Showing posts with label mikopo. Show all posts
Showing posts with label mikopo. Show all posts

Sunday, 12 February 2017

Monday, 14 November 2016

BODI YA MIKOPO YATOA SIKU 30 KWA WADAIWA SUGU


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo Abdul-Razaq Badru amesema kuwa hadi sasa kuna jumla ya wadaiwa sugu 142,470 wenye mikopo ya shilingi 239,353,750,170.27 iliyokwishaiva hawajajitokeza wala kuanza kulipa mikopo yao.

Akitolea ufafanuzi wa maana ya neo "Wadaiwa Sugu", Badru amesema kuwa ni wanufaika waliokopeshwa, muda wa matarajio ukapita bila kuwasilisha taarifa zao na kulipa madeni ya mikopo waliyokopeshwa tangu mwaka wa masomo 1994/1995.

Kuhusu hatua zinazochukuliwa na bodi hiyo, Badru amesema mbali na kutoa siku 30, bodi hiyo inakamilisha taratibu za kuwafikisha mahakamani kwa kuvunja sheria ya bodi ya mikopo kifungu cha 19A(1).

Hatua nyingine ni pamoja na kuyawasilisha majina hayo katika taasisi za mikopo, kuwasiliana na wadhamini wao pamoja na kuyatangaza hadharani majina ya wadaiwa sugu wote ili waajiri, wadhamini na wadau wengine wayajue na kutoa taarifa katika bodi hiyo.

Kuhusu takwimu za mikopo iliyotolewa, amesema tangu 1994/95 hadi 2015/16 jumla ya shilingi 2,595,932,575.56 zimekopeshwa kwa jumla ya wanufaika 379,179.

Amesema kati ya mikopo yote iliyokopeshwa, mikopo iliyoiva ni shilingi 1,425,708,285,046.48 kwa wanufaika 238,430 ambao tayari wamemaliza kipindi chao cha matazamio.

Badru amesema kuwa jumla ya wanufaika wa mikopo 93,500 wamebainika na kupelekewa ankara za madeni yao, ambapo kati yao wanufaika 81,055 wanaendelea kulipa.

Monday, 31 October 2016

BODI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU YATOA SIKU 90 KWA WALIOKOSA MIKOPO KUKATA RUFAA


Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza siku 90 kuanzia leo (Jumatatu, Oktoba 31, 2016) kwa waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2016/2017 kukata rufaa kwa njia ya mtandao ikiwa hawajaridhsihwa na matokeo ya upangaji uliotangazwa hivi karibuni.

Serikali imetenga Tshs 483 bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo kwa jumla wanafunzi 119,012 – kati yao, wanafunzi 93,295 ni wanaondelea na masomo na wanafunzi 25,717 ni wa mwaka wa kwanza. Hadi sasa, jumla ya wanafunzi 20,183 wa mwaka wa kwanza wameshapata mikopo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo (Jumatatu, Oktoba 31, 2016) na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru, Bodi imeanza kupokea rufaa hizo kwa njia ya mtandao (Online Loan Application and Management System) kuanzia leo (Oktoba 31, 2016) hadi Januari 31, 2017.

“Wanachotakiwa kufanya wanafunzi ni kuingia katika mtandao wetu wahttp://olas.heslb.go.tz na kujaza fomu, kuichapa na kuiwasilisha kwa Afisa Mikopo wa chuo chake ambaye atawasilisha kwetu fomu zote za chuo chake kwa barua kwa ajili ya sisi kuzifanyia kazi,” amesema Bw. Badru.

ANGALIZO: Ada ya Maombi ya Tshs 10,000/- iliyopaswa kulipwa na waombaji mikopo kwa MPesa kwa ajili ya malipo ya Rufaa (HESLB) imefutwa.Taratibu nyingine zinabaki palepale.

Wednesday, 26 October 2016

ASILIMIA 90 YA WANAFUNZI KUPATA FEDHA ZAO ZA MIKOPO KESHO

Wakati baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu wakiendelea kusubiri kupata mikopo yao, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia kesho, asilimia 90 ya wanufaika watakuwa wameshapata fedha zao. 

Majaliwa alisema hayo jana wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). 

“Taarifa niliyonayo ambayo nimepata asubuhi hii (jana), wachache sana wameanza kulipwa jana (juzi), lakini ulipaji utaendelea mpaka keshokutwa (kesho), tunatarajia kufikia asilimia 90 ya wanaostahili kulipwa watakuwa wameshalipwa,” alisema. 

Majaliwa ambaye ni mhitimu wa UDSM, aliwataka waombaji wa mikopo washirikiane na Wizara ya Elimu kwa kutoa taarifa sahihi ili kurahisisha ulipaji.

“Serikali haitavumilia tena ucheleweshwaji wa makusudi  wa malipo ya fedha za mikopo ya chuo. Kama kuna tatizo, taarifa zitolewe haraka ili kuzuia migogoro kati ya wanafunzi na Serikali yao,” alisema.

Alisema upungufu wa wahadhiri waandamizi umesababishwa na masharti ya ajira za mkataba, unaowataka kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70.

“Hii inaathiri hali ya utoaji wa taaluma kwa fani za ‘Post-Graduates’. Serikali itaendelea kuweka kipaumbele cha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo,” alisema Majaliwa. 

Alisema licha ya juhudi hizo za Serikali, vyuo pia vinatakiwa kuwa na utaratibu wa kurithishana kazi ili kusiwe na pengo katika utoaji wa taaluma pale baadhi ya wahadhiri wanapostaafu.

Majaliwa ambaye pia alizindua kitabu kilichopewa jina la ‘From Lumumba Street to The Upper Hill and Beyond’, alisema Serikali itatoa ushirikiano katika utekelezaji wa mipango ya chuo hicho. 

Akizungumzia kuhusu masilahi  ya watumishi wa vyuo vikuu, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi wote wa umma na sasa inakamilisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi ili kubaini watumishi hewa.

 “Serikali inaendelea na maboresho na kuimarisha masilahi kwa watumishi wote wa umma kupitia bodi ya mishahara na mara tutakapokamilisha, tutapanga upya mishahara na motisha kwa watumishi,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Dk Leonard Akwilapo alisema wizara hiyo imetenga Sh9 bilioni kwa ajili ya kufanya ukarabati wa miundombinu kwenye chuo hicho zikiwamo maabara. 

Awali, katika hotuba yake, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala aliishukuru Serikali kwa kuanza kufanyia kazi baadhi ya changamoto zanazokikabili chuo hicho ikiwamo upungufu wa hosteli za wanafunzi.

Sunday, 16 October 2016

BODI YA MIKOPO YAPITISHA MAJINA 7904 YA WANAFUNZI WALIOPATA MKOPO KATIKA AWAMU YA KWANZA

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza awamu ya kwanza ya majina ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini watakaopewa mkopo kugharimia masomo yao.
 
Idadi ya wanafunzi ambao tayari wamepitishwa kupata mkopo ni 7,904, hata hiyo imeelezwa kiwango hicho kitaendelea kubadilika kwa kuwa mchakato unaendelea.

Taarifa iliyotolewa jana na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Stella Manyanya ilibainisha kuwa bodi imekamilisha uchambuzi wa majina ya waombaji ambao wana sifa zinazotakiwa na majina ya wanufaika wapya ambayo yameanza kutangazwa kupitia tovuti ya bodi hiyo.

 “Kwa kuzingatia mpango mkakati, pia mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka 2016/17, Serikali imetoa vigezo vitakavyozingatiwa katika utoaji mikopo,” alisema Manyanya.

Alitaja vigezo vilivyotumika kuwa ni pamoja na vipaumbele vya kitaifa vinayoendana na mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na mafunzo ambayo yatazalisha wataalamu wanaokidhi mahitaji ya kitaifa katika fani za kipaumbele.

Manyanya alizitaja fani zilizopewa vipaumbele kuwa ni sayansi za tiba na afya, ualimu wa sayansi na hisabati, uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo, mafuta na gesi asilia, sayansi asilia na mabadiliko ya tabianchi, sayansi za ardhi, usanifu majengo na miundombinu.

Katika taarifa yake, Manyanya alisema pia mchakato wa kuwapata wenye sifa za kukopa uliangalia uhitaji wa waombaji, hususan wenye mahitaji maalumu kama walemavu na yatima, ufaulu wa waombaji katika maeneo ya vipaumbele na umahiri.

“Kuanzia mwaka huu wa masomo, wanufaika wote wa mikopo (wapya na wanaoendelea na masomo) watakopeshwa kulingana na uwezo wao katika vipengele vyote vya mikopo,” alisema.

Akizungumzia mchakato huo, mkurugenzi mtendaji wa bodi hiyo, Abdul Badru alisema unaendelea kufanywa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na timu ya bodi imejigawa katika vikundi ili kuhakikisha mipango inakwenda jinsi inavyotakiwa.

 “Timu ipo kazini na inafanya kazi yake kwa umakini. Kwa sasa majina ya waliochaguliwa kutokana na vigezo yamewekwa, lakini ni wahusika wenyewe au walezi na wazazi ndiyo wanaweza kuyaona kupitia namba zao za usajili wa kidato cha nne. Lakini siku chache zijazo tunaweza kuwataja wakaonekana kwa kila anayehitaji kuyaona,” alisema Badru.

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA