ACT WAZALENDO CHAZINDUA KAMPENI ZAKE ZA UBUNGE JIMBO LA MANYONI
Baadhi ya wagombea ubunge wa chama cha ACT Wazalendo waliohudhuria mkutano wa uzinduzi katika jimbo la Manyoni-Singida.
Na, Jumbe Ismailly, Manyoni
CHAMA Cha ACT Wazalendo wilaya ya Manyoni Mkoani Singida kimezindua kampeni za ubunge wa jimbo la Manyoni mashariki kwa kumnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo,Muttee John Henry na kuwatisha watendaji wa idara ya afya wanaouza madawa kwenye vituo vya kutolea huduma na hivyo kusababisha wananchi kukosa huduma katika vituo vya kutolea huduma hizo.
Akiwahutubia wananchi wa mji wa Manyoni na vitongoji vyake,mgombea ubunge wa jimbo la Manyoni mashariki kupitia tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo,Henry amesema vituo vingi vya kutolea huduma za afya vimekuwa vikikabiliwa na uhaba mkubwa wa madawa jambo linalowafanya wagonjwa wanaofuta huduma kutakiwa kwenda kununua dawa kwenye maduka ya madawa yaliyopo karibu na vituo hivyo.
Hata hivyo mgombea huyo alifafanua kwamba kutokana na kuwepo kwa tatizo kubwa la upatikanaji wa dawa,ni asilimia sita tu ya watanzania ndiyo wanaonufaika na mfuko wa afya ya jamii (CHF),hali inayoonyesha bado kuna idadi kubwa ya watanzania wanaopoteza maisha kwa kukosa huduma hizo za afya kwenye maeneo ya vijijini.
‘Ndugu zangu nchi hii asilimia sita tu ya wananchi wa Tanzania ndiyo wanaonufaika na mfuko wa afya ya jamii na asilimia 98 ya wakulima,wafugaji,bodaboda,mama lishe na wafanyakazi katika sekta isiyokuwa rasmi hawanufaiki na mfuko wa afya ya jamii(CHF)’’alifafanua Henry.
Kwa mujibu wa Henry,licha ya wananchi hao kupigania kuongeza uchumi kwa nguvu zote kwa kipindi cha miaka 35,wanapofikia umri wa miaka 60 huwa wamechoka na hivyo kujikuta wakisahaulika katika taifa lao walilolitumikia kwa kipindi kirefu katika maisha yao.
Aidha alisisitiza kwamba taifa linalowasahau wananchi waliolitumikia kwa miaka mingi ikilinganishwa na watumishi wa serikali ambao wanapostaafu hulipwa mafao yao ya kustaafu,hilo siyo taifa jema ambalo baba wa taifa alikuwa akijivunia.
Alisisitiza mgombea huyo kijana kwamba ni wakati muafaka sasa wa kuweka utaratibu wa kuwasaidia watanzania wanyonge hao pale wanapochoka.
Ili kukabiliana na hali hiyo ya ukosefu wa madawa kwenye vituo vya kutolea huduma,Henry alisema chama cha ACT Wazalendo kimetafakari sana na kuja na mpango mpya wa kuanzisha mfuko utakaowasaidia watanzania wanyonge.
“Najua fedha zetu tunazokusanya ni chache sana lakini mfuko wa wanyonge ambao utaweza kuhifadhi fedha kidogo kidogo ndiyo kimbilio la wanyonge wanaopata majanga ya kuugua basi wanapona kwa mfuko wa afya ya jamii”alifafanua.
Naye katibu wa Mkoa wa Chama Cha ACT Wazalendo,Lipu Loti Robert alisema idadi kubwa ya watendaji wamebainika kulihofia azimio la Arusha lililoachwa na baba wa taifa marehemu,Mwalimu Julius Nyerere na ndiyo maana waliamua kulivunja kwenye moja ya vikao vilivyofanyika Zanzibar.
Hata hivyo Roberti aliweka wazi kuwa ACT baada ya kubaini kutokuwepo kwa azimio la Arusha ndipo walipozindua azimio la Tabora ambalo lina mambo manne,ambayo ni pamoja na Hifadhi ya jamii,suala la uchumi shirikishi,sekta ya afya na sekta ya elimu.
katibu wa ACT Mkoa wa Singida,Bwana Lipu Loti Robert akifungua mkutano wa uzinduzi wa kampeni kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Manyoni mashariki.
Mmoja wa wakereketwa wa chama hicho akipeperusha bendera kwenye mkutano wa uzinduzi
baadhi ya viongozi wa ACT waliohudhuria mkutano wa uzinduzi kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Manyoni mashariki.Picha zote na Jumbe ismailly
0 comments:
Post a Comment