WANAFUNZI WANNE KAMPALA UNIVERSITY KIZIMBANI KWA KUMKASHIFU RAIS
Wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu cha Kampala Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, wakikabiliwa na shitaka la kuchapisha picha zinazoonyesha Rais Dk. John Magufuli amevaa hijabu kama mwanamke wa Kislamu na kuzisambaza kwenye mtandao wa WhatsApp.
Shtaka jingine ni kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao ya amii (WhatsApp) kwa lengo la kumuudhi Rais.
Washitakiwa hao ni Amenitha Kongo (19), Maria Tweve (20), Agnes Gabriel (21) na Anne Mwansasu(21).
Walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Catherine Kiyoja.
Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Florida Wenceslaus, alidai washitakiwa walitenda kosa hilo Juni 9, mwaka jana Dar es Salaam.
Florida alidai washitakiwa kwa pamoja walitengeneza picha hizo kwa kutumia kompyuta na baadaye kuisambaza kwenye WhatsApp kwa lengo la kumuudhi Rais.
Washitakiwa walikana shitaka hilo na kurudishwa rumande kutokana na kutotimiza masharti ya dhamana. Kesi itatajwa tena Machi 13, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment