Thursday 15 December 2022

VITU VYA KUEPUKA KATIKA MITANDAO UNAPOFANYA BIASHARA


Na Phenty Kiria

Mpendwa msomaji wangu, karibu katika mfululizo wa makala zetu. Leo nakuletea  elimu ya nini uepuke unapokuwa unafanya biashara yako mtandaoni. Bila ya shaka hakuna aliyeanzisha na anayefanya biashara anatamani apate faida na pia ikue. Baadhi ya wafanyabishara mitandaoni wamekuwa wakilalamika kuwa biashara zao hazikui japokuwa wana sponsor page zao, wanalipa waraghabishi kutangaza biashara zao. Zipo sababu nyingi lakini hizi ni baadhi ya sababu zinazopelekea kutokukua na kudumaa kwa biashara mitandaoni tafadhali ziepuke;

 

  KUTOWEKA BEI YA BIDHAA

Wafanyabiashara wengi sasa hivi hawataki/ hawapendi kuweka bei ya bidhaa kwa sababu wanataka kuuza bei tofauti kutokana na mtu atakae mtafuta. Mfano mtu yeyote maarufu akimuulizia bei atamtajia bei kubwa akiamini ana pesa, au mtu ambae hamjui atamuuzia bei ya kawaida. Lakini pia watu wengi hawapendi kumfuata mtu DM wengine wanaona uvivu, wengine wanajua dalali au tapeli. Kuweka bei ya bidhaa inafaida nyingi

1. Kuongeza uaminifu kwa wateja

2. Kukuza biashara yako

3. Kuongeza wafuasi katika ukurasa wako wa biashara

 ( ambao ndio wateja wenyewe)

4. Husaidia katika utafutaji masoko ( marketing ); kuna muda utahitaji kufanya sales sasa ni muhimu mteja kujua bei imetoka wapi na imeshuka kwa kiasi gani

5. Kupunguza usumbufu wa kuulizwa bei kila mara.

 

KUFUNGA SEHEMU YA UJUMBE (DM)  

Mitandaoni kuna baadhi ya watu ni wasumbufu sana ndio maana watu wengi hawapendi kuacha sehemu zao za ujumbe wazi lakini wewe kama mfanyabiashara unaetaka kukuza biashara yako unahitaji kuacha sehemu yako ya ujumbe wazi ili mteja aweze kuwa uhuru kuuliza kitu chochote. Lakini wafanyabiahara wengi wamekuwa na tabia ya kufunga sehemu zao za ujumbe, wengi wakiandika kabisa “usije sehemu za ujumbe piga simu” hii ni mbaya kwa sababu unapoteza wateja wengi sana bila kujua, na sio kila mtu anapenda kuongea na simu.

Kama mfanyabiashra na hupendi shida zinazotokana na sehemu za ujumbe nakushauri mtafute mtu atakaekuwa ana manage ukurasa wako hata kama kwa kumlipa au kutomlipa ili aweze kujibu jumbe za watu lakini pia kujibu kwa wakati.

 


KUWEKA UKURASA WAKO PRIVATE

Wafanyabiashara wengi hawana elimu juu ya biashara za mtandaoni wengi wamenza biashara hii bila kujua nini wanatakiwa kufanya na nini hawatakiwi kufanya, watu wengi (Instagram na twitter) wameweka kurasa zao private lakini pia baadhi ya wafanyabiashara  wameweka kurasa zao private. 

Kuweka ukurasa wako private wewe kama mfanyabiashara inakupotezea fursa nyingi sana bila wewe kujua maana wateja wako watakuwa ni wale wale wa kila siku waliopo mpaka pale utakapoamua wewe kuongeza. Lakini pia kuna watu wengine watapenda kuongea na wewe jinsi ya kukusapoti na wakashindwa kutokana na kuwa private.

    



KUWEKA UJUMBE KUFUTIKA BAADA YA MUDA (DISAPPEARING MESSAGE)

Mtandao wa WhatsApp umeleta madaliko mtu anaweza kuweka jumbe zake kupotea kila baada muda fulani. Hii kwa mfanyabishara sio nzuri maana unapoteza taarifa muhimu za mteja wako, mfano mtu alikuuliza bei ya bidhaa zako lakini hakununua ila baada ya wiki akarudi nakusema anataka ile bidhaa, na ujumbe wake ushapote, hivyo itakupasa kuanza kuulizia upya ni nini anataka wateja wengine hawapendi na wanaweza wasijibu na hivyo wasinunue pia.

 

 

   EPUKA KUWEKA MAELEZO MAREFU / KUTOWEKA KABISA

(CAPTION)

Kuna baadhi ya wafanyabiashara wanapenda kuandika vitu vingi sana wanapotangaza biashara zao lakini pia wapo wasioandika kabisa, wote hawa wanafanya vitu tofauti lakini wote wanapoteza wateja. Sio kila mtu anapenda kusoma hivvo akiona maneno mengi anapita tuu, huyu asie andika kabisa mtu hawezi elewa bei au anapatikana wapi nk. Andika kwa ufupi ili uweke urahisi wateja zako kusoma, mfano

         “Dawa ya kuzuia meno kuuma na kuoza

           Bei; ………..

           Piga/ WhatsApp: ……..”

Hakikisha tangazo lako linaelezea faida ya bidhaa yako yaani kwa nini mteja anunue bidhaa yako? Bila kuelezea faida ya bidhaa yako mteja hawezi jua kwa nini anunue kitu chako asinunue kwa mtu mwingine.

 

LUGHA

Ni vizuri ukajua soko lako ni lipi, ukishajua soko lako ni lipi unaweza jua ni lugha ipi utumie mara nyingi. Mfano ukijua soko lako lipo Uganda, Kenya na Zambia kuliko Tanzania basi ni vizuri ukatumia kingereza mara kwa mara lakini kama soko lako unaona lipo Tanzania ni vizuri Kiswahili mara nyingi ili kupata wateja sio kwamba usitumie kingereza kabisa, hapana

   Ki bongo bongo watu wakiona kingereza kingi katika matangazo yako wanajua bei ni kubwa hata hawaangalii tena bei wanapita tuu. Hivyo fanya tafiti  jua wateja wako wanaokuja mara kwa mara kununua au kuulizia bei wanatumia lugha gani, hii ni njia moja wapo ya kuweza kujua soko lako lipoje.

  

USIFUTE MAZUNGUMZO YAKO NA MTEJA.

Tunashauri kutofuta mazungumzo yako na mteja hata kama amenunua tayari bidhaa yako, kwa nini? Sio kila mtu atapenda kazi yako mtu anaweza sema amelipia bidhaa yako na hajapokea na uthibitisho wa kutuma pesa akatuma mtandoni hii moja kwa moja utaitwa tapeli na madhara yake ni makubwa maana utapoteza wateja wote hata wa zamani ambao walishanunua kwako. 

Lakini kama ama una mazungumzo yote mliofanya unaweza weka picha zake (screenshort) na kila mmoja akaona kwamba ni kweli alipokea mzigo wake, ni muhimu kumuuliza mteja kama kapokea mzigo wake, pia  kumwambia karibu tena sio akaribie tu tena siku nyingine lakini ni ishara kwamba mzigo umemfikia. Naomba kuwakumbusha kuwa  kujenga brand ni kazi ngumu sana lakini kuibomoa ni rahisi sana.

 

Vipo vitu vingi visohitajika katika biashara za mitandaoni lakini hizi za leo ni vitu vikubwa vya kutofanya. Teknolojia inakuja na faida zake lakini pia na changamoto zake ni vizuri tukatumia mitandao kama njia ya kutuongezea vipato au njia ya kukuza akili zetu.              


Ni Imani yangu kuwa mwaka 2023 utaenda kupiga hatua kubwa katika namna ya uendeshaji wa biashara yako mtandaoni..... NAKUTAKIA HERI YA MWAKA MPYA

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA