Showing posts with label jamii. Show all posts
Showing posts with label jamii. Show all posts

Wednesday, 19 January 2022

WATOTO 14 WAISHIO MAZINGIRA HATARISHI MTAANI WAKUBALI KWENDA MAKAO YA WATOTO

 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, akiongea na Watoto waishio katika Mazingira hatarishi jijini Dodoma hawapo picha

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee, Wanawake na Makundi Maalum,Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, akiongea na Watoto waishio katika Mazingira hatarishi jijini Dodoma hawapo picha

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dk.Zainab Chaula,akiongea na Watoto waishio katika Mazingira hatarishi jijini Dodoma hawapo picha

 Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Gasper Muya wakati wa kikao hicho akizungumza na kutoa Msimamo wa Ofisi hiyo katika kushughulikia tatizo la Watoto waishio Mazingira hatarishi

Na WMJJM-DODOMA

Watoto waishio katika mazingira magumu kwenye Jiji la Dodoma wamemueleza Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, (Mb), madhila wanayokumbana nayo katika mitaa wanayoishi huku wakiiomba Serikali iweze kuwanusuru na maisha hayo kwa kuwa siyo kusudi lao kuishi hivyo.

Hayo yamejiri jana Januari, 17, 2022 Waziri huyo alipoongoza jopo la wataalamu wa Wizara hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwenda mitaani wanakoishi watoto hao kwa ajili ya kuzungumza nao na kujifunza toka kwao jinsi gani Serikali inaweza kuwabadilishia maisha yao yawe na ustawi zaidi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti watoto hao walioweza kufikiwa, walisimulia madhila na changamoto wanazopitia wakiwa katika mitaa mbalimbali ya Jiji la DODOMA.

“Mhe. Waziri, sisi watoto tuishio katika mazingira ya mitaani tunapitia madhila mengi sana, tunalazimika kutumia vilevi, kujifunza mambo mengi mabaya pia tunafanyiwa mambo mabaya na tunalazimika kuwa watu wasio wema ili tuishi na matokeo yake tunabaguliwa na kutengwa na jamii” alisema mmoja wa watoto ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kimaadili.

Vilevile, mtoto huyo, alisema wapo baadhi yao wamekuwa wakipitia ukatili wa kupigwa na wenzao wanaowazidi umri, wapo wanaofanyiwa ukatili wa kingono na kuambukizwa magonjwa na kupata maradhi ambayo mwisho wa siku yameondoa uhai kwenye umri mdogo.

Waziri Dkt Gwajima, akizungumza na Watoto hao, aliwaambia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuboresha ustawi wa watoto na ameunda Wizara mpya ambayo pamoja na mambo mengine itasimamia maendeleo na ustawi wa makundi maalumu ikiwemo watoto kwa ujumla wake.

Hivyo, ziara hiyo ya kujifunza huu ni mwanzo wa safari ya kuwaondoa watoto wanaoishi mitaani, wakaishi maisha salama na yenye ustawi hivyo wananchi na watendaji toeni ushirikiano kwani ufumbuzi wa jambo hili utatokana na wanajamii wenyewe.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula, alisema tayari ameanza kuratibu ushirikiano na makatibu wakuu wa Wizara zingine ili watoe ushirikiano kwenye operesheni hii kubwa ya kuwarejesha watoto wa mitaani kwenye maisha yenye ustawi na atasimamia jambo hili kwa ushirikiano na wadau wengine wote.

Kwa upande wake Kaspar Kaspar Muya, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu amesema, ofisi hiyo iko tayari kuratibu ushirikishwaji wa wizara na Sekta zote ili jambo hili lifanikiwe kama ilivyokusudiwa kwenye Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA, 2017/18-2021/22) na ILANI ya Uchaguzi Mkuu CCM, 2020-2025.

Kama sehemu ya mpango wa haraka, Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu imeanza kuratibu kuwezesha watoto waishio kwenye mazingira magumu ya mitaani wanarejea kwenye maisha yenye ustawi ili wakiwa watu wazima waweze kuchangia maendeleo ya taifa kwa tija.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Fatma Mganga akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo amesema, Mkoa upo tayari kushirikiana na wadau wote kusimamia utekelezaji wa zoezi hilo kwa ufanisi.

Ziara hiyo imefanikisha kuwarejesha watoto 14 kwenye makao ya watoto na uratibu unaendelea mkoani Dodoma na utaendelea mikoa yote.

 

Monday, 2 April 2018

WANAMABADILIKO WASAIDIA KUPUNGUZA UKATILI WA KIJINSIA WILAYANI TARIME

"Shemeji zangu walikuwa sita walinipiga sana kwa kweli kwa sababu ya kutaka kumiliki Mali za Mume wangu ambaye ni Marehemu" , ni mmoja ya wanawake wa Tarime akisimlia  kwa masikitiko kutokana na ukatili alioupata baada ya kufiwa na mumewe, ambapo ndugu wa mume alilazimisha kumrithi yeye na mali za mumewe. Mila kama hizi zinazomkandamiza mwanamke zinapaswa kusitishwa 
"Tumekubali kabisa watoto wetu wa kike wasiendelee kukeketwa ,lakini bado jamii zetu hazituelewi tunaendelea kuwaelimisha ili nao wabadilike."- Mzee wa Kimila (Aliyesimama). Bado kuna kazi kubwa ya kumaliza swala la ukeketaji lakini kupitia elimu mbalimbali na mafunzo yanayotelewa kuhusu maswala ya ukeketaji juu ya hasara na madhara yake inaendelea kupunguza idadi ya wanaokeketwa.
"Kwa Tarime mwanamke kupigwa na kuvuliwa nguo hadhalani ilikuwa ni kitendo cha kawaida tu" - Sara Boniface (aliyesimama) , alielezea kwa kina kuhusu ukatili wa kupigwa ambapo aliongeza kwamba kwa sasa ukatili huo umepungua kutokana na elimu wanayoipata wanajamii juu ya ukatili wa kijinsia.
Mmoja wa wazee wa Kimira kutoka Tarime(aliyesimama) akieleza juu ya ukeketaji na kudai kuwa mwanamke aliyekeketwa anakuwa na thamani kubwa kama ilivyo kwa mwanamke mweupe kwa wasukuma, hii ni moja ya sababu zinazosababisha ukeketaji uendelee. Ikiwa elimu itaendelea kutolewa ukeketaji huu utapungua kwa kiasi kikubwa.
 "Ukatili wa ukeketaji ulikuwa unafanyika hadharani  kweupe, wazazi walikuwa wanalazimisha mabinti zao kukeketwa ili wapate mahali nyingi zaidi, ambapo fedha hizo ziwasaidie katika kupata kipato zaidi" - Nyakerandi Mariba. Swala hili limepungua sana kutokana na juhudi za wanamabadiliko kuendelea kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia.
"Maswala ya ukatili wa kijinsia yanaleta madhara makubwa katika jamii zetu,hasa kwa mabinti na akina  mama"-Lucy Matemba Afisa maendeleo ya jamii Tarime
Meneja wa kampeni ya Tunaweza Bi. Eunice Mayengela akiendelea kutoa Muongozo wa majadiliano
Wanamabadiliko wakiendelea kufuatilia mjadala
"Kila wiki tunapokea kesi zaidi ya kumi (10) zanazoripotiwa Tarime zikihusu kipigo,ubakaji, ulawiti na wanawake kutishiwa kuuwa,kupigwa sana kisha kubakwa kwa lazima ama kulawitiwa"- Dawati la Jinsia . Licha ya kesi hizo kuwa nyingi lakini elimu inayoendelea kutolewa na kampeni ya tunaweza imesaidia sana kupunguza ukatili wa kijinsia.
Wazee wa Kimila kutoka Tarime wakiteta jambo wakati wa mjadala
 Wanamabadiliko wakiwa katika picha ya pamoja.
Picha na Fredy Njeje

Monday, 19 June 2017

WAZIRI MKUU::TAIFA LA WATU WAADILIFU HUANZIA KWENYE FAMILIA

Image result for majaliwa
Picha /Maktaba
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema wazazi wana jukumu la kulea watoto kwenye misingi ya kumcha Mungu ili Taifa liweze kuwa na watu waadilifu na wachapakazi. 

“Taifa la watu waadilifu na wachapakazi huanzia katika ngazi ya familia. Kama kaya zetu haziishi kwa uadilifu, ni vigumu sana kuwa na Taifa lenye wananchi waadilifu. Ni muhimu basi familia zetu zihakikishe kuwa tunakuwa na watoto wenye hofu ya Mungu na wenye kumcha Mungu,” alisema.

Alitoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Juni 17, 2017) wakati akizungumza na wageni waliohudhuria harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa na nyumba ya Paroko katika Parokia Teule ya Zuzu, nje kidogo ya mji wa Dodoma. 

Harambee hiyo ilitanguliwa na ibada ya misa ya shukrani kwa ajili ya marehemu Mzee Xavery Mizengo Pinda, ambaye ni baba yake, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Peter Pinda. Mzee Xavery Pinda alifariki Novemba 27, mwaka jana katika hospitali ya mkoa wa Dodoma na kuzikwa kijijini kwake Kibaoni, wilayani Mlele, Katavi.

Waziri Mkuu alisema wazazi wanapaswa kujitathmini juu ya malezi ya watoto wao na kujihoji kama wamepata malezi yanayostahili. “Kupitia funzo tulilolipata leo, tujitathmini kuhusu makuzi ya watoto wetu. Je watoto wetu wanapata malezi stahiki? Je tunawalea katika misingi ya kutoa kwa ajili ya Mungu au tunawafundisha wajilimbikizie mali? Je, tunawahoji watoto wetu kuhusu utajiri wanaoupata ghafla? Au tunawapongeza na kufurahia bila kujua wanapata wapi utajiri huo?,” alihoji.

“Nitumie nafasi hii kuwasihi wazazi wote kwamba tujitahidi kuwekeza katika malezi ya watoto wetu. Ili tuwe kioo cha aina ya Taifa tunalotaka kulijenga, hatuna budi kuwalea watoto wetu katika misingi ya imani, uadilifu na uzalendo mkubwa kwa nchi yetu,” alisisitiza.

Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu na mke wake walichangia sh. milioni 10 ambapo jumla ya sh. milioni 160 zilikusanywa. Kati ya hizo, sh. 111,150,000 zilikuwa ni ahadi, sh. 38,447,000 zilikuwa ni fedha taslimu na sh. 10,403,000 zilikuwa ni vifaa vya ujenzi.
Mapema, akiongoza ibada ya shukrani, Makamu wa Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Padre Chesco Msaga alisema kila mtu anapaswa kumshukuru Mungu kwani hakuna mwanadamu anayeweza kudai kuwa yuko jinsi alivyo kwa sababu ya akili zake. 

“Hata sisi tunasahau kumshukuru Mungu hasa pale mambo yetu yanapotunyookea. Tunadhani ni kwa akili zetu ndiyo mambo yetu yananyooka. Tunapaswa tukumbuke kuwa maishayetu yapo mikononi mwa Mungu, na yeye ndiye anajua njia zetu,” alisema akirejea mfano wa wakoma 10 walioponywa na Bwana Yesu na mmoja tu ndiye alirudi kushukuru.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda alisema harambee hiyo inafuatia uamuzi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya wa kuiteua Zuzu iwe parokia. 

“Sasa hivi tulikuwa na kigango. Kuteuliwa kuwa parokia maana yake tutakuwa na padre anakaa hapa Zuzu saa 24 na tutakuwa na ibada kila Jumapili, na katikati ya wiki kadri ratiba zitakavyoruhusu. 

“Kikubwa tunachopaswa kufanya kufuatia uamuzi huo, ni kuhakikisha kuwa mapadre wana nyumba ya kuishi. Sasa hivi, wa kwetu anakaa Dodoma mjini. Kwa hiyo tuna kazi ya kukarabati kanisa, lakini kwanza tukamilishe ujenzi wa nyumba ya mapadri,” alisema wakati akielezea madhumuni ya harambee hiyo. 

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA. 
JUMAPILI, JUNI 18, 2017.

Tuesday, 29 November 2016

25 MBARONI KWA BIASHARA YA UKAHABA MOSHI


Image result for UKAHABA
Moshi. Watu 66 wakiwamo wanawake 25 wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya kuuza miili maarufu kama dadapoa katika maeneo mbalimbali ya mjini Moshi, wanashikiliwa na polisi.

Licha ya kuwashikilia wanawake hao, polisi wamewakamata wafanyabiashara saba wanaojihusisha na biashara za dawa za kulevya na watumiaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita amesema watu hao walikamatwa Novemba 26 saa mbili usiku kwenye maeneo ya katikati ya mji katika operesheni ya kutokomeza biashara hizo haramu.

“Tukiwa na Diwani wa Mawenzi, Hawa Mushi tulishirikiana kuwakamata wahalifu mbalimbali katika mji wetu maana nyakati za usiku kuna mambo yanafanyika ambayo tusipoweza kuyakabili  mapema yanaweza kuleta madhara baadaye,” amesema Moita.

 Moita amesema baadhi ya wafanyabiashara wadogo ndiyo chanzo cha kuuza dawa za kulevya na huwaficha wanawake wanaofanya biashara ya miili yao usiku.

“Tumewakamata wanawake wanauza miili yao 25, wafanyabiashara wanaowalinda wanawake hao na kuuza dawa za kulevya saba na walikutwa wakitumia dawa hizo nao wako saba,” amesema Moita.

Saturday, 26 November 2016

MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO AZINDUA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI KANDA YA KASKAZINI

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Said Mecky Sadiki akizungumza wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ,uzinduzi iliofanyika katika viwanja wa vya kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi.Mwenyekiti wa Kamati ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia,Elizabeth Mushi akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatli wa kijinsia.Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi katika Shule ya Polisi Theresia Nyangasa akisoma taarifa juu ya vitendo vya kuutali na njia zilizoanza kuchukuliwa katika kukabiliana navyo wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili kanda ya Kaskazini .Mwenyekiti wa TAWREF ,Dafrosa Itemba akitoa taarifa juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa kanda ya kaskazini uliofanyika katika viwanja vya kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Elizabeth Mushi akipeana mkono na Mgeni rasmi katika unzinduzi huo,Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Said Mecky Sadiki mara baada ya kutoa taarifa juu ya ukatili

Uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kanda ya kaskazini ulitanguliwa na maandamano yaliyopita katika barabara mbalimbali za mji wa Moshi na kuhitimishwa katika viwanja vya kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi.
Washiriki kutoka Asasi mbalimbali wakipita mbele na mabango yakiwa na ujumbe mbalimbali katika uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kanda ya kaskazini.
Baadhi ya viongozi wa taasisi mablimbali wakiwa wameketi meza kuu na mgeni rasmi wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili kanda ya kaskazini Said Mecky Sadiki.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kippi Warioba akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ,Said Mecky Sadiki kutoa hotuba yake wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupina ukatili wa kijinsia.
Baadhi ya washiriki katika uzinduzi huo wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Said Mecky Sadiki pamoja na Mkuu wa wilaya ya Moshi Kippi Warioba wakifuatilia taarifa juu ya ukatili wa kijinsia iliyokuwa ikitolewa na viongozi wa Asasi mbalimbali .
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro akitoa cheti kwa Kaimu Kamnada wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro Koka Moita cha kutambua mchango wa jeshi la Polisi katika kupamban vita dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Said Mecky Sadiki akipena mkono kabla ya kumkabidhi cheti Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF Network) Grace Lyimo ,kutambua mchango wake katika vita dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Said Mecky Sadiki akipeana mkono na Mwenyekiti wa Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi wilaya ya Moshi,Elina Maro kabla ya kumkabidhi cheti kutambua mchango wake katika vita dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Mkuu wa wilaya ya Moshi,Kippi Warioba akipata maelezo kutoka kwa baadhi ya washiriki alipopita kugagua mabanda ya maonesho ya shughuli zinazofanywa na taaisisi zinazopambana na ukatili wa kijinsia.


                            Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya
 Kaskazini.

Thursday, 24 November 2016

IFAHAMU MIKOA MITANO INAYOONGOZA KWA NDOA ZA UTOTONI TANZANIA

Tanzania imetajwa kuwa ni moja kati ya nchi zenye viwango vya juu vya matukio ya ndoa za utotoni. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika utafiti uliochapishwa mnamo Januari, 2016 uliitaja kuwa ni nchi ya tatu barani Afrika kwa matukio ya ndoa na mimba za utotoni kwa 28%.

Kutokana na shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), kwa wastani watoto wakike wawili kati ya watano huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18. Pia takwimu za utafiti wa Idadi ya watu na Afya Tanzania (TDHS, 2010) 37% ya watoto wa kike Tanzania huolewa kabla ya kufikisha miaka 18.

Takwimu za shirika la Watoto Duniani (UNICEF 2012) lilitaja mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni huku mkoa wa Shinyanga ukiongoza kwa 59%, ukifuatiwa na Tabora 58%, Mara 55%, Dodoma 51%, Lindi 48%.

Mikoa mingine inayofatia ni pamoja na Mbeya 45%, Morogoro 42%, Singida 42%, Rukwa 40%, Ruvuma 39%, Mwanza 37%, Kagera 36%, Mtwara 35%, Manyara 34%, Pwani 33%, Tanga 29%, Arusha 27%, Kilimanjaro 27%, Kigoma 26%, Dar es Salaam 19% na Iringa 8%.

Sababu kuu zinazochangia kukua kwa tatizo hili ni pamoja Mila na desturi potofu, Sheria na sera kinzani, Mifumo dhaifu ya uongozi katika ngazi ya kata, vijiji, Mitaa na vitongoji.

Sunday, 6 November 2016

KAMPENI YA BINTI WA KITAA YAFIKA WILAYA YA TEMEKE JIJINI DAR, WAKAZI WAPATA ELIMU JUU YA KUZUIA MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI


 Afisa Mtendaji wa Wilaya ya Tandika Hija Kipeleka akizindua Rasmi kampeni ya Binti wa kitaa katika Wilaya ya Temeke, ambapo aliwashukuru wanaoendesha kampeni hiyo na kuahidi kushirikiana nao katika kupinga mimba na ndoa za utotoni.
 Mkurugenzi Mtendaji wa CVIF George David  Maarufu kwa jina la Ambassador Angelo akielezea kwa kina kampeni ya Binti wa kitaa ilivyo wasaidia mabinti wengi na kutoa ufafanuzi wa kina juu ya kampeni hiyo ambapo kwa sasa inaendelea kuzinduliwa katika Wilaya zilizopo jijini Dar.
 Mkazi wa Mtaa wa Mvomero Tandika Bi. Rauva Maulid akieleza namna akina baba walivyo na tabia ya kuwarubuni mabinti wenye chini ya umri wa miaka 18 na kuwababishia Mimba,na kuongeza kuwa kwa tandika watoto wengi wanapata mimba wakiwa na miaka kuanzia miaka 12.
 Mkazi wa Mtaa wa Mvomero Said Mgeni akisisitiza kuwa wazazi wanatakiwa kuwa jirani na watoto wao ili waweze kuwa rafiki na kuwaeleza matatizo wanayoyapata kwa sababu kwa kufanya hivyo mabinti watakuwa huru kueleza matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na tatizo la mimba.
 Aisha mkazi wa Tandika akieleza namna vijana wanavyowarubuni na kuwasumbua ili waweze kushiriki nao katika ngono uzembe.
 Mkazi wa Mtaa wa Sheraton Tandika Fatuma akieleza namna baadhi ya mabinti wenye umri chini ya Miaka 18 wanavyopata mimba kutokana na kurubuniwa kufanya ngono uzembe na kuwapelekea kupata Mimba, na kuwasihi wasiwe wepesi kudanganyika na vijana.
 Binti huyu aliyetambulika kwa jina moja tuu Mwajuma akieleza alivyo achishwa Shule akiwa kidato cha pili kutokana na kukosa fedha za masomo hivyo timu ya Binti wa kitaa kwa kushirikiana na Serikali ya Mtaa wa Tandika kwa pamoja wameungana kumsomesha Binti huyo SIDO kwa kuwa anapenda kuja kuwa mfanyabiashara.
 Anaitwa Amani Muuza Juice ya Miwa maarufu mtaa wa sokoni akielezea jinsi Mimba za utotoni zinavyowaharibia maisha mambinti wenye  umri chini ya Miaka 18, na kuwasihi wananchi wote kuipa sapoti kampeni ya Binti wa kitaa
Muwezeshaji katika uzinduzi wa kampeni ya Binti wa Kitaa Zero akitoa elimu juu ya kuzuia mimba na ndoa za utotoni
 Kampeni ya Binti wa Kitaa huwakutanisha Mabinti pamoja na watu wa rika zote, hapa Msema chochote Steven Mfuko  maarufu kwa Jina la Zero akiwa na Bibi Zakia Seif akiwafunda mabinti wenye umri chini ya Miaka 18 kutokuwa na papara ya kukimbilia katika ngono.
 Mmoja ya wageni waliofika katika kampeni ya Binti wa Kitaa Jesca Kitomary alishauri kuwa wazazi wanatakiwa kuwaelimisha mabinti wao juu ya athari za mimba za utotoni  na kuolewa mapema, kwa kufanya hivyo itawasaidia kupata mimba na kuolewa kwa muda.
 Meneja wa Kampeni ya Binti wa Kitaa Mhandisi Eliwanjeria James kutoka kikundi cha wanawake Ma Injinia Tanzania akitoa shukurani kwa wote waliofika katika kufanikisha uzinduzi wa Kampeni ya Binti wa kitaa katika  Wilaya ya Temeke
 Mwakilishi wa Sunshine Group Fatuma akizungumza jambo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Binti wa kitaa Temeke
 Wakiendelea kufuatilia kwa makini masomo mbalimbali wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Binti wa kitaa
Baadhi ya watu zaidi wakiwa katika pande mbalimbali wakifuatilia uzinduzi wa kampeni ya Binti wa Kitaa 
Baadhi timu ya Binti wa kitaa pamoja na wakazi wa Tandika wakiwa katika picha ya pamoja
Picha na Fredy Njeje/Blogs za Mikoa

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA