PROFESA ANNA TIBAIJUKA AFIKISHWA KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA KULA FEDHA ZA ESCROW
BARAZA la Maadili ya Viongozi wa Umma, limemsomea rasmi mashitaka
aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka (pichani), na kubainisha kuwa kiongozi huyo anastahili kujibu
mashitaka kwa kosa la kuomba na kujipatia fedha kinyume na Sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma.
Hata hivyo, Profesa Tibaijuka alikana mashitaka hayo, na kusisitiza
kuwa hakukiuka maadili hayo ya viongozi wa umma, kwa kuwa fedha hizo
hakuziomba kwa maslahi yake binafsi, bali kwa ajili ya kuendeleza na
kuboresha taasisi yake inayotoa huduma ya elimu kwa watoto wa kike wasio
na uwezo lakini wenye vipaji.
Akimsomea mashitaka hayo mbele ya baraza hilo, Mwanasheria wa
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Wemaeli Mtei alisema
Profesa Tibaijuka ambaye ni kiongozi wa umma, alishawishi na kuomba
fedha na baadaye kupokea Sh bilioni 1.6 kutoka kwa James Rugemalira na
mkewe.
Aidha, Sekretarieti hiyo kupitia shahidi wake ambaye ni Katibu
Msaidizi wa Idara ya Viongozi wa Siasa kutoka Sekretarieti hiyo, Waziri
Kipacha, alisema kupitia Kamati ya Uchunguzi iliyoundwa na sekretarieti
kufuatilia sakata hilo, ilibaini kiongozi huyo aliomba na kupokea fedha
hizo kupitia barua aliyoandika Februari 4, mwaka 2012.
“Tulibaini kuwa fedha alizoomba mlalamikiwa zilitumwa kwake kupitia
akaunti yake namba 00120102640201 ya Benki ya Mkombozi iliyopo St Joseph
jijini Dar es Salaam,” alisema huku akikabidhi baraza hilo barua hiyo
ya Tibaijuka ya kuomba fedha na taarifa za kibenki kama ushahidi.
Alisema pamoja na hayo, kamati hiyo pia katika uchunguzi wake
ilibaini mlalamikiwa ni mmoja wa wadhamini katika Bodi ya Wadhamini ya
Taasisi ya Barbro Johansson Girls Education Trust, ambapo barua kutoka
Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), ilithibitisha suala hilo.
Na kwamba wamiliki wa shule hiyo ndiyo wadhamini.
“Tumebaini kuwa mlalamikiwa alipokea kiasi hicho cha fedha na wadhifa
aliokuwa nao kama Waziri, jambo lililomwingiza katika mgongano wa
kimaslahi,” alisema.
Alisema kitendo cha mlalamikiwa kupokea fedha hizo na kuingizwa
katika akaunti yake binafsi, ni kosa kwa mujibu wa masharti ya maadili
ya viongozi wa umma kwa kuwa viongozi wa umma hawaruhusiwi kuomba fedha
au msaada au kujipatia maslahi ya kiuchumi au kumpatia mtu mwingine
maslahi hayo ya kiuchumi.
Wakili wa Tibaijuka, Dk Rugemeleza Nshara, alidai mbele ya Baraza
mteja wake hakuna kosa alilofanya, bali alitumia wadhifa alionao kama
viongozi wengine akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuomba na
kuchangisha fedha kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na si binafsi.
“Nataka kuuliza Baraza hili, ina maana juzi Waziri Mkuu, alivyoongoza
uchangishaji fedha kwa ajili ya maendeleo alikwenda kinyume na maadili
ya uongozi?,” alihoji. Profesa Tibaijuka, alikiri kuomba fedha hizo kwa
ajili ya kuendeleza taasisi hiyo yenye lengo la kujenga shule za mfano
za wasichana wenyewe vipaji kila kanda ili kukuza na kuimarisha elimu ya
mtoto wa kike nchini.
“Huu si msaada wa kwanza, tumekuwa tukifadhiliwa na Serikali ya
Sweden kupitia msaada tuliopatiwa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa,
ambaye alitambua juhudi zetu na kutuunga mkono, tumechangiwa na taasisi
za ndani na nje na watu binafsi, kiasi kinachohitajika kuboresha shule
hizi ni dola za Marekani milioni 14 sawa na takribani Shilingi bilioni
25.2,” alisema.
Alisema pamoja na Rugemalira aliyetoa Sh bilioni 1.6, pia
mfanyabiashara maarufu nchini, Reginald Mengi alichangia taasisi hiyo Sh
milioni 278, ikiwemo Serikali ya Sweden iliyomaliza mkataba wake
iliyochangia Sh bilioni 8.1.
“Sisi tuliopo kwenye taasisi hii, tunaaminiana na ni waadilifu ndiyo
maana fedha nilizoomba ziliingizwa kweli kwenye akaunti yangu lakini
niliziwasilisha, zilizobaki ni deni nililokuwa naidai taasisi, lakini
pia nimekopa Benki M Sh bilioni mbili kwa ajili ya kuboresha taasisi hii
na kuweka dhamana nyumba yangu iliyopo Oysterbay. Mbona hili
hamlioni?,” alihoji.
Wakati akijitetea, Tibaijuka aliomba akabidhi andiko lake mbele ya
baraza hilo. “Nina andiko langu na naomba nilikabidhi, kabla hujafa
hujaumbika, nasimama hapa leo kwa sababu tayari nimeshahukumiwa bila
kusikilizwa, niliomba hata bungeni nipewe nafasi lakini nilihukumiwa
kama Waziri nikavuliwa madaraka, nashangaa leo nimesimamishwa hapa kama
mbunge,” alisema.
Alisema “mimi mpaka sasa nasema sijakiuka maadili labda wanasheria
wanieleweshe kwa sababu nilisimama kama mimi wakati wa kuomba fedha na
si kama waziri au mbunge, hivyo sasa naona lengo ni kunivunja moyo,
kunidhalilisha, kunifanya kama mwanamke mhuni na tapeli.” Aliendelea
kujitetea, “nimekuja kujieleza ila..
Mimi siyo mwanasheria ila ukweli sina kosa na ndiyo maana nyaraka
zote ambazo zipo hapa, mimi ndo nimewapa, nimekuja hapa kwa nia njema na
naamini kwamba Baraza hili litanisikiliza kwa sababu ukweli ndiyo
mwanzo wa maadili, lazima tupiganie haki na tupiganie ukweli.
“Kama mimi nimefanya kosa kusimama kuwasaidia watoto wenye vipaji ni
kosa, naomba mwanasheria anieleweshe na naomba ukweli usimame maana
tukienda na fitina peke yake, hatutafika. Mimi ni profesa na mchumi na
ni mstaafu wa muda mrefu na nina pensheni, sina makuu, maisha yangu ni
‘simple’ (ya kawaida) huwezi kunikuta Dubai... Ila nipo tunafanya
maendeleo na wananchi wangu,” alisema.
Hata hivyo alisema fedha anazodaiwa kuhamisha baada ya kupokea na
kukatwa za kulipa deni la Benki M, zilizobaki zilikuwa ni halali yake
kwa kuwa alikuwa akidai shule hivyo fedha hizo zilizobaki ni kwa ajili
ya matumizi yake binafsi. “Mimi ni mchakarikaji, mtafuta fedha na
kiongozi anayeshindwa kutafuta fedha kwa ajili ya watu wake hafai.
Hivyo nilipolipwa milioni 117 (Shilingi), nilitoa milioni mbili
nikachangia Kanisa la Makongo na nikatoa laki nne nikapeleka kanisani na
milioni 10 niliitoa kwa ajili ya matumizi yangu ya kununulia mboga, “
alisema. Shahidi wa Profesa Tibaijuka ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya
Wadhamini wa Taasisi hiyo, Balozi Paul Rupia katika ushahidi wake mbele
ya Baraza, alisema fedha hizo zimetafutwa na Profesa Tibaijuka.
Alisema aliitaarifu bodi kwamba zipo fedha zimeingia katika akaunti
yake na zinatakiwa kulipa madeni wanayodaiwa. Alisema katika kikao hicho
cha kutoa uamuzi wa kugawanywa kwa fedha hizo kilichofanyika Luguruni ,
hakuhudhuria, ingawa alikuwa na taarifa zote za kinachoendelea.
Rupia alisema bodi hiyo haikumpa masharti yoyote Profesa Tibaijuka ya
kumaliza kulipa madeni hayo kwa sababu hawakuona sababu ya kumfuatilia
kwa kuwa walimwamini, kutokana na juhudi zake binafsi za kupata fedha
hizo. Shauri hilo lilianza saa 3 na baadaye kuahirishwa kwa muda hadi
saa 6.30 mchana, lilipoanza kusikilizwa tena na kumalizika saa 11.45
jioni.
Katika shauri hilo, Profesa Tibaijuka alitoa ushahidi kwa zaidi ya
saa tatu, akilalamika kuonewa na kuhukumiwa bila kusikilizwa. Shauri
hilo liliahirishwa hadi Machi 13 mwaka huu, kutokana na muda kutotosha.
Wakili aliomba udhuru wa kwenda Marekani kwa siku 10 na Jaji Msumi
alikubali.
Jaji Msumi alisema wajumbe watapitia shauri hilo na siku hiyo itaamuliwa, endapo hukumu itatolewa wazi au kwa uamuzi wa ndani.
-EDDY BLOG
0 comments:
Post a Comment