Monday, 17 August 2026

Kwa Nini Marubani Wanavaa Mistari ya Dhahabu Mabegani?

 


Ukiwa uwanja wa ndege, huenda umewahi kumuona rubani akitembea kuelekea kwenye ndege akiwa amevalia sare nadhifu, kofia maalum na mistari ya dhahabu mabegani. Muonekano huo umekuwa sehemu inayotambulika sana ya taaluma ya urubani duniani.

Lakini je, umewahi kujiuliza mistari hiyo ilianzia wapi na ina maana gani?

Hadithi yake inaturudisha nyuma hadi katika miaka ya mwanzo ya ukuaji wa usafiri wa anga wa kibiashara, hususan miaka ya 1930.

Anga Ilipokopa Utamaduni wa Baharini

Katika kipindi hicho, baadhi ya ndege zilizotumika kusafirisha abiria zilikuwa aina ya flying boats — ndege zilizokuwa na uwezo wa kutua na kuondoka juu ya maji.

Kwa kuwa usafiri huo ulikuwa na uhusiano mkubwa na mazingira ya baharini, mashirika ya ndege yakaanza kukopa baadhi ya mila na mifumo iliyokuwa tayari imezoeleka katika jeshi la wanamaji.

Jeshi la wanamaji lilikuwa na mfumo ulio wazi wa sare, vyeo, mamlaka na nidhamu. Hivyo, mashirika ya ndege yaliona mfumo huo kuwa njia nzuri ya kujenga taswira ya utaalamu, uwajibikaji na mamlaka miongoni mwa wafanyakazi wao.

Kwa abiria wa kipindi hicho, kusafiri kwa ndege bado lilikuwa jambo jipya na kwa wengi lilihitaji ujasiri mkubwa. Sare rasmi za marubani zilisaidia kuwapa abiria hali ya kujiamini kwamba ndege ilikuwa chini ya usimamizi wa wataalamu wenye mafunzo na majukumu yanayotambulika.

Ndipo utamaduni wa mistari mabegani ukaendelea kukua na kuwa sehemu ya taswira ya rubani wa ndege za kiraia.



Mistari ya Dhahabu Inaashiria Nini?

Leo, mistari hiyo haitumiki tu kama mapambo ya sare. Mara nyingi husaidia kutambulisha nafasi na kiwango cha majukumu ya rubani ndani ya kikosi cha ndege.

Kwa kawaida, mfumo unaweza kuonekana hivi:

Mstari mmoja unaweza kutumiwa kumtambua rubani mwanafunzi au rubani aliye katika hatua za awali za mafunzo na majukumu.

Mistari miwili inaweza kuhusishwa na rubani mwenye nafasi ya awali katika uendeshaji wa ndege, kutegemea mfumo unaotumiwa na shirika husika.

Mistari mitatu mara nyingi huonekana kwa First Officer, au rubani mwenye uzoefu na majukumu ya juu zaidi katika baadhi ya mashirika ya ndege.

Na unapomuona rubani akiwa na mistari minne, mara nyingi huyo ndiye Captain — Nahodha wa Ndege. Captain ndiye mwenye mamlaka ya juu katika uendeshaji wa ndege wakati wa safari na hubeba jukumu kubwa katika kuhakikisha ndege, abiria na wafanyakazi wanafika salama katika safari yao.

Hata hivyo, mpangilio wa mistari unaweza kutofautiana kati ya shirika moja la ndege na jingine kutokana na mifumo yao ya ndani.




Zaidi ya Sare

Kwa hiyo, mistari ya dhahabu unayoiona mabegani mwa rubani ina historia ndefu kuliko ambavyo wengi wanaweza kudhani.

Ni utamaduni uliotokana kwa kiasi kikubwa na mifumo ya baharini na ambao baadaye ukawa sehemu ya utambulisho wa taaluma ya urubani.

Zaidi ya kuonyesha cheo, sare ya rubani imeendelea kuwakilisha nidhamu, taaluma, uwajibikaji na mamlaka — sifa ambazo ni muhimu katika sekta ambayo usalama ni kipaumbele cha kwanza.

Na unapomuona rubani mwenye mistari minne akielekea kwenye chumba cha rubani wakati mwingine, sasa utajua kuwa zile si alama za mapambo pekee.

Zinaelezea nafasi, wajibu na sehemu ya historia ndefu ya usafiri wa anga.

Nchini Tanzania, shughuli za urubani wa kiraia zinasimamiwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ambayo pamoja na majukumu mengine, husimamia utoaji wa leseni na viwango vya kitaaluma kwa marubani na wataalamu wengine wa sekta ya usafiri wa anga ili kuhakikisha shughuli za anga zinaendeshwa kwa usalama na kwa kuzingatia matakwa ya kisheria na kitaaluma.

Monday, 13 July 2026

TCAA KUWAHUDUMIA WATEJA WAKE KIMKAKATI

 Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na wadau kupitia Dawati la Huduma kwa Wateja, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa, kupokea maoni na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa haraka na kwa ufanisi.

Akizungumza katika Banda la TCAA kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa wa Dawati la Huduma kwa Wateja, Bw. Rashid Mngoya, alisema dawati hilo limeanzishwa ili kuwa kiungo kati ya Mamlaka na wananchi kwa kuwapatia taarifa sahihi kuhusu huduma mbalimbali za usafiri wa anga.

Alieleza kuwa kupitia dawati hilo, wadau wanaweza kuuliza maswali, kuwasilisha maoni, kutoa mapendekezo au changamoto wanazokutana nazo, pamoja na kupata mwongozo kuhusu taratibu mbalimbali zinazosimamiwa na TCAA.




Kwa mujibu wa Bw. Mngoya, uwepo wa dawati hilo unaimarisha mawasiliano kati ya TCAA na wateja wake, huku ukihakikisha hoja na malalamiko yanashughulikiwa kwa wakati ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa.

Alisisitiza kuwa TCAA itaendelea kuboresha huduma zake kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa katika usalama, ulinzi na utoaji wa huduma bora kwa wadau wote wa sekta ya usafiri wa anga.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa TCAA, Bw. Ally Changwila, alisema Mamlaka imefanya maboresho mbalimbali katika mifumo yake ya mawasiliano ili kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi. Alitaja mojawapo ya maboresho hayo kuwa ni tovuti ya TCAA ambayo sasa inapatikana kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, ikiwa na taarifa zilizoboreshwa na sehemu maalum ya Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQs) ili kuwasaidia watumiaji kupata majibu ya haraka kuhusu huduma mbalimbali.

Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Sabasaba, TCAA inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake ya kiudhibiti, haki na wajibu wa abiria, matumizi salama ya ndege zisizo na rubani (drones), pamoja na huduma nyingine zinazohusiana na sekta ya usafiri wa anga.


Hatua hizi zinaonyesha dhamira ya TCAA ya kuendelea kuboresha huduma kwa wateja, kuimarisha mawasiliano na wadau na kuongeza uelewa wa umma kuhusu mchango wa Mamlaka katika kuhakikisha sekta ya usafiri wa anga nchini inaendelea kuwa salama, yenye ufanisi na kuendana na viwango vya kimataifa.

Wednesday, 25 February 2026

WATAALAM WA SHERIA ZA USAFIRI WA ANGA DUNIANI WAKUTANA DAR ES SALAAM


Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari akizungumza wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa Warsha juu ya Mikataba ya Sheria za Anga ya mwaka 2026 iliyoandaliwa na TCAA kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO)





Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bw. Salim Msangi akizungumza wakati wa ufunguzi wa  Warsha juu ya Mikataba ya Sheria za Anga ya mwaka 2026 iliyoandaliwa na TCAA kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO)


Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria na Mahusiano ya Nje wa ICAO, Bw. Michael Gill akitoa salam kwa niaba ya ICAO wakati wa ufunguzi wa  Warsha juu ya Mikataba ya Sheria za Anga ya mwaka 2026 iliyoandaliwa na TCAA kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO)




Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi akiwa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria TCAA Bi. Maria Memba wakati wa ufunguzi wa Warsha juu ya Mikataba ya Sheria za Anga ya mwaka 2026 iliyoandaliwa na TCAA kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO)




Washiriki wakisikilza yanayojiri wakati wa ufunguzi wa Warsha juu ya Mikataba ya Sheria za Anga ya mwaka 2026 iliyoandaliwa na TCAA kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO)




Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari amesema Serikali imeongeza msukumo wa mageuzi ya sheria za usafiri wa anga nchini.

Akifungua Warsha juu ya Mikataba ya Sheria za Anga ya mwaka 2026 iliyoandaliwa na TCAA kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO), Mheshimiwa Johari alisema sekta ya anga inakabiliwa na mageuzi makubwa yanayotokana na matumizi ya Akili Bandia (AI), ndege zisizo na rubani, mifumo ya kidijitali na ongezeko la vitisho vya usalama mtandao.


Mhe. Johari, aliongeza kuwa, kwa kutoa wito wa kuharakishwa kwa uridhiaji na uingizaji wa mikataba ya kimataifa ya anga katika sheria za kitaifa ili kuendana na mabadiliko ya kasi katika sekta hiyo.


Alibainisha kuwa ingawa teknolojia hizi zinafungua fursa kubwa za ubunifu na ufanisi, pia zinaibua maswali magumu ya kisheria na kimaadili. Hivyo, alisisitiza umuhimu wa nchi kutafakari upya namna ya kutunga, kusimamia na kutekeleza sheria za anga.

Mheshimiwa Johari alieleza kuwa usafiri wa anga una mchango mkubwa katika kuunganisha watu, masoko na tamaduni, kuchochea ukuaji wa uchumi, biashara na utalii. Hata hivyo, alionya kuwa manufaa hayo yanategemea mfumo thabiti na ulioratibiwa wa sheria za kimataifa za anga.


Warsha hiyo ya siku tatu imewakutanisha zaidi ya washiriki 150, wakiwemo takriban wajumbe 70 kutoka mataifa mbalimbali, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu mikataba ya anga, kubainisha faida na wajibu wa nchi wanachama, na kujadili mbinu za uridhiaji na utekelezaji wake.


Na kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Bw. Salim Msangi, alisema warsha hiyo ni jukwaa muhimu la kujifunza na pia kichocheo cha mageuzi ya ndani. Alieleza kuwa TCAA inatumia fursa hiyo kutathmini mikataba ambayo Tanzania haijaridhia na kuharakisha hatua za kuiingiza katika sheria za kitaifa.


Alifafanua kuwa kuridhia mikataba ya kimataifa kunasaidia kuleta uwiano wa taratibu na hatua za kiutendaji miongoni mwa nchi wanachama, hivyo kuongeza uhakika na utabirika katika shughuli za usafiri wa anga wa kimataifa.


Naye, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria na Mahusiano ya Nje wa ICAO, Bw. Michael Gill, alisisitiza kuwa uridhiaji na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ya anga ni msingi wa kuhakikisha usafiri wa anga ulio salama, wa uhakika na endelevu duniani. Alibainisha kuwa tangu mwaka 1947, Kamati ya Sheria ya ICAO imeandaa mikataba 24 inayounda msingi wa mfumo wa kisheria wa usafiri wa anga duniani chini ya Mkataba wa Chicago, uliotimiza miaka 80 hivi karibuni.


Aliongeza kuwa Mpango Mkakati mpya wa ICAO wa 2026–2050 unaweka msisitizo zaidi katika kuimarisha uwezo wa kisheria wa nchi wanachama na kuoanisha sheria za anga ili kukabiliana na changamoto mpya za kimataifa.

Tuesday, 3 February 2026

KAMA KWELI UNAHITAJI MWENZI WA MAISHA: HII INAKUHUSU



 
Ni njia gani za kumpata mwenzi wa maisha yako? Inawezekana unakabili mtihani mzito, hujui ni yupi wa nafsi yako. Bila shaka unamtaka yule wako wa kufa na kuzikana.

Mada hii inakuja na suluhisho mahsusi kwako, kumjua mapema anayekufaa, anayeweza kudumu nawe maishani. Zingatia kwamba mwenzi sahihi wa maisha yako ni hatua muhimu kuelekea kwenye mafanikio.

KWANZA TAMBUA HILI

Uhusiano wa kimapenzi ni suala binafsi. Kwanza kabisa ni sanaa inayokutaka uangalie mahitaji yako mwenyewe. Je, unahitaji nini kwa mtu ambaye ungependa awe mwenzi wa maisha yako?

Yale unayotaka kutoka kwa mtu ambaye unapenda awe mwenzi wa maisha yako, unapaswa kuyapa kipaumbele. Hata siku moja, usithubutu matamanio ya mwili na moyo yakupe mwongozo wa kumwona umpendaye.

NANI MWENZI WA MAISHA?

Ni swali ambalo unapaswa kujiuliza. Kwa uwazi kabisa, unatakiwa kuzingatia kuwa mwenzi wa maisha ni yule ambaye utachangia naye mambo mengi kwa uaminifu na maelewano makubwa.

Mwenzi wa maisha si mtu unayeweza kuwa naye kwa mantiki ya kupeana tulizo la ngono unapohitaji au kampani ya kwenda kuangalia ‘muvi’, muziki, ufukweni na kwingineko unapoona huhitaji kuwa peke yako.

Mwenzi wa maisha ni yule atakayefanya ujione umekamilika, bila kujali ‘ubize’ wala ukapa ambao pengine unao ndani ya jamii inayokuzunguka. 

Kingine cha kuzingatia ni kwamba, mwenzi wa maisha yako ni yule ambaye anakukubali na kukupenda kama ulivyo, bila kuwepo kwa nyongeza ambazo zitatokana na kukubadilisha kutoka yule wa zamani.

Kupata mwenzi wa maisha mwenye sifa kamili, ni sawa na kupatia herufi ya mwisho kwenye mchezo wa kubahatisha. Kwa maana hiyo, baada ya kumpata, kila kitu kinakuwa kimekamilika maishani mwako.

NANI MWENZI WA MAISHA YAKO?

Pointi ya msingi kuzingatia ni kwamba unahitaji kuwa na yule anayekubalika ndani ya nafsi yako. Hivyo basi, fikiria kwa yale yanayoweza kukufanya uwe na furaha, pia yanayoweza kukupa huzuni.

Zingatia mapitio yako ya nyuma kuona ni kwa namna gani yamekutengeneza mpaka kufika ulivyo sasa. Jiulize pia kuhusu ndoto na malengo yako siku za usoni.

Ikiwa tu utaweza kutambua mahitaji na matarajio yako ya kimaisha, bila shaka utaweza kutambua ni mtu gani anayefaa katika kukusaidia kutimiza kila kilichomo ndani ya malengo yako.

JENGA IMANI

Kutafuta mwenzi wa maisha siyo suala la kuangalia mtu wa kwenda naye klabu kujirusha usiku. Vile vile ni muhimu kutambua kwamba inaweza kukuchukua muda kupata mtu wa kukidhi vigezo vyako.


Pamoja na ukweli huo, bado unatakiwa uwe na imani kwamba itafika wakati utasahau habari za kutafuta mwenzi na utakuwa mwenye furaha, ukijipongeza kwa kumpata anayekufaa.

Mapenzi ni mchezo lakini ni rahisi kuucheza ukitambua kanuni zake. Hii ina maana kuwa unapokuwa kwenye kipengele hiki, unakuwa na jukumu moja zito la kuhakikisha unampata yule mwenye uwezo wa kukonga moyo. Mwenye sura ya kutimiza malengo yako.

Hata hivyo, muhimu kwako ni kuwa mtulivu na kuacha macho yafanye kazi ya kuangaza kwa utaratibu, halafu akili ifanye kazi ya kutathmini kiwango cha huyo atakayeonwa.

Kitu kingine ambacho unatakiwa kuheshimu ni kuwa, wawili wanaopendana, kila mmoja kwa nafasi yake ni nusu ya kitu kizima kinachoitwa ndoa au wapenzi, hivyo wanapounganishwa ndiyo kinapatikana kitu kizima.

Ukiamini kuwa wewe ni nusu na utakamilika baada ya kukutana na mwenzi wako, unachotakiwa kufanya ni kujenga imani kwamba mwenzi wako yupo sehemu kwa ajili yako, hivyo endelea kumtafuta na siku moja utamuweka mikononi mwako. 

Saturday, 10 January 2026

NJIA ZA KUKABILIANA NA UCHOVU MWINGI

Image result for A TIRED BLACK PERSON
Uchovu unaotokana na kazi ni zaidi ya kuchoka kwa kawaida, na unazidi uchovu unaosababishwa na shughuli za kila siku. Dalili za uchovu huo ni kuchoka kupita kiasi kwa muda mrefu na vilevile kuhisi umekata tamaa na kukosa nguvu. Watu wanaokabili uchovu huo hawafurahii kufanya kazi zao, yaani, wanakosa hamu ya kufanya kazi na hivyo kuathiri ubora wa kazi. Utafiti pia unaonyesha kwamba kuchoka kupita kiasi husababisha matatizo ya kihisia na magonjwa.
Ni nini kinachosababisha uchovu mwingi?
Kwa kawaida kazi nyingi kupita kiasi ndicho chanzo kikuu. Kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi, baadhi ya waajiri hutaka wafanyakazi wao wafanye kazi saa nyingi zaidi, na bila malipo ya kutosha. Maendeleo ya teknolojia hufanya iwe vigumu kwa watu fulani kutenganisha shughuli za kikazi na maisha ya binafsi. Nao wengine hupatwa na uchovu huo kwa sababu wanahofu kupoteza kazi zao, hawawezi kuzidhibiti, au wanahisi kwamba wanaonewa. Vilevile kutojua majukumu yao kazini au migogoro kati yao na wafanyakazi wenzao huchangia kuchoka kupita kiasi.
Uchovu mwingi pia unaweza kusababishwa na mtu mwenyewe. Ili wafikie malengo yao na kupata pesa nyingi, baadhi ya watu hufanya kazi zaidi ya moja. Watu hao wana majukumu mengi na wanakabili hatari ya kuchoka kupita kiasi.
Ikiwa unakabili tatizo la kuchoka kupita kiasi kazini, unawezaje kushinda tatizo hilo? Huenda ikaonekana vigumu kushinda tatizo hilo ikiwa kuna mambo yanayopita uwezo wako. Hata hivyo, chunguza hatua nne zifuatazo za kukabiliana na kuchoka kupita kiasi. Unaweza kupata suluhisho la tatizo lako.

1. CHUNGUZA MAMBO UNAYO YAPA KIPAUMBELE.

Ni nini muhimu zaidi kwako? Watu wengi wanasema kwamba uhusiano na familia zao na afya njema ndiyo mambo muhimu zaidi. Hivyo, ukichoka kupita kiasi familia yako itaathirika na afya yako itazorota.
Ukizingatia mambo muhimu, itakuwa rahisi kwako kufanya maamuzi magumu na kukataa majukumu fulani. Kwa mfano, unaweza kugundua kwamba kazi yako inakusababishia uchovu unaopita kiasi. Hata hivyo, huenda ukasema, ‘Siwezi kubadili kazi au kupunguza muda ninaofanya kazi; ninahitaji pesa!’ Ni kweli, kila mtu anahitaji pesa, lakini kazi yako inaathirije mambo unayothamini zaidi?
Uwe mwangalifu ili usitangulize mambo ambayo wengine wanaona kuwa muhimu. Huenda mambo ambayo ni muhimu kwa mwajiri wako yakatofautiana na mambo yaliyo muhimu kwako. Wengine wanaweza kutanguliza kazi kuliko mambo mengine maishani, lakini haimaanishi unapaswa kufanya hivyo.

2. RAHISISHA MAISHA YAKO.
Ili upunguze mkazo na upate muda wa kutimiza mambo unayothamini zaidi, huenda ukahitaji kufanya kazi kwa saa chache, kumwomba mwajiri wako akupunguzie majukumu, au ukahitaji kubadili kazi. Vyovyote vile, inaelekea utahitaji kupunguza matumizi ya fedha na kubadili mtindo wako wa maisha. Inawezekana kufanya marekebisho hayo, na huenda isiwe vigumu kama unavyowazia.
Katika nchi nyingi, wafanyabiashara wanashawishi watu wanunue bidhaa, na wengi wanafikiri kwamba furaha inatokana na kupata utajiri. Hata hivyo, si kweli. Maisha rahisi yanaweza kukuletea uhuru mwingi na kufanya uridhike. Ili ufanikiwe kufanya mabadiliko hayo, unahitaji kupunguza matumizi yako na kuweka akiba ya pesa. Jitahidi kupunguza au kuepuka madeni. Zungumza na familia yako kuhusu umuhimu wa mabadiliko hayo na uwaombe wakuunge mkono.

3. JIFUNZE KUFANYA  KAZI KWA KIASI.

Ikiwa una kazi nyingi kupita kiasi au tatizo lenye kudumu kazini, zungumza na mwajiri wako. Ikiwezekana, toa mapendekezo yanayofaa hali yako na pia mwajiri wako. Mhakikishie mwajiri wako kwamba unapenda kazi, na ufafanue yale ambayo uko tayari kufanya; lakini utaje waziwazi na kwa uthabiti mambo ambayo huwezi kufanya.
Mwanamume anayetazama saa yake
Uwe mwenye busara na uone mambo kihalisi. Ikiwa unataka kufanya kazi kwa saa chache, huenda mwajiri wako akapunguza mshahara wako. Fikiria pia uwezekano wa kufutwa kazi, na uwe tayari kukabiliana na hali hiyo. Si lazima uache kazi ili utafute kazi nyingine, ni rahisi kupata kazi nyingine ukiwa bado kazini.
Hata kama mwajiri wako atakubali ufanye kazi kidogo ujue kwamba huenda baadaye akasisitiza ufanye kazi zaidi. Ni nini kitakachokusaidia kudumisha msimamo wako? Jitahidi kudumisha makubaliano yenu ya awali. Kufanya hivyo kutakupa uhuru wa kumwomba mwajiri aendelee kufuata makubaliano hayo.

4. UWE NA MUDA WA KUPUMZIKA.

Hata ukifaulu kupunguza kazi, huenda bado utapatwa na mkazo, utashughulika na watu wagumu, au hali zisizopendeza. Uwe na muda wa kupumzika vya kutosha na uwe na burudani kwa kiasi. Kumbuka kwamba si lazima utumie pesa nyingi ili ufurahie burudani pamoja na familia yako.
Mbali na kazi, uwe na mambo unayofurahia kufanya na pia uwe na marafiki, na uepuke kufikiria kazi tu kila wakati. Kwa nini? Kitabu Your Money or Your Life kinasema hivi: “Utu wako ni muhimu kuliko kazi unayofanya ili kupata pesa.” Ikiwa unafikiri utambulisho wako au heshima yako inategemea kazi yako, huenda ukashindwa kuweka mpaka kati ya kazi na shughuli zako mwenyewe.

Monday, 13 October 2025

TCAA Yakabidhi Kisima cha Maji Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege Dodoma

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCAA, Dkt. Hamis Mwinyimvua, akikata utepe kuashiria ufunguzi wa kisima cha maji safi kilichojengwa kwa ufadhili wa TCAA kwa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCAA, Dkt. Hamis Mwinyimvua, akifungua maji kama ishara ya kukabidhi kisima cha maji safi kilichojengwa kwa ufadhili wa TCAA kwa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Dodoma. Kulia ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Cassian Henry.


Muonekano wa kisima cha maji safi kilichojengwa kwa ufadhili wa TCAA

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCAA, Dkt. Hamis Mwinyimvua, akisaini kitabu cha wageni alipowasili Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCAA, Dkt. Hamis Mwinyimvua akizungumza muda mchache kabla ya kukabidhi kisima

Afisa Elimu Kata, Bi. Prisca Barnabas akizungumza wakati wa mahafali 


Picha ya pamoja ya timu ya TCAA

Picha ya pamoja na uongozi wa kata, shule na wadau wa elimu

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCAA, Dkt. Hamis Mwinyimvua, akipanda mti kama ishara ya kuadhimisha miaka hamsini tangu kuanzishwa kwa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege wakitoa burudani ya ngoma wakati wa hafla hiyo


Dodoma, — Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imekabidhi rasmi kisima cha maji safi na salama katika Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege jijini Dodoma, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake iliyotolewa mwaka 2023 na sehemu ya juhudi za kurudisha kwa jamii na kuboresha mazingira ya elimu nchini.


Hafla hiyo ilifanyika sambamba na maadhimisho ya jubilee ya miaka 50 ya shule hiyo na mahafali ya wanafunzi wa darasa la saba, tukio lililohudhuriwa na wazazi, walimu, wanafunzi pamoja na viongozi mbalimbali wa elimu na serikali.


Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCAA, Dkt. Hamis Mwinyimvua, alisema taasisi hiyo itaendelea kuwa mlezi wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo hatua kwa hatua, ikiwa ni sehemu ya jitihada za TCAA za kurejesha kwa jamii.


“TCAA itabaki kuwa mlezi wa shule hii. Tutazidi kushirikiana na uongozi wa shule kutatua changamoto mbalimbali taratibu, ili kuhakikisha mazingira bora ya kujifunzia yanadumu. Maji ni uhai, na tunataka kila mwanafunzi hapa ajifunze katika mazingira safi na salama,” alisema Dkt. Mwinyimvua.


Kwa upande wake, Afisa Elimu Kata, Bi. Prisca Barnabas, aliishukuru TCAA kwa mchango huo muhimu na kuahidi kuhakikisha miundombinu ya maji inatunzwa kwa manufaa ya wanafunzi na jamii.

“Tunatoa shukrani za dhati kwa TCAA kwa kujali elimu. Tutahakikisha kisima hiki kinatumika ipasavyo na kudumu kwa muda mrefu,” alisema Bi. Prisca.


Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Cassian Henry, alisema kisima hicho kitarahisisha upatikanaji wa maji na kuboresha mazingira ya usafi na utunzaji wa bustani za shule.


“Kisima hiki ni msaada mkubwa kwetu. Kitatupa uwezo wa kudumisha usafi, kupunguza gharama, na kufanya shule yetu kuwa mazingira bora ya kujifunzia,” alisema Mwalimu Henry.


Katika kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo, Dkt. Mwinyimvua alipanda mti katika eneo la shule kama ishara ya utunzaji wa mazingira na kumbukumbu ya tukio hilo la kihistoria.


Kisima hicho chenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 20, kinatarajiwa kutatua changamoto ya maji kwa wanafunzi, walimu, na wakazi wa jamii inayozunguka shule hiyo.

Saturday, 11 October 2025

TCAA YAADHIMISHA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA KITOFAUTI




Afisa Habari na Uhusiano Mkuu TCAA, Zuhura Lwamo (katikati) akiwasikilza wadau wa usafiri wa anga waliofika kupata huduma katika ofisi ya TCAA kitengo cha taarifa za anga (briefing office)  uwanja wa ndege wa Arusha


Afisa Mtoa Taarifa za Usafiri wa anga wa  TCAA kituo cha uwanja wa ndege wa Arusha, Johneudes Mwombeki (kushoto) akifafanua jambo kwa mdau wa usafiri wa anga aliyefika kupata huduma katika ofisi hiyo


Afisa Habari na Uhusiano Mkuu TCAA, Zuhura Lwamo (katikati) akizungumza na mdau wa usafiri wa anga aliyefika kupata huduma katika ofisi ya TCAA kitengo cha taarifa za anga (briefing office) katika uwanja wa ndege wa Arusha


Meneja wa TCAA kituo cha Uwanja wa Ndege wa Arusha Jackson Ndalu akikabidhi zawadi kama ishara ya kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja



Kaimu Meneja Uhusiano na Mawasiliano TCAA, Ally Changwila (kulia) akiwakaribisha wadau wa usafiri wa anga waliofika Makao Makuu ya TCAA kupata huduma.

Muwezeshaji Rodrick Nabe akitoa mafunzo kwa watumishi wa TCAA kuhusu namna bora ya kutuoa huduma kwa mteja ikiwa ni sehemu wiki ya huduma kwa wateja




Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) inatumia fursa hiyo kusikiliza na kuhudumia wateja mbalimbali wanaofika katika ofisi zake, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha huduma bora na mahusiano mazuri na wadau wake. Maadhimisho haya ya kimataifa yanafanyika kila tarehe 6 hadi 10 Oktoba, yakilenga kuhimiza taasisi na mashirika kutoa huduma bora, zenye ubunifu na zenye kujali mahitaji ya wateja wao.

Katika kipindi hiki, TCAA inapokea na kushughulikia maoni, mapendekezo, na changamoto kutoka kwa makundi mbalimbali ya wateja, wakiwemo marubani, wahandisi wa usafiri wa anga, wanafunzi, na wawakilishi wa mashirika ya ndege. TCAA inaamini kupitia utaratibu huu wa kuwa karibu na wadau, Mamlaka inalenga kuboresha mifumo ya utoaji huduma na kuhakikisha kuwa kila mteja anapata huduma bora, kwa wakati na kwa ufanisi.

Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Mission: Possible – Mpango Umewezekana,” ambapo kwa upande wa TCAA, kauli mbiu hii inadhihirisha dhamira ya kuendelea kutoa huduma bora na zenye ubunifu unaolenga kumuweka mteja katikati ya huduma zote. Kupitia maadhimisho haya, TCAA inathibitisha kujituma kwa watumishi wake katika kufanikisha malengo ya taasisi, kuongeza ufanisi wa huduma, na kudumisha utamaduni wa ubora wa huduma kwa wateja.

Aidha, maadhimisho hayo yaliambatana na mafunzo kwa watumishi wa TCAA kuhusu utoaji wa huduma bora kwa wateja, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kutoa huduma zenye ubunifu, weledi, na zinazozingatia mahitaji ya wateja. Bila shaka, kwa TCAA – Mpango Umewezekana.

Saturday, 12 April 2025

TRANSFORM YOUR LEADERSHIP JOURNEY WITH MWALIMU JULIUS NYERERE LEADERSHIP SCHOOL

 



Embark on a transformative leadership journey at the Mwalimu Julius Nyerere Leadership School. Rooted in the timeless values of integrity, unity, and service, our programs are designed to nurture visionary leaders who are ready to shape the future of Africa.

Whether you're an aspiring leader or a seasoned changemaker, our immersive training, mentorship, and pan-African perspective will equip you with the tools to lead with purpose and impact. Join a legacy inspired by one of Africa’s greatest leaders – and become part of the change.

TUGHE TCAA YAPONGEZWA KWA USHIRIKIANO IMARA; YASISITIZWA KUHAMASISHA UANDIKISHAJI WA WANACHAMA WAPYA



Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Ndg. Amani Msuya akizungumza wakati wa ufunguzi wa  mkutano mkuu wa mwaka wa cha Chama cha Wafanyakazi wa Serikali kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) uliofanyika jijini Dodoma



Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wamepongezwa kwa kuandaa na kuendesha kwa mafanikio makubwa mkutano mkuu wa mwaka, hatua ambayo imewawezesha kujadili kwa kina taarifa mbalimbali za kiutendaji ndani ya chama na kuweka mapendekezo yenye lengo la kuongeza tija ndani ya TCAA.

Akifungua rasmi mkutano huo wa siku mbili uliofanyika jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Ndg. Amani Msuya aliwapongeza viongozi wa TUGHE TCAA kwa uendeshaji mzuri wa shughuli za chama kwa namna shirikishi, akieleza kuwa tawi hilo limekuwa mfano bora wa kuigwa na matawi mengine.

"Nawasihi viongozi waendelee kuhamasisha watumishi wengi zaidi kujiunga na TUGHE kwa sababu huo ndio uhai wa chama. Bila wanachama hai, hakuna chama hai. TCAA mmeonyesha njia nzuri, endeleeni kushikamana na kushirikiana," alisema Ndg. Msuya.

Kwa upande wake, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Sara Rwezaura aliwataka wanachama wa TUGHE TCAA kuwa wavumilivu wakati wa kuwasilisha hoja zao, na kusisitiza kwamba hoja zao ni muhimu na zisikaliwe kimya bali ziwasilishwe kwa mujibu wa taratibu.

Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la TCAA, Bi. Jackline Ngoda aliwashukuru viongozi wenzake kwa kuendelea kudumisha mshikamano ndani ya uongozi na kuahidi kuongeza nguvu katika kuhamasisha watumishi wengi zaidi kujiunga na TUGHE.

Naye Katibu wa TUGHE TCAA, Bw. Shukuru Mhina alisisitiza umuhimu wa mafunzo kwa viongozi wapya wa TUGHE akieleza kuwa ni kupitia mafunzo ndipo viongozi bora hujengwa.

Mkutano huu wa mwaka wa TUGHE TCAA umeendelea kuonesha mfano wa uwajibikaji, mshikamano na ushirikishwaji, hali inayoendelea kuimarisha misingi ya utendaji bora ndani ya taasisi.





Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Sara Rwezaula akitoa salamu za TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam  wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa cha Chama cha Wafanyakazi wa Serikali kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) uliofanyika jijini Dodoma


Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bi. Jackline Ngoda akizungumza kuhusu namna wanavyoshirikiana na viongozi wa TCAA pamoja na kumkaribisha Mgeni rasmi.


Katibu wa TUGHE Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA),Bw. Shukuru Mhina akifanywa utambulisho wa wajumbe wa mkutano mkuu wa mwaka wa TUGHE tawi la TCAA 



Wajumbe wa mkutano mkuu wa mwaka wa TUGHE tawi la TCAA wakiwasilisha michango wakati wa mkutano






Nsubisi Mwasandende Afisa Elimu Kazi na Mratibu wa Jinsia TUGHE akiwasilisha mada kuhusu mbinu za usajili na kuwatunza wanachama kwa wajumbe wa  mkutano mkuu wa mwaka wa TUGHE tawi la TCAA 




Mgeni rasmi akiwa kwenye picha ya pamoja na Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).





OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA