RAIS FILIPE NYUSI WA MSUMBIJI KULIHUTUBIA BUNGE LA TANZANIA
Na.Aron Msigwa
Rais wa Msumbiji Mhe.Filipe Jacinto Nyusi anatarajia kuwasili nchini Tanzania Mei 17 mwaka huu kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine anatarajia kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma.
Akitoa taarifa ya ziara hiyo leo jijini Dar es salaam Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecki Sadiki amesema kuwa Rais Filipe Nyusi atawasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es slaam, Mei 17,2015 majira ya saa 6.
Amesema mara baada ya kuwasili uwanjani hapo, Rais huyo atalakiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, kupata mapokezi ya burudani ya ngoma za asili na kukagua gwaride la heshima litakaloandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzanian(JWTZ) na baadaye kupigiwa mizinga 21.
Mhe.Sadiki amesema kuwa mara baada ya shughuli ya mapokezi ya Rais huyo uwanja wa ndege ataelekea Ikulu ambako atapokewa rasmi na mwenyeji wake,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Jakaya Kikwete na baadaye viongozi hao wawili watakua na mazungumzo ya faragha.
Amesema Mei 18, 2015 Rais Filipe Nyusi atafanya mazungumzo na wafanyabiashara wa Msumbiji waishio nchini Tanzania na kisha kuendelea na ziara yake Visiwani Zanzibar ambako atakutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein.
Ameeleza kuwa baada ya kukamilisha ziara yake kisiwani Zanzibar Mei, 19 mwaka huu, Rais Filipe Nyusi ataelekea mjini Dodoma ambako atakutana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi,Rais Jakaya Mrisho Kikwete yalipo Makao Makuu ya Chama cha hicho na baadaye ataelekea Ukumbi wa Bunge kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema ,Mhe.Filipe Nyusi atahitimisha ziara yake na kurejea nchini kwake Mei 19,2015 na kuwaomba wananchi hususan wakazi wa jiji la Dar es salaam kuwa wavumilivu kutokana na usumbufu utakaotokana na baadhi ya barabara zikiwemo Nyerere, mzunguko wa Kamata, Barabara ya Sokoine ,Luthuli na Barabara ya Kilwa kufungwa mara kwa mara kupisha msafara wa kiongozi huyo.
-MJENGWA
0 comments:
Post a Comment