha Usafiri wa Tanzania (CATC), jijini Dar es Salaam.



Mkuu wa Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC), Aristid Kanje (wa kwanza kulia), akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete (wa pili kushoto), kuhusu mipango ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kujenga madarasa, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya kujenga madarasa hayo jijini Dar es Salaam. 


Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, akisisitiza jambo kwa wanafunzi wanaosoma Chuo cha Usafiri wa Tanzania (CATC), jijini Dar es Salaam.

Mkurungenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Hamza Johari akitoa maelezo juu ya uendeshaji wa mamlaka hiyo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi) Atupele Mwakibete mara baada kutembelea Makao Makuu ili kujifunza ufanyaji kazi wake

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete (wa tatu kulia), katika picha ya pamoja na Menejimenti  ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzanai (TCAA), mara baada ya kutembelea Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam. 



Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, ameipongeza Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzanai (TCAA), kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kupitia Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC), ambapo katika mwaka huu wa fedha 2020/21  kimeweza kukusanya takribani Shilingi Bilioni 2 kutoka Milioni 500 zilizokusanywa 2017/2018 na hivyo kuongeza mapato ya Mamlaka kufikia zaidi ya Bilioni 45 kwa mwaka.

Ameongeza kuwa makusanyo hayo yametokana na uwepo wa miundombinu bora ya chuo  hicho kuwa ya kisasa ikiwemo mifumo ya kisasa ya mafunzo kwa vitendo (Simulator) za kufundishia kozi mbalimbali chuoni hapo.

Akizungumza hayo jijini Dar es Salaam, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea Mamlaka hiyo na chuo hicho ambapo pamoja na mambo mengine ameipongeza TCAA kwa kuweka mikakati thabiti katika uthibiti katika usafiri wa anga na kuitaka mamlaka kuendelea kuwekeza katika wataalam ili kukidhi mahitaji ya udhibiti.

“Nakupongeza sana Mkurugenzi Mkuu kwa kuweka mikakati mizuri ya mwendelezo wa taasisi yako, nimefarijika sana kusikia mna miradi ambayo mnaitekeleza kwa kutumia fedha zenu wenyewe kama mradi ya rada nne, hili ni la kupongeza”, amesisitiza Naibu Waziri Atupele.

Akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Bw. Hamza Johari, amesema pamoja na ongezeko la mapato ya Mamlaka iko kwenye hatua mbalimbali ya kujenga majengo ya kisasa ambayo yatarahisisha utoaji wa elimu chuoni hapo.

“Idadi ya wanafunzi tunaopokea imekuwa ikiongezeka na kama ulivyoona tuna madarasa machache sana, ila mipango iliyopo kwa sasa ni hukakikisha tunajenga majengo kwenye eneo uliliona ili wanafunzi wetu wasome kwenye mazingira rafiki", amesema Bw. Johari.

Vilevile Mkurugenzi Mkuu amesema pamoja na kuimarisha chuo hicho ambacho kimekuwa sehemu ya pato kwa Mamlaka, mipango mingine iliyowekwa katika kuboresha utendaji ni kuongeza wataalam kwenye fani mbalimbali ili kwenda sambamba na maboresho yanayofanywa na Serikali kuboresha usafiri wa anga.

Naibu Waziri Atupele yuko mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya kutembelea, kufahamiana na kuzungumza na viongozi na watumishi waliopo katika taasisi za Sekta ya Uchukuzi na pamoja na kukagua miradi ya kisekta. 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikali, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Sunday, 16 January 2022

PROF. MBARAWA AWATAKA BANDARI KUJIPANGA UBORA WA MIUNDOMBINU


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa (kulia), akimsikiliza Kaimu Meneja wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSC), mkoa wa Kigoma, alipomweleza kuhusu hatua ya Ukarabati wa Meli ya MT. Sangara mkoani Kigoma, wakati alipotembelea mradi huo.


Muonekano wa meli ya MT. Sangara ambayo ukarabati wake umefikia asilimia 40 na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu.



Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akiangalia sehemu ya miundombinu ya bandari ya Ujiji Mkoani Kigoma ambayo ujenzi wake kwa sasa umefikia asilimia zaidi ya 50 wakati wa ziara yake. 


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kusimamia miradi ya miundombinu kikamilifu kwa kwa kuweka mikakati maalum ya kuitembelea na kufanya vikao vya mara kwa mara ili kuwezesha miradi hiyo kukamilika kwa wakati na viwango. 

Akizungumza Mkoani Kigoma leo baada ya kukagua mradi wa upanuzi wa bandari za Kibirizi na Ujiji Prof. Mbarawa ametoa rai kwa TPA kupitia upya miradi ya wanayotekeleza nchini kote na kwa kuchukua hatua stahiki ikiwemo kuongeza idadi ya wahandisi kweye miradi hiyo. 

“Mamlaka ina miradi nchi nzima lakini miradi niliyotembelea leo ya bandari za ziwa Tanganyika imekuwa ikisuasua sana, mhandisi mshauri anaandika barua ya vikao TPA hamuonekani, kwa namna hii hatutafika na sio sawa’ Amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa. 

Prof. Mbarawa amebainisha kuwa kukamilisha kwa miradi hiyo kutarahisisha shughuli za usafirishaji baina ya Kigoma na nchi Jirani zinazozunguka Mkoa huo ikiwemo Jamhuri ya Kidekrasia ya Kongo (DRC) na Burundi kwani kupitia bandari hizi usafirishaji utarahisishwa. 

Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amekagua maendeleo ya ukarabati ya Meli ya MT Sangara na kuitaka Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kusimamia mradi huo kwa kukagua kila hatua ya ukarabati huo ili kupata thamani ya fedha na kuepuka kufungiwa vipuri visivyokidhi vigezo kulingana na mkataba. 

Naye Meneja wa Bandari ya Kigoma, Manga Gasaya amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa ndani ya wiki mbili kuanzia sasa tathmini itafanyika na Mamlaka itatoa taarifa ya mikakati iliyojiwekea kukamilisha miradi hiyo ikiwemo ratiba za ukaguzi. 

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Allen Butembelo amesema ukarabati wa meli ya MT. Sangara umefikia asilimia 40 na kuahidi kuendelea kuusimamia ili ukamliike kwa wakati.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa yuko Mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine atashiriki kikao kitakachowakutanisha Mawaziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Fedha wa Tanzania na Burundi kujadili miradi ya maendeleo hususani Reli ya Uvinza-Musongati-Gitega.

Saturday, 15 January 2022

UJENZI RELI YA UVINZA-MUSONGATI-GITETA WAIVA


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akisisitiza jambo katika kikao kilichowakutanisha Mawaziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Fedha na Mipango wa Tanzania na Burundi kujadili mradi wa Ujenzi wa Reli ya kisasa toka Uvinza-Musongati-Gitega KM 282 kilichofanyika mkoani Kigoma, (Kushoto) ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba. (Kulia), ni Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dkt. Jily Maleko.



Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba akisisitiza jambo katika kikao kilichowakutanisha Mawaziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Fedha na Mipango wa Tanzania na Burundi kujadili mradi wa Ujenzi wa Reli ya kisasa toka Uvinza-Musongati-Gitega KM 282 kilichofanyika mkoani Kigoma.



Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) wakitia saini za awali za makubaliano ya pamoja ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Uvinza Tanzania hadi Gitega Burundi yenye urefu wa kilomita 282, mjini Kigoma.


Mawaziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Fedha na Mipango wa Tanzania na Burundi katika picha ya pamoja baada ya kusaini mkaubaliano ya awali ya mradi wa Ujenzi wa Reli ya Uvinza-Musongati-Gitega, uliofanyika mkoani Kigoma.

Tanzania na Burundi zimeingia makubaliano ya awali ya utekelezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Uvinza-Musongati hadi Gitega nchini Burundi.  Ujenzi wa reli hiyo utakapokamilika unatarajiwa kuimarisha huduma za uchukuzi kati ya Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano ya awali Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Tanzania, Prof. Makame Mbarawa amesema ujenzi wa reli hiyo ya kisasa unatarajiwa kuwa na urefu wa Kilomita 282 ambayo ni mwendelezo wa ujenzi wa reli ya SGR sehemu ya Tabora hadi Uvinza inayotarajiwa kupata Mkandarasi hivi karibuni.

Ujenzi huo umegawanywa katika sehemu mbili ambazo ni Uvinza hadi Malagarasi kwa upande wa Tanzania yenye urefu wa Kilomita 156 na Maragasi-Musongati hadi Gitega yenye urefu wa Kilomita 126.

Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa ujenzi wa reli hiyo utakuwa na manufaa kwa nchi za Tanzania na Burundi na utaibua fursa nyingi za ajira na biashara hivyo kukuza uchumi kwa wakazi wake.

“Usafiri wa reli ndio usafiri rahisi duniani hivyo reli hii itakayojengwa kwa ushirikiano itajengwa kwa viwango na uharaka kutokana na mahusiano mazuri ya nchi zetu mbili’, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amesisitiza reli hiyo itakapokamilika itawezesha treni ya abiria kuwa na spidi ya kilomita 160 kwa saa na treni ya mizigo kuwa na spidi ya kilomita 120 kwa saa na itatumia umeme hivyo kuongeza chachu na uharaka na huduma za uchukuzi nchini.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa reli hii kunaongeza kasi ya mchakato wa utafutaji wa fedha na kusisitiza kuwa reli hiyo itajengwa kama ilivyopangwa.

Amesisistiza kuwa fedha za utekelezaji wa mradi huo zitapatikana na mradi utaanza kwa wakati kama Serikali ilivyojipanga na hivyo kuweka historia ya mataifa mawili kushirikiana kujenga reli na kukuza uchumi wa wananchi wake.

Waziri Dkt. Mwigulu amesema kuwa uwepo wa madini mengi kutoka Burundi kutawezesha reli hiyo kuwa na mzigo wa kutosha wa kusafirisha kwenda bandari ya Dar es Salaam na hatimaye kuongeza pato la Taifa.

Kwa upande wake Waziri wa Miundombinu wa Burundi, Dkt. Deo Nsanganiyumwani amesema kuwa ujenzi wa reli hiyo ni sehemu ya mikakati ya nchi hizo kukuza uchumi na kuimarisha ushirikiano baina ya wananchi wake.

Ujenzi wa Reli ya Uvinza-Musongati hadi Gitega ni muendelezo wa  mikakati wa Serikali ya Tanzania kuhakikisha nchi hiyo inaunganishwa na nchi jirani ili kuwezesha mzigo mwingi unaopitia bandari ya Dar es salaam kwenda nchi jirani unatumia usafiri wa reli ambao licha ya kubeba mzigo mkubwa mara moja pia ni nafuu na wa haraka zaidi.

Imetolewa na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini Wizara Ya Ujenzi Na Uchukuzi

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA