Tuesday, 30 May 2023

UPWEKE, VIASHIRIA VYAKE, VYANZO VYAKE, MADHARA YAKE NA UFUMBUZI WAKE



Upweke hutokea kwa watu wote ulimwenguni kwa sababu ni sehemu ya maumbile ya binadamu.

Upweke sio hali ya kuwa pekeako hata ukiwa  umejumuika na  watu lakini unajiona tofauti sana na wao au kujiona hueleweki 

Upweke unaweza kukupata labda upo na fedha nyingi sana,au cheo, umaarufu,nguvu kubwa sana ya ushawishi katika jamii lakini kila mtu anajua upo na furaha sana saa 24 hivyo ukianza kusimulia matatizo yako watu wanaona unaigiza maisha au kufanya dhihaka hivyo hawasikilizi chochote hivyo huwezi kueleza hisia zako kwa mtu yeyote

Upweke unaweza kujitokeza kwa sababu upo na marafiki wengi sana wenye mafanikio makubwa lakini hamna muda wa kuzungumza kuhusu maisha nje ya fedha na biashara hivyo huwezi kuzungumza chochote kuhusu upweke wako kwa mtu yeyote

Upweke kupita kiasi unaweza kuja kwa sababu upo na watu wengi sana ambao wanataka kunufaika na uwepo wako tu ila hawana msaada wowote kwako .

Upweke kupita kiasi unaweza kuja kwa sababu upo na uongozi na watu hawataki uongozi wako au hupati ushirikiano wowote kutoka kwa watu wapo chini yako hivyo unaweza kujichukia kupita kiasi na kuwa na hasira kupita kiasi na kuwa mkali kupita kiasi au kuanza ulevi kupindukia ili  kujipa faraja bila mafanikio.

Upweke ni sehemu ya maumbile ya binadamu lakini upweke kupita kiasi ni hatari sana kiafya na katika mahusiano husababisha ugomvi wa mara kwa mara.

Tafiti zinaonyesha kwamba upweke kupita kiasi husababisha uvimbe mwilini (Cole et al  2007)

Vilevile tafiti hizo zinaonyesha kwamba upweke kupita kiasi husababisha uwezekano wa mtu kupata asthma na Autoimmune disorder.

Hatuwezi kuzuia upweke kwa sababu ni jambo litatokea kwa kila mtu kwa njia mbalimbali kama kifo cha umpendaye, kusafiri kwa umpendaye,kuoa au kuolewa kwa marafiki zako au ndugu zako wa familia moja,kuanza masomo mbali na nyumbani n.k

Kabla ya kujua viashiria vya upweke kupita kiasi jibu maswali yafuatayo kujua hali ya upweke wako kwa sasa



Andika NDIYO au HAPANA kulingana na hali yako ya sasa

1.Sina watu wa kuzungumza nao au kushirikiana kufanya kazi?

2.Nikihitaji msaada sioni mtu yeyote wa kumuomba msaada?

3.Sina marafiki wa karibu?

4.Najiona kama nimetengwa ?

5.Sijioni kama mimi ni sehemu ya jamii yangu ?

6.Sina mtu yeyote wa kuzungumza nae?

7.Nipo na mahusiano ya juu juu na watu wengine?

8.Napata wakati mgumu sana kuanzisha urafiki na watu wengine?

9.Sipati mualiko sehemu yoyote?

10.Najiona mpweke muda wote?

11.Naona hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kunielewa?



Kama umejibu NDIYO maswali mengi ni wazi kwamba upo na UPWEKE KUPITA KIASI na itakuwa sababu ya kung'ang'ania mahusiano yenye migogoro au kuamua kuishi pekeako pekeako.


VIASHIRIA VYA UPWEKE KUPITA KIASI

a.Hauna mahusiano mazuri na mwili wako mara kwa mara unajilaumu, kujikosoa,kuona aibu, kujichukia sana,kujipa majina mabaya kama ukifanya makosa


b.Kujiona mbaya sana wa muonekano,kujiona upo na dosari nyingi sana na makosa makubwa sana kuliko wengine,kukuza sana makosa yako na kushusha thamani mafanikio yako

c.Kuona wivu kupita kiasi kwa mahusiano ya watu wengine, kutarajia kuumizwa, kusalitiwa, kutelekezwa kama utampenda mtu yeyote,kushindwa kuamini watu wengine

d.Hofu kubwa sana ya kukosolewa, hofu ya kufokewa,hofu ya kujibiwa vibaya kama utaomba kitu chochote, kujitenga kupita kiasi,kulia mara kwa mara kwa vitu vidogo vidogo sana,kujiona huna thamani wala athari yoyote kwa watu wengine,kujiona mzigo sana.

e.Kupata wakati mgumu sana kukabiliana na matatizo yako,kupata mshtuko mkubwa sana kwa taarifa mbaya,kukwepa matatizo,

f.Kuwajibu vibaya sana watu wengine wakifanya utani juu yako,ukikosolewa unakuja juu sana kwa jazba kujihami na kumshambulia mwenzako 

g.Kuogopa kuwa na furaha,kukataa mualiko, kukataa msaada, kukataa kupewa ushauri,kujitenga na kila mtu anataka kujenga mahusiano na wewe 

h.Kupoteza matumaini ya kuishi,kuwa na hasira kupita kiasi kwa vitu vidogo vidogo, kuhuzunika sana muda wote,kushindwa kusamehe makosa yako na makosa ya wengine

I.Kufanya mazungmzo ya juu juu tu kuepuka kuzungumza habari zenye kukumbusha tukio la kuumiza,kuomba msamaha mara kwa mara au kugombana na kila mtu kila siku

j.Kushindwa kuvumilia mapungufu ya wengine, kuhisi hakuna mtu yeyote anakupenda na kukuheshimu, kujilinganisha na wengine kisha unajiona mnyonge sana

k.Kufikiria sana makosa yako,fursa ulizopoteza na kufeli kwako,kuona kwako matatizo yanazidi kuongezeka kila siku,kushindwa kuona kitu chochote kizuri upo nacho 

l.Kupoteza hisia za mapenzi, kutamani kujiua, kuumia kooni, kutetemeka sana, miguu kuishiwa nguvu, kutokwa jasho bila joto, kupoteza hamu ya kula au kula sana vyakula bila mpangilio,kutumia pesa nyingi sana ghafla,kushindwa kufanya kazi,kushindwa kufanya usafi binafsi

m.Kupaniki haraka sana,kushindwa kumeza mate,kuumia kooni, kuhisi uchungu moyoni,hisia za kisasi, kizunguzungu, kuchanganyikiwa, kupoteza hisia kwenye vidole,mwili kufa ganzi, kichefuchefu, mwili kukosa nguvu kabisa, uchovu mwili mzima, kubanwa kifua, pumzi kuwa ngumu.



VYANZO VYA UPWEKE KUPITA KIASI

Upweke kupita kiasi unaweza kusababishwa na vyanzo vifuatavyo

a.MAHUSIANO

Matukio yenye kusababisha upweke kupita kiasi ni kumfumania mwenza wako,ugomvi wa mara kwa mara na mwenza wako, mahusiano kuvunjika ghafla,kifo cha ghafla cha mwenza wako,ugomvi wa mara kwa mara na  mama/baba yako mzazi au mkwe, mawasiliano kupungua ghafla kati yako na mwenza wako

b.MATATIZO YA KIFEDHA

Upweke kupita kiasi unaweza kusababishwa na kupitia kipindi kigumu sana kifedha kama vile marafiki zako wote wanashiriki harusi na kutoa michango lakini wewe huwezi kuchangia harusi, kufukuzwa kazi, biashara kukosa wateja,madeni makubwa sana,

c.MATATIZO YA KIAFYA

Unaweza kujichukia kupita kiasi kwa kujiona mpweke sana kwa sababu ya kuugua muda mrefu sana bila kupata nafuu, kuambukizwa ugonjwa usiokuwa na tiba,kutokwa harufu mbaya sana sehemu za siri,ngozi kuharibika sana baada ya ajali au ugonjwa ,kupata ajali yenye kusababisha ulemavu wa kudumu, màumivu makali sana ya mifupa, ujauzito kuharibika mara kwa mara, umri kuzidi kuongeza bila kuzaa.

d.MALEZI YA UTOTONI

Unaweza kujiona mpweke sana hata kwenye vyombo vya usafiri,upweke kupita kiasi unaweza kujitokeza hata ukiwa kiongozi mkubwa, unaweza kujiona mpweke sana hata kama upo na mamilioni ya fedha kwa sababu ya kumbukumbu za malezi ya utotoni kama vile

a.ADHABU KUPITA KIASI

kama utotoni mwako umeishi huku unapigwa sana, kufokewa sana, kutukanwa, kudhalilishwa, kukataliwa kushambuliwa kwa maneno makali sana husababisha upweke kupita kiasi mpaka uzeeni

b.UPENDELEO KUPITA KIASI

Kama utotoni mwako umeishi huku unajiona laana katika familia labda kwa sababu ya muonekano, ufaulu duni,jinsia ,makosa ya mara kwa mara n.k husababisha unajiona mnyonge sana hata ukiwa na kila kitu uzeeni.

c.UMASIKINI KUPITA KIASI

Kama utotoni mwako umeishi maisha ya kimaskini kupita kiasi,labda ulikuwa hupati chakula, ulivaa nguo chafu, ulitembea bila viatu, ulikosa mtu wa karibu wa kuzungumza nae ukiwa na maumivu,hukupata faraja ukiwa mgonjwa hali hiyo husababisha upweke kupita kiasi mpaka uzeeni.

d.UGOMVI WA WAZAZI

kama utotoni mwako umeishi huku unaona wazazi mara kwa mara wanagombana, kutukanana, kujibizana, kupeana vitisho, kupeana tuhuma nzito, kuitana majina ya aibu husababisha maumivu makali sana moyoni na upweke kupita kiasi hata ukiwa na uongozi mkubwa bado unaogopa kueleza historia yako kwa watu wengine kwa kuona aibu hivyo unakuwa mpweke sana ukiwa na marafiki.



MADHARA YA UPWEKE KUPITA KIASI

a.Mahusiano

Upweke kupita kiasi husababisha mtu kujenga mahusiano ya juu juu ili kuepuka kukataliwa,kuepuka kuumizwa na wengine kama mahusiano yatavunjika.Madhara yake unakuwa hujui nani rafiki yako ukiwa na matatizo umuone 


Upweke kupita kiasi husababisha mtu kuvumilia manyanyaso katika mahusiano yake hata ukiwa na mamilioni ya fedha bado huwezi kuvunja mahusiano ambayo unapitia manyanyaso 


b.Kiafya

Upweke kupita kiasi husababisha kinga ya mwili kushuka haraka sana na kufanya mwili kuwa hatarini kupata magonjwa mbalimbali kama kisukari, madonda tumbo, uvimbe, shinikizo la damu, asthma, Autoimmune disorder, maambukizo ya magonjwa ya zinaa,uzee wa haraka au kifo cha ghafla,kuumwa kichwa na mgongo,kushindwa kufurahia maisha hata ukiwa na mafanikio makubwa sana kuliko wengine,,kwa wanawake hedhi kuvurugika na ujauzito kuharibika,

Upweke kupita kiasi husababisha watu kuingia kwenye ulevi kupindukia, matumizi ya bangi au dawa za kulevya,kuzaa na mtu yeyote.



UFUMBUZI WAKE

a.TUMIA UPWEKE KAMA HAMASA

anza kwa kufanya vitu vya kumbukumbu za baadaye kupitia upweke kwa mfano huna marafiki anza kujifunza ujuzi mpya,jipe zawadi,anzisha project za maendeleo,


b.RIHUSU MÀUMIVU MAKALI

Ruhusu machozi kutoka machoni mwako.Kulia husaidia kuondoa sumu mwilini.Unaweza kuomboleza ikiwa mahusiano yamevunjika au msiba 


Fanya mazoezi ya viungo,tembea tembea,kaa Juani asubuhi,kunywa maji mengi,oga maji ya baridi au moto,kula chakula kizuri kiafya,vaa nguo nzuri ,soma vitabu


c.TAFUTA UFUMBUZI WA MATATIZO YAKO

Anza kwa kufanya tafiti kujua chanzo cha tatizo lako kisha anza kukabiliana na matatizo yako moja baada ya lingine utajenga uwezo. Wa kujiamini haraka sana.


Andika kwenye karatasi matatizo yako yote na màumivu makali ambayo unapitia .Andika màumivu yako na matatizo yako kwa hisia kali sana.

Anza kushiriki kazi za kijamii,nenda sehemu zenye mikusanyiko anza kusalimia mtu yeyote kisha sogea kwa mtu mwingine kisha mwengine utaondoa upweke

Kama tatizo lako ni kubwa zaidi tunaweza kuwasiliana kwa  ajili ya Counselling session na ufafanuzi wa kilichoandikwa hapo juu na utaona mabadiliko na kujisikia nafuu ndani ya muda mfupi baada ya mazungumzo.


0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA