Showing posts with label UKATILI. Show all posts
Showing posts with label UKATILI. Show all posts

Tuesday, 22 August 2017

VIONGOZI WA SERIKALI WASHIKILIWA KWA MAUAJI YA WANAWAKE WATANO

Watu 32 wamefikishwa mahakamani kujibu shtaka  la mauaji ya wanawake watano yaliyotokea katika Kijiji cha Undomo Kata ya Uchama wilayani Nzega.

Miongoni mwa waliofikishwa mahakamani jana Jumatatu na kusomewa shtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Nzega, Sarafina Nsana wamo viongozi wa serikali ya kijiji hicho na  wengine wa ngazi ya kata.

Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Melito Ukongoji aliiambia mahakama kuwa Julai 25, washtakiwa kwa pamoja, wakiwa katika kijiji cha Undomo waliwashambulia kwa kuwapiga na kuwachoma moto hadi kufa wanawake watano kwa tuhuma za imani potofu za ushirikina.

Akisaidizana na mwenzake, Agustino Nshimba mwendesha mashtaka  huyo aliwataja waliouawa katika tukio hilo kuwa ni Nsuku Masali, Ester Kaswahili, Christina Saidi, Mwashi Mwinamila pamoja na Kabula Kagito.

Waliosomewa  mashtaka  ambao  hata hivyo  hawakutakiwa kujibu  lolote kwa  sababu mahakama  hiyo haina mamlaka ya  kusikiliza  na  kuamua mashauri ya  mauaji ni pamoja na Mtendaji wa Kata ya Uchama, Malewa Maroji, Diwani  wa Kata hiyo, Karoli Massanja, Kiongozi  wa  Sungusungu, Dotto Saraganda, mwenyekiti  wa kijiji, Ramadhani Kulwa na mtendaji wake, Rauliani Sanyiwa.

Washtakiwa wengine ni Dotto Saraganda (49), Taus Ngassa (40), Pill Kapewi (25), Leons Sospeter (36), Issah Eliudi (20), Nhungulu Sospeter (25), Saidi Nsabi(25), Emmanuel Pius(18), Estar Muhamila(25), Tatu Thomas (35), Thotunatus Ngelera (30), Milika Daudi (36), Kisuge Ntemi(31), Kulwa Kizinza (40), Shija Masali (35), na Kulwa shomali(31).

Wengine ni Selelo Mashandete (46),  Steven Saraganda (60), Paul Christoph (60), Makuya Athumani(42), Peter Mapalala(21), Maganga Daudi (19), Omary Seleli (20), Paul Emmanuel (51),Charles Kiberiti (26), Emmanuel Mihayo (27), Shomali Nhyama (75), pamoja na Shija Shomali (20).

Shauri hilo imeahirishwa hadi Septemba 4, itakapotajwa tena na muda wote wakati washtakiwa wakisomewa mashtaka dhidi yao,  jeshi la polisi liliimarisha ulinzi kuzunguka eneo la mahakama.

Saturday, 19 August 2017

MWANZA::MWANAMKE AUAWA KIKATILI KISHA MWILI WATELEKEZWA

Mwanamke mmoja amekutwa akiwa ameuawa na watu wasiyofahamika na mwili wake kutupwa kwenye nyumba ambayo haijamalizika kujengwa (Pagala) huku akiwa amefungwa kwenye mfuko wa sandarusi na kuzungushiwa nguo alizokuwa amevaa.

Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoani Mwanza, DCP Ahmed Msangi na kusema tukio hilo limetokea tarehe 16.08.2017 majira ya saa 11:30 jioni katika mtaa wa Kitangiri kata ya Kitangiri Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

DCP Msangi amesema mwili wa marehemu uliweza kuonekana mahali hapo baada ya watoto waliokuwa wakicheza eneo hilo kuona kifurushi kilichotupwa kwenye Pagala ndipo walipotoa taarifa kwa mama yao na baadaye kutoa taarifa kwa uongozi wa Mtaa pamoja na kituo cha Polisi.

Aidha, Kamanda Msangi amesema mwili wa marehemu haukuwa na jeraha lolote bali uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa wauaji walimuua kwa kumziba pumzi kisha kwenda kumtupa kwenye Pagala eneo ambalo siyo rahisi mtu kupita.

Kwa upande mwingine, DCP Msangi amesema upelelezi unaendelea wa kuwatafuta watu waliyohusika na mauaji ya mwanamke huyo kwa namna moja ama nyingine. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi.

Friday, 28 July 2017

WATANO WACHOMWA MOTO HADI KUFA KWA IMANI ZA KISHIRIKINA HUKO NZEGA

Watu watano wameuwawa kwa kuchomwa moto katika kata ya Uchama Wilayani Nzega Mkoani Tabora na watu wanaosaidikiwa kuwa ni Sungusungu huku wakidaiwa wameuliwa kutokana na imani za kishirikina.

Kufuatia Mauaji hayo Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agreya Mwanri, amezitaka Kamati za Ulinzi na usalama ngazi ya Mkoa na ile ya Wilaya ya Nzega kusitisha shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na sungusungu katika kijiji hicho.

Mwanri amesema kuwa amechukua hatua hiyo baada ya sungusungu hao kutekeleza mauaji hayo ya watu watano ambao wote ni wanawake wakituhumiwa kuwa ni washirikina.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Wilbroad Mutafungwa amesema kuwa katika kuendelea kuchunguza tukio hilo jeshi hilo linawashikilia baadhi ya viongozi wa kijiji hicho ili kuweza kubaini waliotekeleza tukio hilo.

Tuesday, 26 July 2016

WATU WAWILI WAUWAWA KATIKA TUKIO LA SHAMBULIZI LA RISASI HUKO FLORIDA


Watu wawili wameuwawa na wengine 16 kujeruhiwa katika tukio la shambulizi la risasi kwenye klabu ya usiku katika mji wa Fort Myers huko Florida, Marekani.

Shambulizi hilo limetokea kwenye Klabu ya Blu, ambayo ilikuwa ikifanya sherehe kwa kundi la vijana wenye umri mdogo.

Jeshi la polisi linawashikilia watu watatu, na kusema kuwa tukio hilo halina uhusiano na tukio la ugaidi.
   Watu wakiangua vilio katika eneo la Klabu Blu, kufuati tukio la shambulizi la kutumia risasi
                                           Kioo cha gari kilichovunjika baada ya risasi kupenya

Friday, 17 June 2016

KENYA::MWALIMU AFUNGWA JELA MIAKA 90 KWA KUWADHALILISHA KINGONO WATOTO 10

Mwalimu mmoja wa shule ya msingi nchini Kenya amehukumiwa kifungo cha siku 90 jela baada ya mahakama ya Murang'a kumtia hatiani kwa kuwadhalilisha kingono watoto 10 wa kiume.

Hukumu hiyo iliyotolewa jana wakati Afrika ikiadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, imeagiza mwalimu huyo kutumikia kifungo cha miaka tisa kwa kila mtoto mmoja aliyemdhalilisha.


Kwa hukumu hiyo Mwalimu huyo John Gichia Mugi atatoka gerezani akiwa na umri wa miaka 113 kama ataweza kubakia kuwa hai hadi kufikia umri huo.

Tuesday, 14 June 2016

WENGI WAKUSANYIKA KUOMBOLEZA JUU WALIOUWAWA ORLANDO

Wengi walishindwa kujizuia na kutokwa na machozi



Maelfu ya watu wamekusanyika huko Orlando Marekani usiku wa jumatatu, kuwakumbuka na kuwaombea watu 49 waliouwawa kwa mashambulizi ya kikatili ya risasi kwenye Klabu ya Usiku ya Mashoga siku ya jumapili.

Picha za watu 49 waliouawa kwa kupigwa risasi katika klabu ya usiku ya watu wenye mapenzi ya jinsia moja mjini Orlando, Marekani siku ya jumapili. 
  Watu wakiwa wamekumbatiana kwa majonzi wakati wa kuwaomboleza  waliouwawa Orlando
           Vilio vikiwa vimetawala wakati wa kuwaomboleza watu 49 waliouwawa Orlando

Watu wakiwa na mishumaa wakiomboleza wenzao waliouwawa kwenye Klabu ya Pulse huko Orlando

Monday, 13 June 2016

MTU MWENYE SILAHA AUWA WATU 50,AJERUHI WENGINE 53 KWENYE KLABU YA MASHOGA MAREKANI


Watu 50 wamethibitishwa kufa katika tukio la shambulizi la silaha kwenye klabu ya usiku ya mashoga huko Orlando, Florida, huku hali ya tahadhari ikitangazwa kwenye mji huo na Meya Buddy Dyer.

Mtu huyo aliyekuwa na silaha ametambulika kama Omar Mateen, naye aliuwawa baada ya kuwashikilia watu mateka. Watu wengine 53 wamejeruhiwa kwenye tukio hilo katika klabu ya Pulse.
Tukio hilo la shambulizi la kutumia silaha ni baya kuwahi kutokea katika historia ya Marekani, ambapo tayari polisi wamesema ni tukio la kigaidi lililotokana na misukumo ya kiimani.
Akilihutubia taifa Rais wa Marekani , Obama alisema shambulio hilo ni ishara ya ugaidi na chuki huku akisisitiza kuwa siyo tu kwa jamii ya mashoga bali ni kwa jamii nzima ya Marekani.
Polisi akiwa amevalia nguo za kazi katika eneo la tukio la kigaidi huko Orlando, Florida Marekani


















Mshambuliaji aliyeuwawa Omar Mateen akiwa amepozi akijipiga picha za Selfie kwa kutumia simu na kioo.

Sambamba na hilo mgombea anewania kuteuliwa na chama chake kuwania Urais Donald Trump amezidi kupigilia msumari msimamo wake  juu ya waislamu wenye itkadi kali na aliandika haya katika mtandao wa kijamii wa twiter.
 
Watu waliopatwa na mshtuko baada ya kutokea tukio hilo la shambulizi la kutumia risasi katika klabu ya Pulse.

Saturday, 11 June 2016

MWANAMUZIKI CHRISTINA GRIMMIE AUWAWA KWA KUPIGWA RISASI KICHWANI


Mwanamuziki Christina Grimmie ambaye aliwahi kushiriki katika kipindi cha televisheni cha The Voice, amepigwa risasi kichwani na kufa baada ya kumalizika tamasha lililofanyika Orlando, polisi wa Florida wamesema.

Taarifa imeeleza kuwa Grimmie alipigwa risasi na mshambuliaji huyo wakati akitia saini yake kwa moja wa shabiki, ambapo mshambuliaji huyo alidhibitiwa na kaka wa Grimmie lakini baadaye alijipiga risasi na kujiua.

Grimmie mwenye umri wa miaka 22, alifariki dunia baadaye akiwa hospitali. Mwaka 2014 Grimmie alifanikiwa kumaliza shindano la kuimba la The Voice na kushika nafasi ya tatu.

HAWARA WA WA “HOUSGIRL” ATIWA MBARONI AKIHUSISHWA NA MAUAJI YA ANETH MSUYA

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watu wengine wawili, akiwamo mpenzi wa mfanyakazi wa ndani wa Aneth Msuya, aliyeuawa kwa kuchinjwa nyumbani kwake.

Aneth, ambaye ni dada wa Bilionea Erasto Msuya, aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana Mei 26 nyumbani kwake Kibada, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Wauaji hao hawakuchukua chochote kwenye nyumba hiyo. Bilionea Msuya aliuawa Agosti mwaka jana kwa kupigwa risasi na tayari watu 12 wamekatwa, wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo.

Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema hadi sasa wamekamata watuhumiwa wanne wakihusishwa na mauaji ya dada wa bilionea huyo.

Kati ya watuhumiwa waliokamatwa, yumo mume wa Aneth, msaidizi wa ndani wa Aneth na mtuhumiwa mwingine ambaye Kamanda Sirro hakumtaja jina.

“Mwanzo tulimkamata mume wa marehemu na msaidizi wa ndani wa marehemu, lakini sasa wameongezeka wengine wawili, akiwamo hawara wa msaidizi wa ndani. Tunaendelea kuwahoji na upelelezi ukikamilika tutawafikisha mahakamani,” alisema Sirro.

Kwa mujibu wa mama mdogo wa marehemu, Lilian Benjamin, msaidizi wa ndani wa dada wa bilionea huyo aliondoka saa sita mchana na kuacha funguo nyumba ya jirani.

Lilian alisema msaidizi huyo alimpigia simu ghafla bosi wake mchana na kumwambia anaondoka na hataendelea na kazi.

Mauaji ya Aneth ni mwendelezo wa mauaji yanayoikumba familia hiyo ya Msuya baada ya kaka yake, Erasto ambaye alikuwa ni mfanyabiashara tajiri wa madini, kuuawa Agosti 7, 2013 kwa kupigwa risasi zaidi ya 12 kwa kutumia bunduki ya SMG katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.

Februari 10, mawakili wanaosimamia kesi ya Erasto, Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emanuel Safari na John Lundu, waliiambia mahakama kuwa Serikali inakusudia kuita mashahidi 50 kuthibitisha shtaka hilo na kuwasilisha vielelezo 40, ikiwamo bunduki hiyo.

Mawakili hao walidai mipango ya kumuua bilionea Msuya ilianza Julai 26,2013 jijini Arusha, ikiwahusisha washtakiwa na waliotekeleza mauaji hayo wangelipwa Sh5 milioni kila mmoja.

Wakitoa maelezo ya tukio hilo, mawakili hao waliiambia mahakama kuwa washiriki ambao wasingeenda moja kwa moja kwenye mauaji, wao wangelipwa Sh3 milioni kila mmoja.

Mshtakiwa wa kwanza, Shariff Mohamed anadaiwa kuwa ndiye alikuwa mpangaji mkuu na alitoa fedha za maandalizi yote ya mauaji.

Washtakiwa wengine ni Shaibu Jumanne, ambaye anafahamika kwa jina la utani la Mredii, Mussa Mangu, Jalila Zuberi (Said), Karim Kihundwa, Sadick Jabir (Msudani) na Ally Mussa (Mjeshi).

Thursday, 2 June 2016

JWTZ YAJITOSA MAUAJI YA WATU 8 TANGA.......MKUU WA MAJESHI JENERALI MWAMUNYANGE ATANGAZA MSAKO USIKU NA MCHANA


SERIKALI imetuma kikosi maalumu cha ulinzi, kikiongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya kuwasaka watu wanaodaiwa kuwa majambazi ambao wanaendesha mauaji ya kinyama mkoani Tanga.

Uamuzi huo umechukuliwa baada ya watu wanane kuuawa kinyama kwa kuchinjwa juzi usiku katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, Manispaa ya Tanga.

Habari za uhakika ambazo tulizipata jana, zinasema tayari vikosi hivyo vimeanza operesheni kali katika mapango ya Amboni ambayo yanadaiwa kuwa maficho ya watu hao.

Akitoa salamu za rambirambi wakati wa mazishi ya marehemu wanne kati ya wanane waliozikwa Kibatini jana, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema vyombo vya dola vitahakikisha watu wote waliohusika katika mauaji hayo wanatiwa mbaroni.

“Ndugu zangu nawapeni pole kutokana na kuondokewa na wapendwa wetu… naomba kuwahakikisha sisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola tutahakikisha tunawatia nguvuni watu wote waliohusika na mauaji haya,” alisema Jenerali Mwamunyange.

Alisema tukio la mauaji hayo ni la kusikitisha mno kutokana na Tanzania kusifika kuwa nchi ya amani duniani.

“Tanzania inasifika kuwa na amani duniani kote, lazima hatua za kiusalama zichukuliwe haraka ili kunusuru amani yetu isichezewe.

“Ni tukio la ajabu ambalo limegusa watu wengi wasio na hatia, tutasaidiana na wenzetu kuhakikisha wahalifu hawa wanapatikana,”alisema Jenerali Mwamunyange.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Masauni Hamad Masauni, alisema Serikali inaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo ili kuwakamata wahusika ndani ya kipindi kifupi.

Aliwahakikisha wananchi kuwa ulinzi unaimarishwa na kwamba matukio hayo hayatajirudia tena.

“Vyombo vya ulinzi vitafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha tunawatia nguvuni haraka watu waliohusika na mauaji hayo,” alisema Masauni.

Aliwaomba ndugu na jamaa ambao wamefiwa na ndugu zao kuwa na subira wakati Serikali inaendelea kuchukua hatua.

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu alisema wataendelea kuimarisha ulinzi na usalama maeneo yote.

Katika hatua nyingine, wakazi wa mitaa mitatu ya Mleni Kati, Mleni Mashariki na Kibatini katika Kata ya Mzizima, Manispaa ya Tanga, wameanza kukimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wao baada ya mauaji hayo.

Mauaji hayo yalitokea juzi usiku ambapo watu wanaoaminika kuwa majambazi walivamia nyumba tatu katika eneo hilo, wakiwa wamelala usiku, kisha kuwateka na kuwapeleka msituni kabla ya kuwachinja.

Wakazi hao wanaounda zaidi ya kaya 30, walisema wameamua kuyakimbia makazi yao kwa kutokuwa na imani ya usalama wao katika eneo hilo, baada ya wale wanaoitwa majamabzi kuvamia makazi yao kwa mara ya pili kwa staili ya kutisha.

Kabla ya tukio hilo la juzi, watu wasiofahamika walivamia makazi yao na kuchinja kuku 40, mbuzi wanne na ng’ombe mmoja na kukimbilia mapango ya Amboni na hawajawahi kukamatwa.

Mwandishi wetu  jana  alishuhudia wanawake na watoto wakiwa na mizigo mithili ya wakimbizi wakiondoka katika eneo hilo huku wanaume wakibaki kwa ajili ya kuzika ndugu, jamaa na marafiki zao waliouawa katika tukio hilo.

Mmoja wa wananchi hao, Juma Issa, alisema wamelazimika kuwahamisha wanawake na watoto kwa kuhofia wanaweza kuvamiwa tena kwa mara ya pili.

Nae Lucas Muhina alisema kuwa anashindwa kuhama katika eneo hilo kutokana na kuwa na mifugo, hivyo anashindwa kujua mahali salama pa kuihifadhi.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kibatini, Shabani Mwamini, alithibitisha baadhi ya wananchi wa mitaa mitatu kuhama katika eneo hilo.

“Nyumba nyingi zimebaki na wanaume pekee yake kwani wanawake na watoto wote wamehama kwa sasa,” alisema.

Wakati huohuo, maiti nne kati ya nane zimezikwa jana huku nyingine nne zikisafirishwa nje ya mkoa huo.

Mwamini aliwataja waliozikwa kuwa ni Issa Husein, Mkola Husein, Issa Hamis na Salim Adam.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella alisema kuwa vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Simulizi ya Mauaji
Mtoto wa marehemu Mkola Hussein anayeitwa Salimu Mkola (16) alisababisha vilio na simanzi kwa waombolezaji baada ya kusimulia namna watu hao walivyomchukua baba yake na kwenda kumchinja mbele ya nyumba yake.

Akisimulia tukio hilo huku akibubujikwa machozi, mtoto huyo alisema watu hao walifika nyumbani kwao wakagonga mlango saa sita usiku na kumuamrisha baba yao atoke na fedha.

“Nilipoona hivyo nilijaribu kupiga kelele kuomba msaada kwa majirani, lakini mmoja wa wauaji aliingia ndani na kunitoa nje ya nyumba yetu, huku akiniuliza wakati wale vijana saba
wanachukuliwa na polisi mimi nilikuwa wapi.

“Waliendelea kuniuliza kama nina habari ninayoijua, huku wakiwa wameshika mapanga na bunduki, ndipo waliponiambia wapo kwa ajili ya kutetea dini yetu.
 
“Baadaye waliniruhusu niingie ndani na kulala, lakini niliendelea kusikia vishindo vya kipigo na watu wakikoroma ambayo ilikuwa ni ishara ya kuwa baba yangu alikuwa anakata roho pamoja na watu wengine,”alisema.
 
Mtoto mkubwa wa marehemu, Abuu Mkola, alisema vijana saba ambao sasa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi awali walionekana katika Kitongoji cha Kibatini wakiwa wanakimbia kusikojulikana.

Alisema baada ya hali hiyo baba yake ambaye ni marehemu, Mkola Hussein akishirikiana na wananchi wa mtaa huo walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambao walikuja na kuwakamata vijana hao lakini mmoja wao alifanikiwa kukimbia.
 
Abuu alisema kuwa katika tukio la juzi, wauaji hao wakati wanamchukua baba yake walisema wanawahitaji vijana wao saba waliokamatwa na polisi, lakini aliposema hajui ndipo walimuunganisha na watu wengine kwa ajili ya kumchinja.

Bunge Lataka Taarifa
Ofisi ya Bunge imeiagiza Serikali kutoa taarifa rasmi kuhusu mauaji yanayoendelea nchini ili kuwatoa hofu wananchi waliopo katika maeneo mbalimbali.

Akitoa maagizo hayo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson alisema Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni anapaswa kuzungumza na Kamati za Ulinzi na Usalama katika maeneo yote ambayo yametokea mauaji ili aweze kutoa taarifa ndani ya Bunge.

“Waziri atuletee taarifa kwa sababu Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) yupo hapa na waziri anayehusika na mambo ya Bunge yupo, naomba watuletee taarifa kwa sababu mauaji yamekuwa yakitokea mara nyingi na tumekuwa tukiwasihi Serikali ituletee taarifa na si mtakuwa mnazitafuta,” alisema Dk. Tulia.

Baada ya maelezo hayo Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alisimama na kuomba mwongozo chini ya kanuni 68 (7).

“Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na haya uliyoyatolea maelezo juu ya mauaji yanayotokea katika nchi yetu, nimelazimika kuomba mwongozo huu kwa sababu matukio yaliyoanza kujitokeza katika maeneo mbalimbali na maeneo mengine mambo haya tuliwahi kuyauliza Serikali na kuahidi watayatolea ufafanuzi.

“Sasa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani  amekwenda kuangalia na atazungumzia jambo hilo wakati mambo haya wabunge tulishaiomba Serikali itoe ufafanuzi ni jinsi gani inajipanga kukabiliana nayo,” alisema Lugola.

Alisema kitendo cha Serikali kusema Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amekwenda kushughulikia jambo hilo wakati huo huo mambo ambayo yametokea Mwanza na maeneo mengine yalishaombewa ufafanuzi lakini hakuna majibu si kizuri.

Friday, 27 May 2016

DADA WA BILIONEA MSUYA AUAWA KINYAMA DAR


Mtumishi wa Wizara ya Fedha, Aneth Msuya (30) ambaye ni mdogo wa Bilionea Erasto Msuya aliyeuawa kwa kupigwa risasi 22 KIA, ameuawa kwa kuchinjwa nyumbani kwake eneo la Kigamboni jijini Dar Es Salaam.

Mmoja wa ndugu wa familia hiyo, Shujaa Khamis, jana alithibitisha kuuawa kwa Aneth, lakini alikataa kuingia kwa undani.

“Ni kweli wamemchinja usiku wa kuamkia leo (jana) na hapa nipo kwenye msiba hapa nyumbani (Mererani) kwa baba. Tumeambiwa wamechukua Tv tu,” alisema.

Hata hivyo, Khamis alikataa kueleza lolote kama wana mashaka na mauaji hayo zaidi ya kuliomba Jeshi la Polisi nchini, kuchunguza kiini cha mauaji hayo na kuwasaka waliohusika.

Habari nyingine kutoka Wizara ya Fedha, ziliwakariri baadhi ya watumishi wakisema wamepata taarifa za msiba huo, lakini hawajapewa taarifa rasmi.

“Tuna taarifa tunazisikia sikia kuwa ameauawa, lakini jana (juzi) tulikuwa naye kazini ila leo (jana) ndiyo tunasikia amechinjwa na watu wasiojulikana. Imetusikitisha sana,” alisema mmoja wa watumishi hao ambaye hakutaja jina kwa kuwa si msemaji.

Kamanda wa mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Andrew Satta alipofutwa jana kuthibitisha taarifa za mauaji hayo alisema yuko kwenye kikao.

Wednesday, 25 May 2016

14 WAKAMATWA MAUAJI YA WATU WATATU MSIKITINI JIJINI MWANZA


Jeshi la Polisi Nchini linawashikilia watuhumiwa 14 kufuatia tukio la mauaji ya watu watatu lililotokea katika msikiti wa Rahman eneo la Ibanda relini mkaoni Mwanza, Mei 18 mwaka huu.

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Kamishna Msaidizi Advera Bulimba alisema kuwa msako wa kuwakamata watuhumiwa wengine unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Hivyo amewaomba wananchi kutoa ushirikiano mkubwa kwa jeshi hilo ili kufanikisha kuwakamata wale wote wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo.

“Nitoe wito kwa wananchi kushirikiana kikamilifu na vyombo vya usalama katika kufichua wahalifu kwa kuwa ni watu tunaoishi nao, hivyo hakuna budi kutoa taarifa zao ili usalama na mali zetu uendelee kuimarika”, aliongeza Kamishna Msaidizi Bulimba.

Hata hivyo, alieleza kuwa hali ya usalama nchini iko shwari na kuwatoa hofu wananchi kwamba jeshi hilo limejipanga kikamilifu katika kuhakikisha hali ya usalama inaendelea kuwepo.

“Niwaombe wananchi kuondoa hofu juu ya hali ya usalama na wasiwasi na watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuhakikisha kwamba wote wanaojihusisha na uhalifu wanakamatwa haraka”, alisema Kamishna Msaidizi  Bulimba.

Aliongeza kuwa uchunguzi zaidi wa matukio ya uhalifu nchini unaendelea ikiwemo matukio ya mkoani Tanga, Dar es Salaam na mikoa mingine ili kubaini na kuwakamata wahusika na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Hivi karibuni kumeripotia matukio mbalimbali ya uvunjifu wa amani katika mikoa mbalimbali  ikiwemo mauaji ya watu watatu waliouawa wakiwa msikitini jijini Mwanza.

Sunday, 22 May 2016

MUFTI WA TANZANIA ALAANI KITENDO CHA MAUAJI YALIYOTOKEA MKOANI MWANZA


 Shekhe Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mufti wa Tanzania, Aboubakar Zubeir (Mwenye kofia Nyeupe katikati) akiwa na viongozi mbalimbali wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
SHEKHE Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mufti wa Tanzania, Aboubakar Zubeir pamoja amelaani vikali tukio la kinyama lililotokea Mei 17 mwaka huu katika Msikiti wa Ibanda Mkolani, Masjid Rahmaan mkoani Mwanza. 
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo amesema kuwa  kitendo hicho kuwa ni cha kinyama na hakivumiliki.Tukio hilo lilitokea May 17 mwaka huu na kusababisha mauaji ya waumini watatu wa Msikiti wa Ibanda Mkolani waliokuwa katika Ibada  miongoni mwao akiwa ni Imam wa Msikiti huo ikiwa na wengine kujeruhiwa.
"Kwaniaba ya Baraza kuu la Waislam wa Tanzania(Bakwata) tunalaani vikali tukio hili pamoja na kuwataka Waislam wawe watulivu katika kiindi hiki kigumu" Amesema Shekhe Zuberi.Amewaomba Waislam na wananchi kwa ujumla kuvipa ushirikiano wa hali na mali vyombo vya usalam ili hatimae kuwapata waharifu hao ili waweze kufikishwa katika vyombo vya Sheria.



Shekhe Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mufti wa Tanzania, Aboubakar Zubeir akizunumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, na kulaani kitendo cha mauaji ya watu wasio na hatia katika Msikiti huko Mkoani Mwanza. Kulia ni Msaidizi katika ofisi ya Mufti Mkuu wa Tanzania Shekhe, Ally Khamisi Ngeruko. na Kushoto ni Shekhe, Abuubakari Kharid.
Baadhi ya waamini wa dini ya Kiislamu pamoja na waandishi wa habari wakimsikiliza Shekhe Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mufti wa Tanzania, Aboubakar Zubeir jijini Dar es Salaam leo.

Picha na Avila Kakingo, Globu ya Jamii.

Thursday, 19 May 2016

WATU WATATU WAUAWA KWA KUKATWA MAPANGA NA MASHOKA JIJINI MWANZA


Mnamo tarehe 18.05.2016 majira ya saa 20:30hrs katika msikiti wa masjid rahman uliopo ibanda relini mtaa wa utemini @ mapankini kata ya mkolani wilaya ya nyamagana jiji na mkoa wa mwanza. 

Watu wasiozidi 15 wakiwa wamevalia mavazi ya kuficha uso wakiwa na mapanga, shoka na bendera nyeusi yenye maandishi meupe waliingia ghafla katika msikiti tajwa hapo juu wakati waumini wa msikiti huo wakiwa wanaswali na kuzima taa na kutoa sauti wakisema “kwa nini mnaswali wakati wenzetu wamekamatwa na wanashikiliwa na polisi ?” na hapo hapo wakaanza kuwakata kwa mapanga baadhi ya waumini katika sehemu mbalimbali za miili yao. 

Walipata majeraha makubwa kichwani, shingoni na mikononi na walipoteza maisha yao papo hapo na mmoja kupata majeraha sehemu za kichwani na kukimbizwa hospitali ya wilaya ya nyamagana (butimba). 
 
Waliouawa, 1. Feruz ismail elias  mika 27, muha imamu wa msikiti huo na mkazi wa ibanda relini, 2. Mbwana rajab miaka 40, mbondei mfanyabiashara na mkazi wa ibanda, 3. Khamisi mponda miaka 28 dereva wa kiwanda cha samaki (TFP), mkazi wa mkolani, wote walijeruhiwa sehemu za kichwani, shingoni na mikononi. 

Aliyejeruhiwa ni ismail abeid @ ghati miaka 13, mkurya mwanafunzi wa madrasa katika  shule ya kiislamu itwayo jabar hila iliyoko maeneo ya Nyasaka aliyepata majeraha kichwani na anapata matibabu hospitali ya Nyamagana.
 
Kutokana na hali hiyo, waumini wengine walifanikiwa kukimbia huku wakipiga mayowe yaliyopelekea wahalifu hao kukimbia na kurusha ndani ya msikiti chupa mbili za konyagi zilizokuwa na petroli na tambi za moto, chupa moja ililipuka lakini haikuleta madhara makubwa.
 
Jeshila la polisi  limewakamata washukiwa watatu kwa ajili ya kuwahoji kuhusiana na tukio hilo, huku msako mkali wa kuwasaka watu wengine walio husika kwa namna moja au nyingine kwenye mauaji hayo ukiwa bado unaendelea. 

Napenda kuwaeleza  wananchi watulie wakati tukiendelea na upelelezi wa tukio hili, na natoa wito kwa wananchi kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za wahalifu wa mauaji hayo ili tuweze kuwakamata. 

Pia nashauri na kusisitiza kuwepo na kamati za ulinzi na usalama katika nyumba za ibada, kumbi za starehe pamoja na mitaa yao. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo hayo.

Imesainiwa na:
……………………….
Sacp: Ahmed Msangi
Kamanda wa Polisi (m) Mwanza.

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA