Wednesday, 26 October 2016

ASILIMIA 90 YA WANAFUNZI KUPATA FEDHA ZAO ZA MIKOPO KESHO

Wakati baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu wakiendelea kusubiri kupata mikopo yao, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia kesho, asilimia 90 ya wanufaika watakuwa wameshapata fedha zao. 

Majaliwa alisema hayo jana wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). 

“Taarifa niliyonayo ambayo nimepata asubuhi hii (jana), wachache sana wameanza kulipwa jana (juzi), lakini ulipaji utaendelea mpaka keshokutwa (kesho), tunatarajia kufikia asilimia 90 ya wanaostahili kulipwa watakuwa wameshalipwa,” alisema. 

Majaliwa ambaye ni mhitimu wa UDSM, aliwataka waombaji wa mikopo washirikiane na Wizara ya Elimu kwa kutoa taarifa sahihi ili kurahisisha ulipaji.

“Serikali haitavumilia tena ucheleweshwaji wa makusudi  wa malipo ya fedha za mikopo ya chuo. Kama kuna tatizo, taarifa zitolewe haraka ili kuzuia migogoro kati ya wanafunzi na Serikali yao,” alisema.

Alisema upungufu wa wahadhiri waandamizi umesababishwa na masharti ya ajira za mkataba, unaowataka kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70.

“Hii inaathiri hali ya utoaji wa taaluma kwa fani za ‘Post-Graduates’. Serikali itaendelea kuweka kipaumbele cha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo,” alisema Majaliwa. 

Alisema licha ya juhudi hizo za Serikali, vyuo pia vinatakiwa kuwa na utaratibu wa kurithishana kazi ili kusiwe na pengo katika utoaji wa taaluma pale baadhi ya wahadhiri wanapostaafu.

Majaliwa ambaye pia alizindua kitabu kilichopewa jina la ‘From Lumumba Street to The Upper Hill and Beyond’, alisema Serikali itatoa ushirikiano katika utekelezaji wa mipango ya chuo hicho. 

Akizungumzia kuhusu masilahi  ya watumishi wa vyuo vikuu, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi wote wa umma na sasa inakamilisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi ili kubaini watumishi hewa.

 “Serikali inaendelea na maboresho na kuimarisha masilahi kwa watumishi wote wa umma kupitia bodi ya mishahara na mara tutakapokamilisha, tutapanga upya mishahara na motisha kwa watumishi,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Dk Leonard Akwilapo alisema wizara hiyo imetenga Sh9 bilioni kwa ajili ya kufanya ukarabati wa miundombinu kwenye chuo hicho zikiwamo maabara. 

Awali, katika hotuba yake, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala aliishukuru Serikali kwa kuanza kufanyia kazi baadhi ya changamoto zanazokikabili chuo hicho ikiwamo upungufu wa hosteli za wanafunzi.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA