WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUSHIRIKI ZOEZI LA USAFI DISEMBA 9
Na Shamimu Nyaki-Maelezo
Serikali imewaagiza watumishi wa umma
kushiriki zoezi la usafi wa nchi litakalofanyika tarehe 9 disemba mwaka huu
katika maeneo yao wanaoishi.
Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi
wa Idara ya Habari Bw Assah Mwambene alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari leo jijin Dar es salaam na kusema kwamba Watumishi wa Umma wanatakiwa wabaki nyumbani na kufanya usafi
katika maeneo yao na yale watakayo
pangiwa na viongozi wa mitaa wanayoishi.
“Kila mwananchi ahakikishe eneo lake
ni safi”Alisema Mwambene.
Mkurugenzi ameongeza kuwa Watumishi
wa Umma hawataenda kazini badala yake
watabaki nyumbani na kufanya
usafi kwa kushirikiana na wananchi kusafisha maeneo yanayozunguka mitaa
wanayoishi ikiwemo hospitali,kuzibua mitaro iliyoziba pamoja na kuzoa taka
zilizolundikana sehemu ambazo sio rasmi.
Ameongeza kuwa muongozo kuhusu namna
zoezi la usafi litakavyotekelezwa umeshatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI
kwa Uongozi wa Mikoa hadi Mitaa na
kilichobaki ni utekelezaji tuu wa agizo hilo kwa kila mwananchi sehemu
anayoishi,anayofanyia shughuli nyingine za kila siku kuhakikisha anafanya
usafi.
Aidha Mkurugenzi amewataka viongozi
wa kila eneo kutengeneza utaratibu mzuri ambao utafanikisha zoezi la usafi kufanikiwa kwa kuhakikisha wanasimamia kwa
ukamilifu na kuwahimiza wananchi kuwa na tabia ya kusafisha maeneo wanaoishi
kwa kuwa ni wajibu wao kufanya hivyo.
Hata hivyo tarehe tisa disemba kila
mwaka huwa ni siku ya kusherehekea Uhuru wa Tanganyika uliopatikana miaka
hamsini na nne iliyopita lakini kwa mwaka huu itaadhimishwa kwa kufanya usafi
nchi nzima.
0 comments:
Post a Comment