Tuesday 5 December 2023

ZIFAHAMU HATUA TANO ZA KUKUJENGEA UJASIRI KATIKA TAALUMA YAKO




Je wewe hujiamini na elimu au taaluma yako? Ukiweza kujua kitu gani kinahitajika kwenye eneo fulani unaweza kusimama na kwenda juu zaidi ya woga ulionao.
Mambo yanabadilika pale ambapo tunaacha kuangalia tunahitaji nini au taaluma gani na badala yake tujue kinahitajika kitu gani na sisi tufanyaje? Maisha hubadilika na mambo huanza kwenda kwa mtazamo mwingine.
Hii ni kweli pale unapojifunza kwa uchungu mkubwa mara tu unapoingia kwenye ajira au taaluma mpya. Mara nyingi tunataka kupendwa au tunakubalika na watu, ni sawa lakini kitu cha muhimu ni kusimamia taaluma yako vizuri zaidi ili mambo yakuendee vyema.
Haijalishi hujui kwa kiasi gani linapokuja suala la taaluma kwenye eneo la kazi au biashara inategemea sana na mawazo yako umeyajenga wapi. Kama ni jasiri mambo yatakwenda vizuri na kama ni mwoga utaboronga tu. Taaluma kwa kifupi ni kiwango cha huduma unayotoa si idadi ya vyeti ulivyonavyo. Ukiweza kudhibitisha hilo watu watakuamini na watakuthamini kwa wewe kujiamini mwenyewe kwanza na usijidanganye kwa vile ambavyo hujui fanya juhudi ya kuvijua vitu hivyo mapema iwezekanavyo.
Kama mawazo yako yanatokana na ubunifu wa kile unachokiamini inawezekana ukawa sahihi katika huduma au kazi unayofanya.
Mbinu hizi chache zitakusaidia kuongeza ujasiri wako katika zile mbinu nyingine ambazo uko nazo au utaendelea kujifunza mbele ya safari yako kitaaluma.
1 – Sikiliza kile kinachohitajika – Je kwenye jambo lililo mbele yako kinahitajika nini? kinachokosekana ni nini?  Namna gani ya kuingia kwenye jambo hilo? Sikiliza na usiogope kuuliza maswali kabla ya kurukia jambo.
2 – Wakati wote jaribu kujibu au kufanya jambo kwa uwezo wako wa hali ya juu sana. Jambo linapotokea kwenye kazi au biashara watu wengi hukurupuka na kufanya maamuzi ya haraka au kukwaruzana na watu wengi na hata kutoa lugha chafu au zisizopendeza na kukasirisha wengine. Jitahidi kuwa mtulivu, na ujibu mada kitaaluma hata kama umechefuka kiasi gani, wewe utaonekana jasiri na mwenye mwelekeo mkubwa kitaaluma kuliko wengine.
3 –  Kama huna uhakika uliza swali, usijiweke chini au kujidharau na wala usipende kusema samahani kwa kitu ambacho si kosa. Uliza swali kama huna uhakika na hicho kinachoongelewa au kama hujui kumetokea nini. Usijiweke kwenye mazingira ya kudharaulika au watu kukupanda kichwani, maisha ya kitaaluma yatakuwa magumu kwako.
4 –  Tatua kwanza tatizo halafu kukasirika baadaye. Kuwa mtaaluma si jambo jepesi, jambo linapotokea uwe mtulivu na shughulika nalo halafu vitu vingine utahusika navyo baadaye baada ya utatuzi wa jambo. Ukikasirika sana hakikisha uko sehemu ambayo haina watu wengi, kwa usalama wa watu wengine na usalama wako pia. Usiruhusu msongo wa mawazo ukakuua, nenda nje ya tukio au chooni ili kurudisha akili yako kwenye mstari.
5 – Usitengeneze urafiki kwa kusengenya watu – Usijaribu kutengeneza kundi lako kutokana na uwezo wako wa kuzungumzia watu wengine. Hii itakufanya uwe na marafiki wasio sahihi. Utakuwa na watu wengi wanaokufuata kila mtu anatafuta maslahi yake kwako na si urafiki wa kweli.
Ukiwa msengenyaji ni vigumu sana kupata nafasi ya kukupeleka juu na hata ukienda juu ni ngumu kuwa na watu wanaopenda kufanya kazi na wewe. Kwa namna nyingine usitumie nafasi uliyonayo kudhuru watu wengine kitaaluma, unaweza kufurahia kabla hujagundulika ila kuna siku watu watakuchoka na wakishakuchoka wanakuwa tayari kwa jambo lolote lile.
Ujasiri wa kupambana na matatizo na si watu wengine, itakupa nafasi ya kutofautisha hisia na tatizo la kutafutiwa ufumbuzi. Ujasiri wakati mwingine unaweza kutikiswa, ingawa imani yako ya ndani haitokani na kile unakifanya bali unajiamini vipi kufanya kitu sahihi haijalishi mazingira yamekusonga kwa kiasi gani. Hiyo itakutengenezea viwango vyako vya kipekee katika taaluma yako, hutahitaji watu wakutetee bali msimamo wako na ujasiri utawavuta watu na wapende kufanya kazi pamoja na wewe.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA