TCAA NA UMOJA WA ULAYA WATHIBITISHA DHAMIRA YA KUIMARISHA USIMAMIZI WA USALAMA WA USAFIRI WA ANGA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Dkt. Jabiri K. Bakari, amethibitisha dhamira ya Mamlaka hiyo ya kujenga Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya kiwango cha kimataifa barani Afrika, yenye matarajio ya kufikia viwango vinavyolingana na mamlaka za usafiri wa anga za Ulaya katika ubora wa udhibiti, umahiri wa kitaalamu, ufanisi wa kiutendaji na usimamizi wa usalama wa anga.
Alitoa kauli hiyo wakati wa kikao cha kuhitimisha ujumbe wa wataalamu wa msaada wa kujengeana uwezo kutoka Shirika la Usalama wa Anga la Umoja wa Ulaya (EASA), kilichofanyika tarehe 3 Septemba 2026 katika Makao Makuu ya TCAA jijini Dar es Salaam. Dkt. Bakari aliushukuru Umoja wa Ulaya kwa kuendelea kutoa msaada na kuonyesha imani katika maendeleo ya Tanzania. Pia alieleza juhudi zinazofanywa na TCAA kuimarisha mifumo yake ya usimamizi, ikiwemo uundaji na utekelezaji wa Mfumo wake wa ndani wa TCAA wa Huduma za Usafiri wa Anga (Civil Aviation Services Portal – CASP), ambao ulipewa pongezi na timu ya EASA.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Dkt. Jabiri K. Bakari akizungumza wakati wa kikao cha kuhitimisha ujumbe wa timu wataalam kutoka Shirika la Usalama wa Anga la Umoja wa Ulaya (EASA)
Timu ya EASA ilieleza kuridhishwa kwake na maendeleo na juhudi zilizooneshwa na TCAA wakati wa ziara hiyo ya siku tatu. Aidha, timu hiyo ilitambua maendeleo yaliyofikiwa na kuhimiza TCAA kuendeleza kasi katika kushughulikia masuala yote muhimu ya usimamizi wa usalama wa anga.
Kwa upande wake Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya alithibitisha dhamira ya EU ya kuendelea kuisaidia Tanzania kupitia msaada wa kitaalamu, mbinu za utekelezaji wa vitendo na kubadilishana ujuzi. Aidha, alieleza kuwa Umoja wa Ulaya umetenga Euro milioni 2 kwa ajili ya msaada unaohusiana na kuboresha zaidi Masuala ya usafiri wa anga nchini.
Ujumbe wa EASA uliongozwa na Bw. Jose Miguel Manso Angulo akiambatana na Bw. Gustavo Juan Roman Barba na Bw. Antonio Portales Pelaez.
Ujumbe huo, uliopo nchini kwa siku tatu kuanzia tarehe 1 hadi 3 Septemba 2026, ulifuatilia maendeleo ya Nchi (State) katika utekelezaji wa hatua za marekebisho pamoja na kuimarisha usimamizi wa usalama wa Usafiri wa anga. Majadiliano yalihusu maeneo ya ki sheria, muundo wa taasisi, uchunguzi wa ajali ndege, utoaji wa leseni kwa eneo la rasilimali watu la Usafiri wa anga, ubora wa ndege kwa matumizi (airworthiness) na uendeshaji wa ndege, pamoja na kufanya vikao na waendeshaji wa mashirika ya ndege kuhusu hoja zilizobainishwa, Mipango ya Hatua za Marekebisho (Corrective Action Plans) na ufuatiliaji wa utekelezaji wake.
Ujumbe huo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za Tanzania za kuimarisha usimamizi wa usalama wa Usafiri wa anga na kuonesha maendeleo endelevu kuelekea kutimiza matakwa ya kuondolewa kwenye Orodha ya Usalama wa Anga ya Umoja wa Ulaya (European Union Air Safety List).




0 comments:
Post a Comment