WITO:::Watanzania kuleni nyama ya panya.
Watanzania wameshauriwa kufuga na kula panya aina ya ndezi wakieleza kuwa nyama hiyo haina mafuta mengi, ikiwa pia na virutubisho muhimu na vilivyo adimu.
Rai hiyo imetolewa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) katika Maonyesho ya Vyuo Vikuu nchini yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Wataalamu hao walisema kuwa ili kukabiliana na uharibifu wa kuchoma moto misitu kwa ajili ya kuwatafuta wanyama hao, ni vyema wananchi wakaanza kuwafuga kwa kuwa nyama yao ina ladha nzuri na ni laini.
Mhadhiri
Mwandamizi wa SUA, Idara ya Uzalishaji, Mirende Matiko alisema kuwa
ingawa wanyama hao wanafugwa kwa wingi katika nchi za Afrika Magharibi,
hapa nchini ufugaji wake unakabiliwa na changamoto nyingi.
"Wakulima
wetu hapa tunawapa wafuge, siku chache baadaye ukienda utaambiwa
walikufa, lakini ukiwauliza majirani wanakuwambia 'jamaa aliwachinja',
ni sawa na kumpa mkulima mbegu halafu anakula," alisema Matiko.
Akizungumzia
namna nyama hiyo inavyoliwa, Matiko alisema: " Nyama yake ina
viinilishe vingi, yanatupwa manyoya na miguu yake tu, vitu vingine vyote
vinaliwa. Tena utumbo ndiyo mtamu sana, si unajua wanakula nyasi tu."
Alisema
wanyama hao wana faida nyingi kiuchumi ikiwamo kuongeza pato la kaya,
kuchangia uwindaji endelevu, kutunza bioanuwai pia nyama yao ni gharama
nafuu, ikilinganishwa na nyingine.
"Mtu
akitaka kufuga wanyama hao anatakiwa kuwa na banda madhubuti lenye
ubora, chakula na maji safi yawepo bandani muda wote na upandishaji
ufanyike katika muda mwafaka," alisema.
Mhadhiri
huyo alitoa hadhari kwa wafugaji akiwataka kuwakamata wanyama hao kwa
umakini kutumia chandarua, kuepuka kusababisha majeraha.
Ndezi ni
jamii ya nungunungu na pimbi, wakiwa wa aina mbili, ambapo wadogo huwa
na uzito wa kati ya kilo nne hadi sita na wakubwa hufikia hadi kilo
tisa. Wanyama hao hupendelea kuishi kwenye maeneo yanayolimwa mashamba
ya miwa, ulezi na mpunga.
Hata
hivyo, Dk Loth Mulungu alisema kuwa wawindaji wa ndezi porini
husababisha madhara makubwa ikiwamo uchomaji wa misitu, uharibifu wa
bioanuwai, kukanyaga mazao mashambani na upotevu wa muda.
Mmoja wa
watazamaji waliotembelea Banda la SUA, Elizabeth Maro alisema kuwa
ingawa kwa muda mrefu amesikia watu wakila mnyama huyo. Binafsi hawezi
kula nyama yake kwa kuwa anaamini hana tofauti na panya wengine.
"Siwezi
kumla kwa namna yoyote, huyu ni panya tu ndiyo maana hata jina lake kwa
Kiingereza anaitwa 'canerat', maana yake panya mla miwa," alisema.Ipyana
Mwambungu alisema mnyama huyo ameadimika katika baadhi ya mikoa
kutokana na watu wengi kuipenda nyama yake.
"Kuna baadhi ya maeneo kule Kilimanjaro huwezi kuwaona tena ndezi, wakati zamani walikuwa wengi sana," alisema.
CHANZO MWANANCHI
CHANZO MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment