RAIS JAKAYA KIKWETE ASAMEHE WAFUNGWA 4969
RAIS Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 4,969 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 53 ya Uhuru.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, iliyotolewa Dar es Salaam
jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe alisema msamaha huo
utawahusu wafungwa 4,969, ambapo 887 kati yao wataachiwa huru na
wafungwa 4,082 watapunguziwa vifungo vyao na kubaki gerezani wakitumikia
sehemu ya kifungo kilichobaki.
Alisema wafungwa waliopata msamaha ni wale wanaougua magonjwa ya
Ukimwi, TB na saratani, ambao wako kwenye ‘terminal stage,’ na wafungwa
hao watathibitishwa na jopo la waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu
wa Mkoa au Wilaya.
Wafungwa wengine ni wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi; na umri
huo pia utathibitishwa na jopo la waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga
Mkuu wa Mkoa au Wilaya na wafungwa wa kike walioingia gerezani, pamoja
na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.
Wengine waliopata msamaha ni wenye ulemavu wa mwili na akili na
ulemavu huo utathibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa
Mganga Mkuu wa Mkoa na Wilaya.
Hata hivyo, msamaha huo hautahusisha wafungwa waliofanya makosa na
kuhukumiwa kunyongwa, waliohukumiwa adhabu ya kifo na adhabu hiyo
ikabadilishwa kifungo, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na
biashara ya dawa za kulevya.
Wengine ni wale ambao wanatumikia kifungo kwa makosa ya kupokea na
kutoa rushwa, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia
silaha na wafungwa wanaotumia kifungo kwa maoksa ya kupatikana na silaha
au risasi.
Wafungwa wengine ambao hawatahusishwa na msamaha huo ni wanaotumikia
kifungo kwa kosa kuwapa mimba wanafunzi wa shule ambao walitenda kosa
hilo wakiwa na umri wa miaka 18 na kuendelea, wanaotumikia kifungo kwa
makosa ya wizi wa magari kwa kutumia silaha, wanaotumikia kifungo chini
ya Sheria ya Bodi ya Parole na Sheria ya Huduma kwa jamii na wafungwa
waliowahi kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali ambao
watatumikia kifungo hicho gerezani.
Wengine ambao hawatafaidika na msamaha huo ni wafungwa wanaotumikia
kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madarakani yao, wafungwa waliowahi
kupata msamaha wa Rais na ambao bado wapo gerezani kutumikia sehemu ya
kifungo kilichobakia, wanaotumikia kifungo kwa kosa la kufanya biashara
haramu ya binadamu na wanaotumikia vifungo kwa kosa la kupatikana na
nyara za serikali.
0 comments:
Post a Comment