Monday, 10 November 2014

YAMETIMIA,OKWI AFUTA MKOSI SIMBA SC, AFUNGA BAO PEKEE TAIFA


Okwi (katikati) akipongezwa na Ramadhani Singano 'Messi' kulia na Elias Maguri kushoto baada ya kufunga
(CHANZO:  Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM)
BAO pekee la Mganda, Emmanuel Okwi limeipa Simba SC ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuilaza Ruvu Shooting 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Okwi alifunga bao dakika ya 78 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Abdallah Rashid kufuatoa shuti la mshambuliaji Elias Maguri aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Said Ndemla.
Baada ya kufunga bao hilo, Okwi alikwenda kushangilia mbele ya mashabiki wa Yanga SC ambao walikuwa wakimzomea muda wote wa mchezo na kwa hasira mashabiki hao wakamtupia chupa za maji.


Ushidi huo, unaifanya Simba SC ifikishe pointi tisa baada ya kucheza mechi saba na kutoka sare sita katika mechi zake zote za awali.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Isihaka Shirikisho wa Tanga, Simba SC ndiyo waliotawala mchezo na kutengeneza nafasi nyingi zaidi ambazo walishindwa kuzitumia.
Ruvu nayo ilicheza vizuri na kusukuma mashambulizi langoni mwa Simba SC, lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Wekudu wa Msimbazi chini ya kipa mzoefu, Ivo Mapunda uliwanyima mabao.
Mshambuliaji wa Simba SC, Amisi Tambwe kulia akimtoka beki wa Ruvu, Yussuf Nguya
Kipindi cha pili, timu zote ziliongeza kasi ya mashambulizi kusaka mabao, lakini haikuwa bahati yao Ruvu inayofundishwa na Mkenya Thom Olaba, baada ya kupoteza mchezo huo.
Ushindi huo kwa Simba SC pia unarejesha amani kwa kocha Mzambia, Patrick Phiri ambaye uongozi wa klabu hiyo ulitishia kumfuta kazi iwapo hatapata ushindi katika mechi mbili, ikiwemo ya leo. 
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, William Lucian ‘Gallas’, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’, Awadh Juma/Seseme dk90, Amisi Tambwe, Said Ndemla/Maguri dk67 na Emmanuel Okwi.
Ruvu Shooting; Abdallah Rashid, Said Madega, Yussuf Nguya, Frank Msese, Salvatiry Ntebe, Zuberi Dabi, Raphael Keyala/Seif Abdallah dk63, Juma Nade, Mathayo Wilson, Juma Mdindi/Juma Seif dk48  na Abdulrahman Mussa.

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA